BUNGENI TANZANIA:-Hii ndio Miswada iliyopitishwa March 2015 na Bunge la Tanzania ikiwemo ule wa Waandishi wa habari Kutiwa kitanzi. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Sunday, March 29, 2015

BUNGENI TANZANIA:-Hii ndio Miswada iliyopitishwa March 2015 na Bunge la Tanzania ikiwemo ule wa Waandishi wa habari Kutiwa kitanzi.


 Waziri wa Fedha Saada Mkuya  akihitimisha Muswada  wa Sheria ya Bajeti wa Mwaka 2014, Bungeni mjini Dodoma  Machi 28, 2015.


Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana March 28, 2015 limepitisha muswada wa sheria ya bajeti wa mwaka 2014 ambao unatajwa kuwa utakuwa suluhu ya kudumu ya matumizi ya fedha za umma kwa nidhamu na kuliepusha taifa na vitendo vya ubadhirifu vilivyoshamiri hapa nchini.

Akijibu hoja za Wabunge mbalimbali kabla ya muswada huo kupitishwa,Waziri wa fedha Mhe.Sada Mkuya amesema muswada huo utawabana pia baadhi ya viongozi wa wizara wakiwemo mawaziri ambao wamekuwa na tabia ya kushinikiza taasisi ambazo zipo chini ya wizara zao kuwapa fedha za kuendesha wizara pindi bajeti ya wizara husika inapoisha kabla ya wakati.

Naye Mbunge wa Jimbo la Pangani Salehe Pamba pamoja na yule wa Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa wameitahadharisha Serikali kuangalia pia utendaji kazi wa wafanyakazi wake sambamba na kudhibiti vitendo vya rushwa ili kufanya muswada huo uweze kutimiza malengo yake.

Kwa upande wake Mbunge wa Mbozi Magharibi David Silinde amesema Muswada huo utalisaidia kikamilifu Taifa la Tanzania kama pia utawasilishwa pia katika baraza la wawakilishi ili kufanya pande zote mbili za Muungano kunufaika nao.




Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiteta na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo  ya Makazi, Angela Kairuki, Bungeni mjini Dodoma  Machi 28, 2015. 

PIA Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  limepitisha miswada mitatu  ndani ya saa tatu huku moja ya miswada hiyo ikiwa ni kitanzi kwa waandishi wa habari ambapo mwandishi atakayeandika takwimu za kutoka katika chanzo sahihi cha Serikali na  baadaye kugundulika amepotoshwa  na chanzo hicho atahukumiwa miaka mitatu jela au kulipa faini ya shilingi milioni kumi.

Miswada ambayo imepitishwa ni ile ya wakala wa usimamizi wa maafa ya mwaka 2014,muswada wa sheria ya usimamizi wa kodi wa mwaka 2014  pamoja na ule wa sheria ya takwimu wa mwaka 2013 ambapo ulisababisha majibizano kati ya,Mbunge wa Ubungo John Mnyika,Mbunge Viti Maalum Ester Bulaya pamoja na mwanasheria mkuu wa Serikali George Masaju kuhusiana na kuwepo kipengele kisichofaa.

Kipengele hicho ni kile kinachosema mwandishi wa habari atakayeandika takwimu za kutoka katika chanzo sahihi cha Serikali na baadaye kugundulika amepotoshwa na chanzo hicho atalazimika kuchukuliwa hatua za kisheria na Serikali ikiwemo kifungo cha miaka mitatu ama kulipa faini ya shilingi milioni kumi ambapo wabunge hao wamekipinga ilhali mwanasheria mkuu wa Serikali amesema kinafaa.

Maazimio ambayo yamepitishwa bungeni hapo ni la kuridhia mkataba wa msingi na kanuni za utumishi wa umma na utawala barani Afrika la mwaka 2011 na lile la kuridhia makubaliano ya msingi ya ushirikiano katika bonde la Mto Nile .

AIDHA Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  pia limepitisha miswada miwili ya sheria ya usimamizi wa maafa ya mwaka 2014 pamoja na ule sheria  ya usimamizi wa kodi wa mwaka huo huo 2014.

Miswada hiyo imepitishwa baada ya kushindikana katika vikao vilivyopita kutoka na idadi ya wabunge waliotakiwa kuipigia kura kutokutimia.

Mapema  ,Mwenyekiti wa bunge Lediana Mng'ongo alitoa agizo kwa wabunge waliopo nje ya bunge kuingia ndani ili idadi inayotakiwa kisheria kupigia kura muswada wa marekebisho ya sheria ya uhamiaji ya mwaka 2014 ambao inahitaji robo tatu ya wabunge wawepo wakati unapitishwa.

Kumekuwa na mahudhurio yasiyoridhisha ya wabunge katika mkutano wa 19 ambao unaendelea mkoani Dodoma hali inayofanya baadhi ya miswada kushindikanika kupitishwa.
Source:-ITV.

Pata Picha, Habari za Kisiasa, Kijamii, Kiuchumi na Michezo kila stori inayonifikia wakati  wowote ukijiunga na mimi kwa kubonyeza…..FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad