|
Mwanamke
mmoja (jina linahifadhiwa) anayedaiwa ni
mke wa mtu, amefariki dunia katika nyumba ya kulala wageni katika Manispaa ya
Bukoba, akiwa na mwanaume mwingine anayesemekana ni hawara yake.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo
na kueleza kuwa, watu hao walienda katika nyumba hiyo ya kulala wageni iliyopo
eneo la Hamugembe Januari 3, mwaka huu na kuchukua chumba namba nane.
Alisema siku
iliyofuata saa 6:00 mchana, polisi walipokea taarifa kutoka kwa wahudumu wa nyumba
hiyo ya kulala wageni kuwa katika chumba hicho kuna watu waliingia jana yake
lakini hadi muda huo mlango wa chumba ulikuwa haujafunguliwa na kuna ukimya
uliowatia hofu.
Alisema
wahudumu hao waliambatana na polisi na walipofika eneo la nyumba hiyo walimkuta
mmiliki wake ambaye alitoa funguo za akiba na kufungua chumba hicho.
“Polisi
walipofungua chumba walikuta godoro liko chini lakini kitandani lilipopaswa
kuwa kulikuwa na mwili wa mwanamke ukiwa umefunikwa shuka na kuuchukua kwenda
kuuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera,” alisema.
Kamanda huyo
wa polisi mkoa wa Kagera, alisema mtu aliyekuwa pamoja na mwanamke huyo (jina
linahifadhiwa) ambaye ni dereva wa basi la abiria linalofanya safari zake kati
ya Bukoba na Mwanza, hakukutwa katika chumba hicho na alifunga mlango kwa nje
na kuondoka na funguo.
Hata hiyo,
alisema chanzo cha kifo hicho hakijajulikana lakini kutokana na taarifa
walizopata kutoka kwa msaidizi wa dereva huyo wamefanikiwa kumpata mtu
aliyejitambulisha kuwa ni mume wa marehemu.
Kamanda
Ollomi aliongeza kusema kuwa, mume wa
marehemu mkazi wa Butimba, jijini Mwanza, amepatikana na kukabidhiwa mwili wa
mkewe, huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea na kwamba wafanyakazi wawili wa
nyumba hiyo ya kulala wageni wanashikiliwa na polisi kwa upelelezi zaidi lakini
pia kwa kitendo cha kuficha taarifa za wageni wanaolala katika nyumba hiyo.
Papo kwa Papo >>>> Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga na mimi hapa…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp .
|
No comments:
Post a Comment