|
Waziri Mkuu
wa Tanzania,Kassim Majaliwa amewaasa raia wanaokimbia nchi zao na kupata hifadhi Tanzania
kutobeba silaha wanapoingia nchini kuja kuishi kwenye kambi za wakimbizi.
Ametoa onyo
hilo jana wakati akizungumza na mamia ya
wakimbizi wanaoishi kwenye kambi za Nyarugusu na Nduta zilizoko wilayani Kasulu
na Kibondo, mkoani Kigoma waliofika kumsikiliza kwenye mikutano ya hadhara
iliyofanyika kwenye kambi hizo.
“Ninawasihi
mjitambue kuwa mmehama kutoka DRC na Burundi, na mnapoingia hapa inabidi
mbadilike muwe na tabia za hapa. Hatuhitaji mje na silaha au vifaa hatarishi
kwa sababu tunataka mkae kwa usalama,” alisema.
Alisema
suala la usalama ni muhimu miongoni mwao, ni muhimu zaidi kwa majirani zao
lakini pia ni muhimu sana kwa watoa huduma wanaowahangaikia.
“Tunataka
kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake ili siku mkiondoka mrudi nyumbani mkiwa
salama,” alisema.
“Ninyi mko
hapa mnatunzwa kwa hiyo hamruhusiwi kutoka kambini na kutembea hovyo huko nje.
Hii ni kwa usalama wenu.
Hatumruhusu kuingia na bunduki au mabomu na yeyote
atakayemuona mwenzie ana silaha au ameificha mahali aje atuambie ili
tumchukulie hatua na ninyi wengine mbakie salama,” alisisitiza.
Kuhusu
maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU), Waziri Mkuu aliwataka wakimbizi hao
wajiepushe na ngono zembe kwa sababu kiwango cha maambukizi kimeongezeka kwa
asilimia moja ikilinganishwa na mwaka jana,2014.
“Nimetembelea
hospitali yenu hapa kambini na kuelezwa kuwa maambukizi ya VVU hapa yapo na
mwaka huu yamefikia asilimia mbili ya watu waliopimwa ikilinganishwa na mwaka
ambapo ilikuwa ni asilimia moja tu,”
“Kutokana na
uwingi wenu, naomba niwasihi sana mjizuie kufanya ngono zembe na kama mtu
atashindwa kabisa kujizuia ni vema atumie kinga. La sivyo mtaleta maambukizi ya
juu sana na wote mtakwisha,” alisema.
“Suala
lenyewe siyo jambo la dharura, kawaida huwa kuna maandalizi baina ya wahusika,
watu wanakubaliana juu ya muda na mahali pa kukutana ndiyo maana nasema siyo
jambo la dharura. Ndugu zangu tujihadhari sana kwa sababu kasi ya maambukizi
mahali hapa iko juu sana,” alisisitiza.
Mapema, Mkuu
wa kambi ya Nyarugusu, Bw. Sospeter Boyo alimweleza Waziri Mkuu kwamba kambi hiyo
ilifunguliwa Novemba 1996 kwa lengo la kuwahifadhi wakimbizi kutoka Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo waliokuwa wakikimbia vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Alisema
kambi hiyo yenye ukubwa wa kilometa za mraba 28, ina uwezo wa kuhifadhi
wakimbizi 50,000 lakini kwa sasa inao wakimbizi 151,032 ambao ni mara tatu
zaidi ya uwezo halisi wa kambi hiyo.
“Tangu
Aprili mwaka huu,2015, idadi ya wakimbizi imeongezeka hadi kufikia 151,032 miongoni
mwao ni wakongo 61,313, warundi 89,619, Wanyarwanda 75, Waganda 12, Wasudan kusini
wane,Wakenya wane, Msomali mmoja, Mzimbabwe mmoja na raia wa Ivory Coast
mmoja,” alisema Bw. Boyo.
Alisema
wanakabiliwa na changamoto za uhaba wa maji safi, ufinyu wa huduma za afya na
elimu na uharibifu wa mazingira.
Waziri Mkuu
bado anatembelea pia kambi ya JKT ya Mtabila wilayani Kasulu na kesho asubuhi (
leo) anatarajiwa kufanya majumuisho ya ziara yake.
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
JUMANNE,
DESEMBA 29, 2015.
Papo kwa Papo >>>> Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo na Nyingine kwa kujiunga na mimi hapa…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp .
|
No comments:
Post a Comment