|
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Bi.Chiku Gallawa akizungumza na Mafundi wanaojenga Kituo cha Afya Isansa Wilaya ya Mbozi, kituo hicho cha Afya kimepokea
shilingi milioni 500 kwa ajili ya upanuzi wa Miundombinu ya Majengo.
Grace
Gwamagobe-Songwe.
Mkuu wa Mkoa
wa Songwe Bi.Chiku Gallawa amesema atahakikisha anasimamia kwa ukaribu fedha
zilizotolewa na serikali Mkoani hapa kwa ajili ya upanuzi wa vituo vya afya ili
zifanye kazi zaidi ya ile iliyopangwa awali kutokana na kuongezeka kwa nguvu za
wananchi.
Bi.Gallawa
ameyasema hayo mapema jana wakati wa ziara yake Wilaya ya Mbozi alipokagua
maendeleo ya upanuzi wa vituo vya afya vya Isansa kilichopokea milioni 500 na
kituo cha Afya cha Iyula Kilichopokea milioni 400, kwa ajili ya ujenzi wa
maabara, nyumba ya daktari, chumba cha upasuaji, jengo la mama na mtoto na
chumba cha kuhifadhia maiti.
“Fedha hizi
lazima zifanye kazi iliyopangwa vizuri na pia tuongeze kazi nyingine ya ziada
kutokana na kuwa tumepata nguvu ya wananchi lakini pia mafundi wetu hawa
tunaowatumia ni wazawa na wenyeji wa maeneo ya kwetu kwahiyo gharama zao
zitatupa unafuu ambao tunatakiwa kuutumia kuongeza kazi nyingine”, amesema
Bi.Gallawa.
Ameongeza
kuwa licha ya upanuzi wa vituo vya afya kuchelewa kuanza bado ana Imani kuwa
wataweza kumaliza ndani ya muda uliopangwa kutokana na uchapakazi wa mafundi
wazawa wa maeneo hayo.
Bi.Gallawa
amesema kukamilika upanuzi wa vituo hivyo vya afya kutavifanya vituo hivyo
vivutie na hata mgonjwa akifika apate matumaini ya kupona na sio kukatishwa
tamaa na hali mbovu ya mazingira.
|
|
Mkuu wa Mkoa
wa Songwe Chiku Gallawa akizungumza na baadhi ya watendaji na wananchi wa
kijiji cha Iyula waliojitokeza katika eneo la ujenzi katika kituo cha Afya cha
Iyula Wilaya ya Mbozi, kituo hicho cha Afya kimepokea shilingi milioni 400 kwa
ajili ya upanuzi wa kituo hicho.
Aidha
Gallawa amemtaka Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi Lauteri
Kanoni kuhakikisha anaweka mfumo wa maji safi katika vituo hivyo hasa mfumo wa
kuvuna maji ya mvua ili vituo vikikamilika maji yawepo kwa ajili ya matumizi.
Naye Mkazi
wa kijiji cha Isansa Wilaya ya Mbozi Bi.Stela Mkeya ameonyeshwa kufurahishwa na
upanuzi wa kituo cha Afya Isansa huku akieleza baadhi ya kero walizokuwa
wakizipata awali.
“Tunaishukuru
sana serikali ya Magufuli kwakweli wametusaidia, tulikuwa tunapata shida
kufuata huduma za upasuaji wa akina mama wajawazito huko hospitali ya Wilaya
iliyopo Vwawa lakini pia hapa kwenye kituo cha afya mzazi akijifungua hata
mazingira ya kwenda kujisafisha vizuri kama vile mabafu yakiwa hayatoshi
kabisa”, ameeleza Bi.Mkeya.
Kwa upande
wao mafundi waliokabidhiwa kazi ya upanuzi wa vituo hivyo vya Afya wameonyesha
ari ya kufanya kazi hiyo kwa ufanisi na haraka huku wakimuomba Mkuu wa Mkoa
Bi.Chiku Gallawa awasaidie upatikanaji wa taa ili waweze kufanya kazi mchana na
usiku naye Mkuu wa Mkoa amekubaliana na mapendekezo hayo.
|





No comments:
Post a Comment