Maelfu wahudhuria ibada ya kuaga Wanafunzi wa Lucky Vicent-Arusha. - Mwana Wa Makonda

Breaking

Post Top Ad

Monday, May 08, 2017

Maelfu wahudhuria ibada ya kuaga Wanafunzi wa Lucky Vicent-Arusha.

Mmoja wa waliohudhuria ibada hiyo akifarijiwa. 

Maelfu ya watu leo,May 8, 2017 wamejitokeza kuhudhuria ibada ya pamoja kuwaaga wanafunzi 32 wa shule ya Lucky Vicent waliofariki dunia ajalini Jumamosi,May 6, 2017 asubuhi.

Majeneza 35 yenye miili ya waliofariki yalifikishwa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, kwa ibada ya mwisho ya kuwaaga waliofariki kabla ya kufanyika mazishi sehemu tofauti.

Shughuli nyingi mjini Arusha zilisimama leo na hata maduka na biashara zingine kufungwa huku watu wengi wakifika uwanjani kuhudhuria ibada hiyo.

Baadhi ya watu waliofika kuomboleza walipoteza fahamu hivyo kupewa huduma ya kwanza huku wengine wakikimbizwa hospitalini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Bi Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa viongozi wakuu serikali waliohudhuria ibada hiyo.

Katika hotuba yake kwa wananchi waliojitokeza kwa wingi katika tukio la kuaga miili hiyo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amewahakikishia waombolezaji kuwa Serikali ipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu na chenye majonzi mazito kwa kuondokewa na wapendwa wao.

Amehimiza wananchi kote nchini kuungana katika msiba uliotokea kwa kuwafiriji wafiwa katika kipindi hiki kigumu na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali peponi.
Majeneza yakiwa kwenye meza maalum .

Makamu wa Rais pia ameiagiza Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, Jeshi la Polisi nchini,walimu, wazazi na walezi wawe makini katika kuhakikisha kuwa sheria za usalama barabarani zinazingatiwa kwa kuchukua hatua stahiki za kulinda watoto hasa wanapotumia vyombo vya moto kwenye shughuli zao za kimasomo.

Amesema hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuepusha matukio ya ajali ambayo yanaweza kuzuilika kote nchini.

Makamu wa Rais amewataka madereva nchini kuzingatia sheria za usalama barabarani na waache kutumia pombe na dawa za kulevya ili kuepukana na ajali ambazo zinagharimu maisha ya wananchi.

Makamu wa Rais pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta na Wakenya kwa ujumla kwa kuungana na Wananchi wa Tanzania katika msiba uliotokea.

Rais Magufuli kupitia ujumbe kwenye Twitter, ameelezea, jinsi alivyopatwa na huzuni kutokana na ajali hiyo.

"Nimepatwa na uchungu na majonzi makubwa ninapoyaona majeneza ya watoto na walezi wao waliopoteza maisha katika ajali ya basi huko Arusha. Tumewapoteza mashujaa wetu katika elimu," amesema.


Majeneza yakitolewa kwenye lori na wanajeshi wa JWTZ.

Waziri wa elimu wa Kenya Dkt Fred Matiang'i, mmoja wa wageni kutoka nje ya Tanzania waliohudhuria ibada hiyo, amewapa pole Watanzania kwa msiba huo.

"Kenya itaendelea kuwa pamoja nanyi kwenye kipindi hiki kizito cha msiba huu mzito uliowafika. Msiba huu si wa Tanzania peke yake ni wa wote hata kwetu Kenya Rais Kenyatta na mkewe wanawapa pole sana na kuwaombea," amesema.
Baadhi ya waliohudhuria ibada hiyo wamezidiwa na huzuni .

Wanafunzi hao wa darasa la saba walifariki dunia pamoja na walimu 2 na dereva wa gari la shule hiyo ya msingi ya Arusha baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali katika eneo Rhotia Marera, Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.

Wanafunzi na walimu hao walikuwa wakitoka shuleni kwao kwenda shule ya msingi iitwayo Tumaini kwa ajili ya kufanya mtihani wa ujirani mwema na walipofika katika eneo la Rhotia Marera basi walilopanda liliacha njia na kisha kutumbukia korongoni.

Wanafunzi watatu walijeruhiwa.

Rais Magufuli, akituma salamu za rambirambi Jumamosi alisema „ajali hiyo imezima ndoto za watoto waliokuwa wakijiandaa kulitumikia taifa na imesababisha uchungu, huzuni na masikitiko makubwa kwa familia za marehemu na Taifa kwa ujumla."

"Muhimu kwa sasa tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali pema, majeruhi wapone haraka na wote walioguswa na msiba huu wawe na moyo wa subira, ustahimilivu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu."

Post Bottom Ad