UHALIFU:-Askofu GWAJIMA Ajisalimisha Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam huku akisema maneno aliyoyatoa ni maneno ya Mungu. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Friday, March 27, 2015

UHALIFU:-Askofu GWAJIMA Ajisalimisha Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam huku akisema maneno aliyoyatoa ni maneno ya Mungu.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limeanza kumhoji Askofu JOSEPHAT GWAJIMA wa Kanisa la Ufufuo na Uzima baada ya kujisalimisha kama alivyotakiwa kufanya hivyo na Kamishana wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.


Askofu Gwajima alifika kituo kikuu cha Polisi saa nane na dakika kumi na tano mchana wa tarehe 27/03/2015. Mara baada ya kufika kituoni hapo alielekezwa kwenda kumuona Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Constantine Masawe ambaye alikuwa akisubiri kufika kwake.

Tuhuma zinazomkabili Askofu Gwajima ni pamoja na kumkashfu na kumtukana hadharani Kiongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Taratibu za mahojiano zimekwishaanza kwa mujibu wa sheria na mtuhumiwa atapewa haki zote anazostahili kama vile kuwa na ndugu yake wa karibu, rafiki yake anayemwamini au wakili wake. 

Kama ilivyo kawaida utakusanywa ushahidi kutoka pande zote za shauri hilo ili kubaini ukweli wa jinsi tukio hilo lilivyotokea na athari zake.

Baada ya hapo hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kupata maoni ya kitaalamu na ya kisheria ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka. 

Ili ufanisi upatikane katika upelelezi wa shauri hili, ni muhimu kupata ushirikiano kutoka kwa kila atakayetakiwa kulisaidia Jeshi la Polisi kukamilisha haraka upelelezi wa shauri hili ambalo sasa limepata mvuto mkubwa katika jamii.

Imetolewa na:

S. H. KOVA

KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM

DAR ES SALAAM

 Pata Picha, Habari za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi na Michezo kila stori inayonifikia wakati  wowote ukijiunga na mimi kwa kubonyeza…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630. 



Katika hatua nyingine…,’’Mara baada ya kuwasili katika kituo hicho alipokelewa kwa mahojiano ya awali kutoka kwa vyombo vya habari ambapo Askofu Gwajima amesema maneno aliyoyatoa ni ya kumkemea kiongozi mwenzake wa kiroho kwa madai ya kukiuka msimamo wa viongozi wengine wa dini wa kuikataa mahakama ya kadhi.

Akijibu swali kuhusu sababu za kufanya hivyo badala ya kutumia maneno ya kistaarabu ,Askofu Gwajima amedai kuwa maneno aliyoyatoa ni maneno ya mungu huku akishangazwa na wito wa Polisi kwa kuwa maneno hayo hakuyatoa kwa Jeshi la Polisi bali kwa kiongozi mwenzie wa kiroho.

Askofu Gwajima alirekodiwa kwenye ibada ya kanisa lake Jumapili iliyopita ambapo ‘alimtusi’ Pengo akituhumu kuwa ni msaliti kwani amekwenda kinyume na Taasisi ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste (CPCT) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa kuwataka waumini waisome Katiba Inayopendekezwa kisha wapewe uhuru wa kupiga kura ya “ndiyo” au “hapana” tofauti na vyombo hivyo vyenye dhamana ya kuongoza dini ya Kikristo vilivyotaka waumini waipigie kura ya “hapana” Katiba Inayopendekezwa.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad