Mwenyekiti
wa kamati ya Bunge ya mambo ya nje, Ulinzi na usalama, Katiba na sheria Mtandao na Mbunge wa Muheza Mhe. Balozi Adadi
Rajabu katika picha ya pamoja na baadhi ya wabunge na wadau kutoka asasi za
kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera ihusuyo usalama barabarani
Tanzania.
MTANDAO WA
WADAU KUTOKA ASASI ZA KIRAIA U NAOTETEA MAREKEBISHO YA SHERINA SERA IHUSUYO
USALAMA BARABARANI TANZANIA.
TAMKO LA
HABARI.
Mtandao wa
wadau kutoka asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera ihusuyo
usalama barabarani Tanzania siku ya tarehe 26 na 27 Januari, 2017 wamefanikiwa
kukaa na baadhi ya wabunge kutoka kamati ya mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama,
Katiba na Sheria pamoja na miundo mbinu katika kikao kilichoongozwa chini ya
mwenyekiti wake Mbunge wa Muheza Mheshimiwa Balozi Adadi Rajabu, pamoja
walionyesha ushirikiano wao katika kuboresha usalama bararani kwa maendeleo ya
Taifa letu.
Wajumbe wa
kikao husika walipata nafasi ya kusikiliza
mada mbalimbali kuhusiana na masuala ya usalama barabarani na hali
ilivyo sasa, ambapo ilielezwa kuwa hali ilivyo kulingana na takwimu
zinaonyesha kuwa takribani watu milioni
1.25 hufariki dunia kila mwaka kutokana na
ajali za barabarani, aidha, watu
milioni 20 hadi 50 hujeruhiwa na wengine hupata ulemavu wa kudumu wengi wao
wakiwa ni vijana wenye nguvu kazi ya Taifa. Hii ni kutokana na takwimu za
Shirika la Afya Duniani (WHO) 2015.
Kwa upande
waTanzania Bara, taarifa kutoka jeshi la polisi Kikosi cha Usalama Barabarani inaonyesha kwamba, kwa mwaka 2016 jumla ya watu 3,256 walipoteza maisha
kutokana na ajali za barabarani.
Katika
vifo hivyo wanaume ni 2,580 na wanawake
ni 676. Aidha kumekuwa na majeruhi 8,958
kati yao wanaume ni 6,470 na wanawake 2,488.
Wakati vyombo vya moto
vilivyoongoza katika ajali ni magari binafsi ambayo idadi yake 3,649 ikifuatiwa
na pikipiki kwa idadi ya 2,544.
Kutokana na
idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani nchini, Mtandao wa
wadau kutoka asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera zinazohusu
usalama barabarani Tanzania umeona umuhimu na kuchukulia jambo hili kulifanyia
kazi kwa kina. Tafiti zinaonyesha kwamba asilimia 76 ya ajali zote zinatokana
na vyanzo vya kibinadamu kama vile Ulevi, Mwendokasi, Uzembe, Uchovu, kupuuzia
au kutokuwa makini uwapo barabarani na kutokutii sheria za Usalama Barabarani.
Tuna amini matendo haya ya kibinaadamu yana dhibitika kisheria, hivyo basi
tunaisihi serikali kuboresha sheria.
Kama wadau
wa Usalama Barabarani, tunadhani kuna umuhimu wa sheria sasa kuboreshwa, na
hivyo utashi wa kisiasa unatakiwa.
Ndiyo
maana tukaitisha majadiliano ya pamoja na Wabunge pamoja na wadau mbalimbali wa
Usalama Barabarani ili kuona ni kwa namna gani tunaweza kuleta mabadiliko ya
sheria kwa ufanisi na kwa haraka.
Wabunge
waliohudhuri kikao hiki kwa ujumla wao,
waliona umuhimu wa kuwa na mikakati ya kitaifa ya kupunguza ajali na
walikiri kwa nia moja na kukubali kuunda Mtandao wa Wabunge wanaotetea usalama
barabarani.
Maeneo ambayo tunayapa kipaumbele katika
maboresho ya sheria ni kama haya yafuatayo:
a) Matumizi ya mikanda; Sheria ya sasa
ya Usalama barabarani inasema ni kosa kisheria kwa dereva na abiria anayekaa
kiti cha mbele kutokufunga mkanda wakati wa safari lakini sheria hiyo hiyo
haisemi chochote kwa abiria wanaokaa kiti cha nyuma.
Utafiti
uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) unasema kuwa iwapo ajali ikitokea
madhara/athari kwa abiria wa kiti cha mbele itapungua kwa 50% na kwa abiria wa
nyuma madhara yatapungua kwa 70%.
Kanuni zilizotungwa na SUMATRA zinataka
abiria wote wafunge mkanda ila kwa vile sheria mama (Road Traffic Act of 1973)
ipo kimya katika eneo hili utekelezaji wa kanuni unakuwa mgumu.
Hivyo basi
ni rai yetu sheria hiyo ibadilishwe na kuwataka abiria wote wanaokuwa katika
chombo cha usafiri wa kibiashara au binafsi kufunga mkanda wakati wote wa
safari.
b) Matumizi sahihi ya kofia ngumu; Sheria
ya sasa ya usalama barabarani inasema kuwa ni kosa kwa muendesha pikipiki kutokuvaa
kofia ngumu wakati wa kuendesha chombo hicho.
Lakini sheria hiyohiyo haisemi
chochote kwa abiria anayepanda katika chombo hicho.
Vilevile
pamoja na kuanisha kosa kwa dereva wa pikipiki kutokuvaa kofia ngumu lakini pia
sheria haielezi ni jinsi gani kofia inatakiwa kuvaliwa na aina maalum ya kofia
inayotakiwa kuvaliwa.
Kwa mujibu
wa Utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO)
unaonyesha kuwa iwapo ajali itatokea madhara yanayotokea kwa kutovaa
kofia maalum na kwa usahihi ni makubwa sana ukilinganisha na kofia hiyo
ikivaliwa kwa usahihi.
Hivyo basi
ukizingatia kuwa sasa hivi usafiri wa pikipiki umekuwa unatumika kwa kiasi
kikubwa (public transport) hivyo ni rai yetu sheria hiyo ifanyiwe maboresho na
kuweka kuwa ni sheria kwa mtu yoyote anayepanda pikipiki kuvaa kofia ngumu na
kwa usahihi.
c) Ulevi: Sheria ya sasa ya usalama
barabarani inasema kuwa itakuwa kosa kwa mtu yoyote kuendesha chombo cha moto
akiwa na kiwango cha kilevi katika damu yake kinachozidi asilimia 0.08% katika
mfumo wa mwili.
Kiwango hiki ni kikubwa sana kikilinganishwa na tafiti
zilizofanywa na Shirika la Afya Duniani na kupendekeza kiwango cha asilimia
0.05% kwa dereva aliyebobea (experienced driver) na asilimia 0.02% kwa
dereva mchanga (young driver).
Hivyo
basi ni rai yetu kuwa sheria ifanyiwe marekebisho ili iendane na kiwango cha
sasa cha kimataifa kilichofanyiwa utafiti.
d) Mwendo kasi (Speeding): Mwendokasi
umeendelea kuwa sababu kubwa ya ajali zinazogharimu uhai wa watu wengi.
Sheria
yetu inayo mapungufu kadhaa pamoja na juhudi nyingi za Jeshi la Polisi na wadau
wengine kutaka kudhibiti jambo hili limeendelea kuwa tatizo.
Adhabu zisizokidhi
wala kuleta hofu kwa maderava wasiotaka kutii zimeendelea kufifisha juhudi za
kudhibiti tatizo hili.
Tunatoa wito
kwa watunga sera kushirikiana zaidi na wadau kuuelimisha umma katika eneo la
uhusiano wa adhabu zitokanazo na makosa ya usalama barabarani na ongezeko la
ajali. Pia sheria kufanyiwa maboresho na kuangalia kwa upya mianya iliyopo.
TAMKO HILI
LIMETOLEWA LEO NA MTANDAO WA WADAU KUTOKA ASASI ZA KIRAIA:
1. TAWLA
2. TAMWA
3. WLAC
4. TCRF
5. TLS
6. TMF
7. RSA
8. AMEND TANZANIA
9. SHIVYAWATA
10. TABOA &
11. SAFE SPEED FOUNDATION
|
Tuesday, January 31, 2017
Home
HABARI
Mapendekezo ya Maboresho ya Sheria ya Usalama Barabarani kwa mtazamo wa visababishi vitano vya Ajali.
Mapendekezo ya Maboresho ya Sheria ya Usalama Barabarani kwa mtazamo wa visababishi vitano vya Ajali.
Tags
# HABARI
Sambaza Hii
Chief Editor | Mhariri
HABARI
Labels:
HABARI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Kuhusu Mwandishi
Journalist / Chief Editor / Tanzanian Blogger
Simu: 0756830214 / 0620197747 / 0789925630.
No comments:
Post a Comment