MGOGORO WA KISIASA BURUNDI:-Raia 940 wapewa Hifadhi wilayani Kasulu huku wakazi wa Ngara wakitakiwa kujiandaa kuwapokea. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Wednesday, May 06, 2015

MGOGORO WA KISIASA BURUNDI:-Raia 940 wapewa Hifadhi wilayani Kasulu huku wakazi wa Ngara wakitakiwa kujiandaa kuwapokea.


Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Bw John Mongella (Pichani kushoto) ameiagiza Halmashauri ya wilaya ya Ngara kusitisha uuzaji wa Ardhi na Rasilimali nyingine zinazoweza kuwanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla katika siku za usoni.

Bw Mongella ametoa agizo hilo Jana May 05,2015  wakati akikagua eneo la Rumasi wilayani Ngara kuona iwapo linafaa kwa ajili ya Mapokezi ya Raia wa Burundi ambao baadhi yao wameanza kukimbia nchi yao kutokana na vurugu na maandamano ya Kupinga Rais Pierre Nkurunziza asiwanie muhula wa tatu wa uongozi kwenye uchaguzi ujao.

Amesema baadhi ya maeneo ilipokuwa Kambi ya Wakimbizi ya Lukole na Rumasi yameuzwa na mengine kugawiwa kwa wananchi jambo alilosema kuwa hatari iwapo yatatokea Majanga yanayohitaji maeneo ya hifadhi ili kutoa huduma za Kijamii.

Pichani Mkuu wa wilaya ya Ngara mkoani Kagera,Bw.Costantine Kanyasu akizungumza na waandishi wa Habari katika ziara hiyo ya Mkuu wa mkoa wa Kagera.

Kwa upande wake Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Kagera Bw George Kombe amewataka Wakazi wa Ngara kujiandaa kuwapokea Wakimbizi kutoka Burundi watakaoingia nchini kwa mujibu wa Sheria kutokana na hali ya Kisiasa nchini mwao.

Katika Hatua nyingine, Raia 940 wa Burundi wamepewa Hifadhi katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu wilayani Kasulu Mkoani Kigoma baada ya kukimbia vurugu na maandamano yanayoendelea nchini mwao kutoka na mgogoro wa Kisiasa.

Mkuu wa Makazi ya Wakimbizi Kambini humo Bw Sospeter Boyo amesema idadi hiyo ya waliopokelewa kwa sasa inafanya Idadi ya Raia wa Burundi wanaoomba hifadhi kwenye Kambi ya Nyarugusu kufikia watu elfu 2 na 274 na kwamba asilimia kubwa ni wanawake na watoto.

Amesema mbali na raia hao wa Burundi ambao tayari wamepewa Hifadhi kambini humo hadi sasa lakini wapo wengine wasiopungua 600 wanatarajia kuwapokea wakati wowote ili wapepe Hifadhi.

Bw Boyo amesema baada ya kupokelewa Kambini humo, waomba hifadhi hao wameorodheshwa na kupewa Chakula, Vifaa vya Kujengea nyumba za muda pamoja na vifaa vya ndani yakiwemo Maturubai, Ndoo na Mablanketi .

Aidha tayari Mahakama ya Katiba nchini Burundi imemruhusu Rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu wa Urais kwenye Uchaguzi  Mkuu uliopangwa kufanyika mwezi June mwaka huu 2015 na hivyo kumpa Mamlaka kisheria Rais Nkurunziza kuendelea na harakati za Kuwania Urais kwenye uchaguzi ujao.

Source:-RADIO KWIZERA FM.

Pata Picha, Habari za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi na Michezo kila stori inayonifikia wakati  wowote ukijiunga na mimi kwa kubonyeza…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad