JWTZ laanza Utekeleza agizo la Rais Magufuli Mererani. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Friday, September 22, 2017

JWTZ laanza Utekeleza agizo la Rais Magufuli Mererani.

Meja Jenerali Michael Isamuhyo akisalimiana na viongozi wa Wilaya ya Simanjiro na wananchi mara baada ya kutua katika uwanja wa wazi wa Mererani, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara tayari kwa kukagua eneo litakalojengwa uzio kuzunguka kitalu A hadi D katika eneo la Madini la Tanzanite Mererani ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Meja Jenerali Michael Isamuhyo akipenya kwenye vichaka wakati wa kukagua eneo litakalojengwa ukuta. 

Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania JWTZ limeanza kutekeleza agizo  la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyelitaka kujenga uzio wa kuzunguka kitalu A hadi D katika eneo madini ya tanzanite, Mirerani Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara ili kudhibiti uchimbaji na biashara ya madini hayo.

Dk Magufuli September 20,2017 aliiagiza JWTZ kwa kushirikiana na Shirika la Uchumi la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) kuanza mara moja kujenga uzio kwenye eneo la kitalu A hadi D lililopo eneo la Simanjiro ambalo kunapatikana madini ya kipekee ya tanzanite. Aidha, aliagiza kufungwa kwa kamera maalumu, kuweka fensi maalumu na kutakuwa na eneo moja la mlango wa kutokea na kuingia ili kubaini wezi wanaoiba madini hayo.

Jana September 21,2017, Meja Jenerali Michael Isamuyo akiwa na wataalamu wa JWTZ, wamefika Mirerani kwa helikopta na kisha kukagua eneo lenye vitalu vya tanzanite wakiwa angani na baadaye wakatua na kukagua wakiwa ardhini kwa kutumia magari na kutembea kwa miguu. 

Akizungumza baada ya kutua kwenye uwanja wa wazi wa Mererani, Meja Jenerali Isamuyo alisema JWTZ imeanza kutekeleza agizo la Rais na Amiri Jeshi Mkuu mara moja na ipo tayari kukamilisha kazi kama ilivyokusudiwa.

Meja Jenerali Isamuyo alisema baada ya kutembea kwa miguu katika eneo la vitalu A hadi D, amebaini kuwa eneo linalopaswa kujengwa uzio huo ni la kawaida na ametaka wananchi watoe ushirikiano wa kutosha wakati wa ujenzi wa uzio huo.

 Alionya kuwa wakati wa utekelezaji wa jukumu hilo, JWTZ haitarajii kukwamishwa na mtu yeyote na haitakuwa tayari kukwamishwa kwa namna yoyote. 

Baadhi ya viongozi wa Chama cha Wachimbaji wa Madini wa Mkoa wa Manyara waliokuwepo wakati Meja Jenerali Isamuyo akitua na akikagua eneo la vitalu vya tanzanite, walimpongeza Rais Magufuli kwa kuagiza kujengwa kwa uzio huo na wameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha wakati wa ujenzi huo.

Meja Jenerali Michael Isamuhyo akioneshwa ramani ya vitalu A hadi D katika eneo la madini ya Tanzanite huko Mererani.
Meja Jenerali Michael Isamuhyo akisalimiana na baadhi ya wakazi wa eneo la Mererani,mara baada ya kutua katika uwanja wa wazi wa Mererani, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara

Helkopta iliyombeba Meja Jenerali Michael Isamuhyo ikitua katika uwanja wa wazi wa Mererani, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara tayari kwa kukagua eneo litakalojengwa uzio kuzunguka kitalu A hadi D katika eneo la Madini la Tanzanite Mererani ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad