|
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
Kanda ya Ziwa, imekamata na kuziteketeza bidhaa zenye uzito wa tani 8.26
zisizokidhi vigezo vya ubora na usalama kwa chakula, dawa za binadamu na mifugo
pamoja na vipodozi vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 4.5 katika kipindi
cha 2014/15.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya
habari iliyotolewa na mamlaka hiyo, hatua hiyo ni utekelezaji wa Sheria Na.1 ya
2003 ya Chakula, Dawa na Vipodozi kwa wasindikaji, wauzaji wa chakula,
dawa, vipodozi na vifaa tiba.
“Bidhaa za dawa za binadamu na
mifugo zenye uzito wa tani 1.8 zikiwa na thamani ya Sh. bilioni 1.2,
zilikamatwa sokoni na kuteketezwa kutokana na viwango duni, bidhaa bandia
pamoja na bidhaa nyingine kwa kutokuwa na usajili wa mamlaka,” ilifafanua
taarifa hiyo.
Pia taarifa hiyo ilisema vipodozi
vyenye uzito wa tani 3.6 vyenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 2.3,
vilikamatwa baada ya kukutwa na makosa ya kutokuwa na usajili wa mamlaka pamoja
na vipodozi vingine kupigwa marufuku kutokana na kuwa na viambata vyenye sumu.
TFDA imewataka wafanyabiashara wa
chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba, kuzingatia matakwa ya Sheria ya Chakula
na Dawa kwa kuhakikisha bidhaa wanazozalisha, kununua, kuziuza, kuzitunza na
kuzisambaza, zinakidhi vigezo vya ubora, usalama na ufanisi ili kumlinda
mtumiaji wa bidhaa hizo.
TFDA imesema kazi ya kukamata na
kuharibu bidhaa zinazokwenda kinyume na matakwa ya kisheria ni endelevu na
itaendelea kuwachukulia hatua stahiki wafanyabiashara watakaokiuka taratibu na
masharti husika.
CHANZO: NIPASHE
Papo kwa Papo >>>> Pata Picha, Habari za Siasa, Kijamii, Biashara, Muziki na Michezo
na Nyingine kwa kujiunga na mimi hapa…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia
tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
|
No comments:
Post a Comment