Rais Dkt. Magufuli Azungumza na Madiwani , Watumishi Chato Mkoani Geita. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Friday, August 31, 2018

Rais Dkt. Magufuli Azungumza na Madiwani , Watumishi Chato Mkoani Geita.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Baraza la  Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato mara baada ya kumaliza mkutano huo na Madiwani, Viongozi mbalimbali pamoja na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato. Wengine katika picha ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Christian Manunga wapili kutoka (kulia) mstari wa kwanza mbele, Mkuu wa Wilaya ya Chato Eng. Mtemi Msafiri Semeon watatu kutoka (kulia), Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani, wanne kutoka (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chato Eliud Mwaiteleke.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wote nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria sambamba na kuhakikisha wanasimamia ipasavyo matumizi ya rasilimali za umma kwa maslahi ya wananchi.

Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo tarehe 30 Agosti, 2018 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, wakati akizungumza na Viongozi na Wafanyakazi wa wilaya hiyo, ambapo amesisitiza kuwa viongozi wote wajenge utaratibu wa kusoma sheria na kujiepusha kutumiwa kwa maslahi ya watu binafsi.

Huku akitolea mfano wa mgogoro wa makontena yanayodaiwa kuwa na fenicha za shule, na yanayoshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika bandari ya Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli amesema makontena hayo yanapaswa kulipiwa kodi kwa mujibu wa sheria, huku akisisitiza kuwa Waziri wa Fedha na Mipango ndiye mwenye dhamana ya kupokea misaada kwa niaba ya Serikali na sio Mkuu wa Mkoa.

Kwa mujibu wa sheria ya Madeni, Dhamana na Misaada Namba 30 ya mwaka 1974 (kama ilivyorekebishwa na sheria namba 9 ya mwaka 2003) kifungu cha 3, 6, 13 na 15, Waziri wa Fedha na Mipango ndiye mwenye mamlaka ya kukopa nje na ndani, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali.

“Kwa msingi huo, hakuna mtu yoyote mwenye mamlaka ya kukopa, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali bila mtu huyo kukasimiwa mamlaka hayo na Waziri wa Fedha kwa mujibu wa sheria hiyo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka Madiwani wa halmashauri zote hapa nchini kuhakikisha wanasimamia kwa ukaribu matumizi ya fedha za bajeti ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha hizo zinaelekezwa katika miradi na huduma zenye kujibu kero na kuboresha maisha ya wananchi badala ya kuacha zikitumiwa kulipana posho za vikao na safari zisizo na tija.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono Madiwani pamoja na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato wakatika akiondoka katika Ofisi za Halmashauri hiyo Chato mkoani Geita. 

Kuhusu uhaba wa watumishi, Mhe. Rais Magufuli amesema baada ya Serikali kuokoa Shilingi Bilioni 138 zilizokuwa zikilipwa kwa watumishi hewa na wenye vyeti feki, sasa imeanza kuajiri watumishi ambapo watumishi 52,000 wanaajiriwa na kwamba sambamba na hilo katika kipindi kifupi kijacho itaanza kulipa madeni ya watumishi baada ya uhakiki kukamilika.

Amewaagiza viongozi wa wilaya ya Chato ambao wamesikiliza kero za wafanyakazi na Madiwani akiwemo Mbunge wa Jimbo hilo na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani kufanyia kazi kero zote zilizo ndani ya uwezo wao.

SOMA HAPA TAARIFA ZAIDI.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad