![]() |
|
MWANANCHI.
Mfumuko wa
bei kwa mwezi januari umeshuka hadi kufikia asilimia 4.0 kutoka asilimia
4.8 ya Desemba mwaka jana kutokana na kupungua kwa bei za bidhaa
mbalimbali ikielezwa kwamba kupungua huko kulikuwa hakujatokea kwa miaka miwili
iliyopita.
Mkurugenzi
wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo alieleza
kuwa kushuka huko kumetokana na kupungua kwa kasi ya upandaji bei ya bidhaa na
huduma ikilinganishwa na ilivyokuwa Desemba .
Amesema
mfumuko wa bei za vyakula na vinywaji umepungua hadi asilimia 4.9 kutoka
asilimia 5.7 ya mwezi Desemba.
Ametaja
baadhi ya vyakula vilivyochangia kushusha mfumuko huo kuwa ni mahindi
yaliyoshuka kwa asilimia mahindi 13.3, unga wa mahindi (6.2), samaki (2), ndizi
za kupika (11.3), mihogo (12.0)
Kwa mujibu
wa Kwezigabo bidhaa zisizo za chakula nazo zilipungua. Mafuta ya taa yalishuka
kwa asilimia 8.4, dizeli (10.2), petroli (6.8) na gesi ya kupikia ilishuka kwa
asilimia 2.9. Takwimu hizo mpya zinaonyesha kuwa fahirisi za bei zimeongezeka
kutoka 146.0 Januari 2014 , hadi kufikia 152.43 Januari mwaka huu.
MWANANCHI.
Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye
amesema chama hicho hakitampitisha mgombea urais asiye na sifa na kuhangaika
kumsafisha kwa dodoki ili atakate.
Amesema
chama hicho kimeweka mfumo mzuri wa kupata mgombea mwenye sifa, msafi na salama
ambaye kazi kubwa itakayokuwapo kwa CCM ni kumwombea kura tu na si kumsafisha.
Alisema CCM
ina utaratibu imara ambao utatoa mgombea bora, huku akisisitiza kuwa
utawashangaza wengi pale atakapopitishwa mgombea ambaye hakutarajiwa na wengi.
“Mwaka 1995
Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema ‘msinipe mgombea ambaye nikisimama naanza
kumsafisha kwanza.’ Tutatafuta mgombea wa kumuombea kura,”
Nape alisema jana
Februari 09,2015, wakati akizungumza na wahariri wa Magazeti ya Mwananchi na The Citizen
alipotembelea ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata
Relini.
Kauli hiyo
ya Nape imekuja siku chake baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya
Kikwete kuwataka wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu huku akisema:
“Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu wa kupata rais wa awamu ya tano,
utakuwa wa kihistoria.”
MWANANCHI.
Zinaitwa
bodaboda, kule Nigeria wanaziita okadas kwa jina jingine ni pikipiki. Hiki ni
chombo cha usafiri ambacho katika miaka ya hivi karibuni kimeiteka miji mingi
ya Afrika ikiwamo Tanzania.
Licha ya
kutumika katika uhalifu, kusababisha vifo kwa kiasi kikubwa, utafiti
uliofanywa na gazeti hili katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam ambako
kuna matumizi makubwa ya bodaboda ulibaini kuwa usafiri huu unapendwa zaidi na
wanawake.
Dereva wa
bodaboda katika maeneo ya Tabata Relini, Ayubu Msigala anasema
idadi kubwa ya abiria wake ni wanawake. Anasema wanawake wajawazito pia
wanatumia usafiri huo kwa kiasi kikubwa.
“Zamani
wanawake walikuwa wanaogopa bodaboda, lakini sasa hata wajawazito
wanatumia zaidi, hawaogopi kama ilivyokuwa zamani:-Msigalla.
Akizungumzia
suala la wanawake kupenda bodaboda, Msigala anasema wanawake waliokuwa
wakiziogopa bodaboda sasa ndiyo wanaozipanda kwa wingi huku wanawake wajasiriamali
wakiongoza kuzitumia.
Anasema
mamalishe, wauza nguo, vocha, hata wafanyakazi wa maofisini wamekuwa wapandaji
wakubwa wa bodaboda.
“Hata
akina mama wanaokwenda hospitali kupeleka watoto hutumia zaidi usafiri huu ili
kuwahi, wakati mwingine naweza kumpakia mama na watoto wake wawili na mzigo,”
anasema.
Hata
wajawazito wenye kipato cha chini wameelezwa kuzitumia pindi inapowabidi na
wengine zimekuwa zikiwapeka kujifungua.
NIPASHE.
Tuhuma za
kuwapo kwa vigogo wanaoficha fedha katika benki za Uswisi sasa ni dhahiri baada
ya ripoti ya mtandao wa Swiss Leaks chini ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi
wa Kimataifa (ICIJ) kufichua kuwa wapo Watanzania 99 wenye akaunti za
siri nchini humo zenye mabilioni ya fedha.
Taarifa ya Swiss
Leaks iliyotolewa juzi inaonyesha kuwa Watanzania hao, wakiwamo wanasisa na
maofisa wa juu wa serikali, wana akaunti za siri zenye Dola za Marekani milioni
114, ambazo ni sawa na Sh. bilioni 199.6.
Kwa mujibu
wa ripoti hiyo, Tanzania iko nafasi ya 100 kati ya nchi zenye kiasi kikubwa cha
dola kwenye akaunti za siri nchini Uswisi.
Msingi wa
ripoti hiyo umetokana na aliyekuwa mfanyakazi wa benki ya kimataifa HSBC,
Hervé Falciani, kuvujisha siri za akaunti za wateja baada ya kuacha
kazi; na mwaka 2008, alivujisha siri za akaunti za siri za baadhi ya watumishi
wa umma na wanasiasa wa Ufaransa ambayo mamlaka za kodi nchini humo ilifanya
uchunguzi kuthibitisha.
HSBC ni
benki kubwa ya biashara duniani ambayo ilianzishwa mwaka 1836.
Kwa mujibu wa
Swiss Leaks, matokeo ya uchunguzi huo yanatokana na aina tatu za taarifa ndani
ya benki kwa vipindi tofauti; Mosi ni taarifa za wateja na uhusiano wao na
akaunti za benki nchini Uswisi kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1988 hadi 2007.
NIPASHE.
Vyama vya
vya siasa nchini vinalaumiwa kuteka demokrasia kwa kuwanyima wanawake nafasi za
uongozi.
Hayo
yalielezwa na wanaharakati wa haki za wanawake wakati wakitoa mafunzo kwa
waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa wanawake katika uchaguzi mkuu wa mwaka
2015.
Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi cha Muhimbili (MUHAS), Dk. Ave
Maria Semakafu alisema demokrasia ya Tanzania inawanyima fursa
wanawake katika kushika nyazifa mbalimbali za uongozi katika vyama vya siasa
huku nafasi nyeti zimeshikiliwa na wanaume.
Alisema
wanawake ambao wamebahatika kupata nafasi katika vyama hivyo wamezipata kwa
upendeleo, udugu na rushwa ya ngono.“Katika vyama vya siasa wanawake, watu
wenye ulemavu na vijana hawajapewa kipaumbele kushika nafasi za uongozi,”alisema.
Alisema
katika siasa za Tanzania, vijana wamepewa kipaumbele katika kushiriki vurugu na
wanawake wao katika kupiga vigelegele na makofi katika mikutano ya siasa lakini
hawapo katika ngazi za maamuzi.
MTANZANIA.
Jeshi la
Polisi mkoani Kilimanjaro, limelazimika kutumia mabomu ya machozi na silaha za
moto, kuzima maandamano ya wafugaji wa jamii ya Kimasai kutoka mikoa ya Arusha,
Manyara na Kilimanjaro, waliokuwa wamejipanga kuvamia Kituo Kikuu cha Polisi
Sanya Juu, Wilaya ya Siha mkoani hapa.
Wafugaji hao
wanadaiwa walikuwa wakishinikiza kiongozi wao anayeshikiliwa (jina
halijafahamika), kuachiwa na Polisi Wilaya ya Siha.
Askari wa
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kutoka Mjini Moshi waliokuwa na
magari manne, walilazimika kutumia nguvu walipokutana na wafugaji hao wakiwa
wamefika eneo la mwisho wa lami njia panda ya Karansi na Magadini, Wilaya ya
Siha wakielekea kilipo kituo hicho umbali wa kilomita tano.
Habari
zilizopatikana jana na baadaye kuthibitishwa kwa njia ya simu na Kamanda wa
Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela, zilisema makundi ya wafugaji hao yaliingia
Wilaya ya Siha kwa nyakati tofauti yakitumia malori, pikipiki aina ya bajaj,
bodaboda na magari ya kukodi.
“Kwa sasa
niko Siha kwenye operesheni maalum baada ya kuwatawanya wafugaji kutoka mikoa
ya Arusha na Kilimanjaro. Bahati nzuri tumefanikiwa kuzima maandamano hayo
yaliyokuwa na lengo la kuvamia Kituo cha Polisi, na hivi sasa tunakusanya
taarifa za kiuchunguzi kwa hiyo kesho au baadaye nitatoa taarifa ya
kilichotokea:-Kamanda Kamwela.
Kwa mujibu
wa Kamanda Kamwela, wafugaji hao ambao idadi yao hadi sasa haijajulikana, licha
ya kuingia mkoani hapa wakitokea mikoa hiyo ya jirani kwa ajili ya kuunganisha
nguvu na wenzao wa Wilaya ya Siha kutafuta malisho ya mifugo yao,
walikuwa wakitumia mbinu mbalimbali kuwakwepa Polisi.
HABARI LEO.
Bweni la
wanafunzi wa shule ya sekondari ya Idodi wilayani Iringa mkoani Iringa,
limeteketea kwa moto na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi, ikiwa ni
miaka sita tu tangu bweni hilo liungue na kusababisha hasara kubwa na vifo vya
wanafunzi 13.
Agosti 25,
2009 bweni la shule hiyo, liliwaka moto na kusababisha vifo vya wanafunzi wa
kike 13, ambao baadhi yao walizikwa shuleni hapo baada ya miili yao kuharibika
vibaya.
Katika tukio
hilo, wanafunzi wengine 23 walijeruhiwa vibaya, baada ya bweni hilo kushika
moto uliosababishwa na mshumaa uliowashwa na aliyekuwa mwanafunzi wa shule
hiyo, Naomi Mnyali ambaye alisahau kuuzima baada ya kumaliza kusoma.
Akizungumza
kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto mkoani
Iringa, Inspekta Kennedy Komba alisema kuwa bweni hilo
limeteketea lote na kuunguza baadhi ya mali, zikiwemo za wanafunzi zilizokuwemo
katika bweni hilo.
Alisema
taarifa za awali zinaonesha chanzo cha moto huo, kilitokana na hitilafu ya
umeme na kwamba hakuna mwanafunzi yeyote aliyejeruhiwa katika tukio hilo. Komba
alisema kuwa baada ya jeshi la zimamoto kupata taarifa ya tukio hilo, lililotokea
kati ya saa 3 na 4 jana asubuhi wakati wanafunzi wa shule hiyo wakiwa darasani,
iliwachukua dakika 45 kufika katika eneo la tukio.
Alisema
baada ya kufika katika eneo la tukio kutoka Iringa mjini ambako ni umbali wa
kilometa 40, kazi ya kuuzima moto huo haikuwa kubwa, kwani wananchi waliofika
kutoa msaada, walifanikiwa kuzima moto huo kwa kiasi kikubwa.
Aliwapongeza
wananchi kwa moyo wa ushujaa wa kujitolea na kuwataka kutoa taarifa mapema
pindi majanga ya moto, yanapojitokeza katika maeneo yanayowazunguka.
“Endapo
tungepata taarifa mapema ninaamini tungeweza kuokoa vitu vingi zaidi,” alisema
Kamanda huyo na kuwataka wananchi wasitegemee mtendaji au kiongozi apige simu
kwa kikosi cha kuzima moto kwani kila mtu ana fursa ya kupiga simu 111 katika
kitengo cha mawasiliano cha jeshi hilo”.
MTANZANIA.
Upande wa
Mashikata kesi inayomkabili Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini,
Sheikh Ponda Issa Ponda umewasilisha ushahidi muhimu wa mkanda wa
video unaodaiwa kuonesha uhalisia wa tukio zima la kesi yake inayomkabili ya
kutoa maneno ya uchochezi.
Mkanda huo
wa video uliletwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, Mary
Moyo na kuoneshwa na shahidi wa tano wa kesi hiyo ambaye ni askari
kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi kitengo maalumu cha uchunguzi wa picha,
Aristides alieleza vigezo alivyovitumia kuitambua uhalisia wa video hiyo
iliyochukuliwa Agosti 10 mwaka 2013.
Shahidi huyo
akiongozwa na Wakili wa Serikali, Benard Kongola alieleza
mahakamani hapo kuwa video aliichunguza na kugundua kuwa ilichukuliwa katika
eneo la tukio kupitia kamera ndogo aina ya JVC na kwamba baada ya kuichunguza
aliandika hati na taarifa iliyoeleza vigezo alivyovitumia katika uchunguzi huo
na yale aliyoyaona na kuyasikia katika video hiyo ambayo aliitoa mahakamani
kama kielelezo.
Pamoja na
ushahidi wake, lakini pia aliionesha video hiyo mahakamani hapo ambapo
ilionesha tukio zima pamoja na maneno aliyoyatoa Shehe Ponda ambayo yanadaiwa
kuwa yalikuwa ya uchochezi na yaliyoumiza imani ya dini nyingine.
Shahidi huyo
pia alitoa kamera, DVD, hati na taarifa ya uchunguzi wa video hiyo kama
kielelezo na kupokewa na mahakama hiyo.
MWANANCHI.
Baada ya
kumalizika mkutano wa 18 wa Bunge Jumamosi iliyopita, wabunge wengi
wamekimbilia kwenye majimbo yao hatua inayohusishwa na homa ya Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba.
Tofauti na
kawaida ya wabunge wengi ambao baada ya vikao vya Bunge hukimbilia Dar es
Salaam, safari hii wengi wameelekea majimboni kuweka mikakati ya kuhakikisha
wanarudi bungeni katika uchaguzi huo.
Baadhi ya
wabunge waliohojiwa jana wameelezwa kuwa wako katika mikakati mbalimbali ya
kupambana na wapinzani wao watakaojitokeza kuwania nafasi hiyo.
Mbunge wa
Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani jana alikuwa kwenye
mazishi ya rafiki yake na taarifa zinasema kwamba baada ya mazishi hayo
ataendelea na shughuli zake za jimbo.
Mbunge wa
Tanga Mjini (CCM), Omar Nundu, Mbunge wa Lushoto (CCM), Henry
Shekifu, Mbunge wa Mkinga (CCM), Dastan Kitandula, Mbunge
wa Muheza (CCM), Herbert Mtangi wapo majimboni mwao
wakiendelea na shughuli zao.
Imeelezwa
pia kwamba wabunge Yusuph Nassir (Korogwe Mjini – CCM), Saleh Pamba (Pangani –
CCM) wako Dar es Salaam wakijipanga kurudi majimboni mwao kufanya mikutano na
shughuli zao za kisiasa.
Source:-Millardayo.
UNGANANASI KATIKA FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
|
Tuesday, February 10, 2015
Home
HABARI
Mkusanyiko wa stori 09 zilizopewa headlines kwenye Magazeti ya leo Tanzania February 10,2015... ziko hapa
Mkusanyiko wa stori 09 zilizopewa headlines kwenye Magazeti ya leo Tanzania February 10,2015... ziko hapa
Tags
# HABARI
Sambaza Hii
Chief Editor | Mhariri
HABARI
Labels:
HABARI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Kuhusu Mwandishi
Journalist / Chief Editor / Tanzanian Blogger
Simu: 0756830214 / 0620197747 / 0789925630.






No comments:
Post a Comment