PICHA / HABARI:-Soma hapa siku ya Matokeo ya mtihani kidato IV 2014 na Daftari la Wapiga kura. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Tuesday, February 10, 2015

PICHA / HABARI:-Soma hapa siku ya Matokeo ya mtihani kidato IV 2014 na Daftari la Wapiga kura.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde.


Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne nchini ya mwaka 2014, yanatarajiwa kutangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Jumapili Februari 15,2015.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde (pichani), alitoa ahadi hiyo kama zawadi kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mpwapwa mkoani Dodoma, kufuatia ajali ya moto iliyotokea Januari  20, mwaka huu na kuteketeza mali zote zilizokuwa kwenye bweni la wasichana 64 wa kidato cha tano na cha sita.

Dk. Msonde alikuwa miongoni mwa viongozi walioongozana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi-Elimu), Kassim Majaliwa, kwenye ziara ya kutoa pole katika shule hiyo.

Zawadi niliyowaandalia ni taarifa kwamba Februari 15, mwaka huu, tutatangaza matokeo ya mitihani iliyofanywa na watahiniwa wa kidato cha nne nchini. Nasema ni zawadi kwa sababu sijaitoa mahali kokote, nyie ndiyo wa kwanza kuipata,” alieleza Msonde.

Watahiniwa waliotarajiwa kufanya mtihani huo Novemba, mwaka jana 2014 ni 297,488 huku watanihiwa 245,030 wakiwa wa shule na watahiniwa wa kujitegemea walikuwa 52,448. Watahiniwa wa shule walioandikishwa ni wavulana 132,244 (asilimia 53.97) na wasichana 112,786 (asilimia 46.03).

Kwa kawaida, matokeo ya kidato cha nne hutolewa Aprili, lakini mwaka huu yatatoka mapema kutokana na uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu. Walimu ni miongoni mwa watumishi wa serikali ambao hutumiwa kusimamia uchaguzi mkuu.

Source:-Nipashe.

Mkuu wa Idara ya Elimu ya Mpiga Kura na Habari wa NEC, Ruth Masham.

SASA ni rasmi kwamba kazi ya kuliboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura nchini kote, itaanza Jumatatu ijayo Februari 16,2015  na kumalizika Aprili 29 mwaka huu.
Uandikishaji huo utaanzia katika mikoa ya Lindi, Ruvuma, Mtwara na Njombe na baadaye utahamia katika mikoa mingine.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema ratiba ya upigaji wa kura ya maoni ambayo ni Aprili 30,2015 iko pale pale, kama ilivyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete. Wakati uandikishaji huo ukianzia katika mikoa minne, utafungwa kwa kumalizia Dar es Salaam na Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Februari 09,2015, ofisini kwake, Mkuu wa Idara ya Elimu ya Mpiga Kura na Habari wa NEC, Ruth Masham aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika uboreshaji wa daftari la wapigakura baada ya utoaji wa elimu kwa waratibu kukamilika.

Alisema tume hiyo imetoa elimu kwa waratibu wa waandikishaji kwa kila mkoa na katika kila mkoa wametoa mafunzo hayo kwa mratibu mmoja.

Pia, elimu imetolewa kwa maofisa waandikishaji wa Halmashauri, na wasaidizi wao na hao ndio watakaotumika kutoa elimu kwa waandikishaji wadogo katika ngazi za tarafa na kata.

Masham alisema ni haki ya kila Mtanzania kujiandikisha. Alisema wananchi wana haki ya kutumia fursa hiyo ya kujiandikisha ili ifikapo Oktoba mwaka huu waweze kutumia haki hiyo ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka.

Katika kikao cha Bunge kilichomalizika wiki iliyopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwahakikishia Watanzania kuwa uandikishwaji wa wapiga kura ambao utatumia Mfumo wa Kielektroniki (BVR), utafanyika kwa ufanisi na kwa wakati uliopangwa.

Source:-Habari Leo.

UNGANANASI KATIKA  FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad