MASWALI / MAJIBU :-10 Kwa Mbunge wangu, Deogratias Ntukamazina - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Friday, February 27, 2015

MASWALI / MAJIBU :-10 Kwa Mbunge wangu, Deogratias Ntukamazina

WASIFU Jina: Deogratias Aloyce Ntukamazina , Chama: CCM Jimbo: Ngara,Kagera.


1.Mwalimu Superi Jeremiah wa Shule ya Msingi Bihororo Ngara.

Uliahidi kuondoa kero ya wazee kulipia gharama za matibabu katika vituo vya kutolea huduma, hadi sasa wananchi bado wanataabika. Je, umefanya jitihada gani kuhakikisha wazee hao wanatibiwa bure katika hospitali ndani ya meneo yao?

Jibu: Naomba wananchi wa Ngara wakumbuke vizuri, mimi nilitoa ahadi moja tu kwamba nitashirikiana na Serikali na halmashauri ya wilaya ya Ngara pamoja na wananchi kupambana na maadui watatu yaani umaskini, ujinga na maradhi. 

Chini ya adui maradhi nimeshirikiana na wabunge wenzangu kuhimiza Serikali ihakikishe sera yake ya matibabu bure kwa wazee wa miaka 60 akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano inatekelezwa. 

Nakiri kwamba watoa huduma  ni wakaidi lakini Serikali imeahidi kuendelea kuwabana. Nimefanya juhudi kubwa kama mwenyekiti wa Mfuko wa Bima ya Afya kuhamasisha kaya mbalimbali kujiunga na mfuko  huo ambao kaya moja inalipa Sh10,000 kwa matibabu ya kaya nzima kwa mwaka mmoja. Kuna wazee wanaweza kumudu Sh10,000 kwa mwaka.

2.Mohamed Namtimba Kata ya Kabanga- Ngara.

Uliahidi kuishauri Serikali kutenga fedha za uhamisho wa watumishi waliokaa kituo cha kazi muda mrefu, lakini ahadi yako haijatekelezeka hadi sasa?

Jibu: Nimeshauri mara nyingi Tamisemi kuhakikisha inakuwa na utaratibu wa kuwahamisha hamisha watumishi wake ili wasikae kwenye kituo kimoja cha kazi kwa zaidi ya miaka 10, tatizo ni fedha. 

Muuliza swali utakumbuka Rais (Jakaya Kikwete) alipofika Ngara mwaka juzi akiongozana na Waziri wa Tamisemi nilimwomba awahamishe watendaji wa halmashauri ya Ngara ambao walikuwa wamekaa kwenye halmashauri kwa zaidi ya miaka 10. Waziri ameshawahamisha watendaji saba katika kutekeleza ombi langu.

3. Kenedy Staford,  Mwenyekiti wa Chadema wilayani Ngara.

Uliahidi kuondoa kero ya maji mbele ya Rais Kikwete hapa mjini Ngara. Je? Baada ya kusikia Meneja wa maji amepora zaidi ya Sh32 milioni, ulichukua hatua gani? Na miradi ya maji ya Benki ya Dunia mboa haijakamilika kikwazo ni nini?

Jibu: Rais alipofika Ngara mwaka 2013 ni mimi kama mbunge nilimuomba mbele ya wananchi atusaidie kutatua tatizo la maji katika mji mdogo wa Ngara. 

Rais bila kuchelewa alimuagiza Waziri wa Maji kutembelea mitambo ya maji ili kubaini tatizo. Mara tuliporudi bungeni waziri aliniahidi angetoa fedha Sh200 milioni. 

Wizara ilitoa Sh150 milioni na meneja wa maji akatuibia Sh 32 milioni bahati nzuri nilipohudhuria kikao cha halmashauri nilishiriki katika kuhakikisha meneja huyo anapelekwa mahakamani na sasa kesi inaendelea. 

Kuhusu kukwama kwa maji chini ya mradi wa Benki ya Dunia tatizo ni Serikali kutokuwa na fedha. Naendelea kufuatilia jambo hilo.

4.David Mapunda wa Idara ya Afya Ngara.

Tangu ahadi za kujenga na kusambaza umeme vijijini kufika kituo cha Forodha Rusumo mpakani mwa nchi ya Rwanda, ujenzi wake unasua sua umefuatilia kwa kiasi gani ili umeme upatikane kabla ya kuondoka kwako madarakani?

Jibu: Namshukuru Mungu kwa ufuatiliaji wangu na kupata ushirikiano wa REA na hivi sasa umeme umeshawaka katika kituo cha Forodha Rusumo na mchakato unaendelea wa kusambaza umeme kwenye vijiji vya jirani na Forodha ya Rusumo.

 REA imepeleka umeme Mgoma na Mamlaka ya Mji mdogo Rulenge. Nafuatilia mradi wa ORIO-Holland wa kuweka Jenereta mbili kubwa kwenye Tanesco ya Ngara ili kusambaza umeme Benaco, Kabaheshi, Nyamahwa hadi kijiji cha Kashinga.

5. Frank  Peterson

Baadhi ya changamoto za vijana ni kupata ajira kupitia idara za Serikali kwa kutumia nafasi yako ya kuishauri Serikali ni vijana wangapi kutoka wilayani Ngara wamepata ajira rasmi tangu uwe mbunge?

Jibu: Ajira serikalini inasimamiwa na sekretarieti ya ajira iliyoko Dar es Salaam. 

Sekretarieti hii huwa inatangaza nafasi zilizowazi na kuwaomba vijana wenye sifa waombe kazi hizo. 

Sina hakika ni vijna wangapi wa Ngara wamepata kazi kwa utaratibu huu. 

Bahati nzuri sekretarieti hii ya ajira kupitia idara ya menejimenti ya utumishi wa umma inawajibika kwenye kamati yangu ya Katiba, Sheria na Utawala. 

Nimekuwa mshauri mkubwa kwa sekretarieti kuitaka ikasimu madaraka ya ajira kwa halmashauri ili ziweze kuajiri vijana kwa maeneo yanayohusika kwa kazi za kawaida.

6. Philmon Charles.

Vijana walio katika Wilaya ya Ngara waliahidiwa kupata ajira kupitia mradi wa Kabanga Nickel na kwamba wazawa ndiyo wangepewa kipaumbele. Je, baada ya Kabanga Nickel kutoanza uzalishaji na kutoa ajira amechukua hatua gani serikalini kujua sababu za kukwama mradi huo na kuwaeleza wananchi sababu hizo?

Jibu: Nasikitika kwamba mradi wa Kabanga Nickel ambao ulikuwa ni tegemeo kubwa la wananchi wa Ngara kwa kutoa ajira na kusaidia huduma za jamii umesimama. 

Umesimama kwa sababu bei ya Nickel kwenye soko la dunia imeshuka sana kwa sababu China imeanzisha Nickel mbadala inayopitiwa Nickel Pig Iron. 

Serikali imenishirikisha sana katika sakata hili, ikiwa ni pamoja na kunituma niende Canada mwaka jana kuzungumza na wawekezaji. 

Hatimaye wawekezaji wa Canada wameamua kuuza hisa zao lakini  hawajapata mnunuzi. Tuendelee kuwa na subira huenda tukapata mwekezaji mwingine.

7. Askofu Dk Aaron Kijanjali.

Ahadi zilikuwa nyingi ikiwa ni pamoja na kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji kupitia mpango wa Mkurabita. Je, katika vijiji vya jimbo lako ni kipi kimekwamisha wananchi wasitengewe maeneo kila kundi kujua sehemu ya matumizi yake ya ardhi?

Jibu: Sikutoa ahadi ya kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, lakini nimeshiriki bungeni katika kuiomba Serikali ambayo inashughulikia tatizo hili la kitaifa. 

Lakini nakiri kwamba ni mimi ambaye nimeleta mpango wa Mkurabita Ngara kwa sababu naamini ni ukombozi kwa Mtanzania wa kawaida.

Kupitia mpango huo mashamba ya kaya yatapimwa na kupewa hati miliki ya kimila ambayo inaweza ikatumika kama mdhamana na kupatia mikopo kutoka Benki.

 Nakubaliana na baba Askofu Kijanjari kwamba kwa kupitia utaratibu huu wa Mkurabita tunaweza kumaliza mgogoro wa wakulima na wafugaji.

8. Hadija Hussen wa kata Bugarama- Ngara.

Uliahidi kijiji chetu cha Rwinyana kitapata maji kupitia Benki ya Dunia lakini hadi leo hatuna maji hatuna zahanati wala kituo cha afya na wanawake tulio na bima za afya ukienda Hospitali huudumiwi kama mwenye fedha tasilimu. Je, wewe unafanya jitihada gani kutusaidia sisi wanawake?

Jibu: Mradi wa maji kwa kijiji cha Rwinyana chini ya mradi wa maji wa Benki ya Dunia ulishaanza, lakini unasuasua kwa sababu Serikali inatafuta fedha na imeahidi kumaliza tatizo la maji kwa kijiji hicho kabla ya Juni mwaka huu. 

Bima ya Afya ni muhimu sana kwa mwananchi yeyote. Tatizo la watoa huduma wakorofi ni la muda, tatizo kubwa lililopo ni upungufu wa dawa ambalo linashughulikiwa na Serikali. 

Wananchi wa Rwinyana sasa hivi wanatumia Kituo cha Afya Bukiriro na Sera ya Serikali ni kuwa na kituo cha afya kila kata na zahanati kila kijiji. Naamini fedha za Serikali ikiboreka kata ya Bugarama inapata kituo cha afya.

9. Martin Mwampamba mkazi wa Rulenge.

Wakati  ukiomba kura kwa wananchi ulisema mara vikao vikiisha utakuja kuishi jimboni siyo Dar es Salaam. Je? Mbona hadi unamaliza kipindi chako cha uongozi hukai jimboni na kufanya mikutano ya hadhara na wananchi kusikiliza kero zao? Ahadi hiyo imekuaje ukashindwa kuitekeleza?

Jibu: Ndugu Martin Mwampamba unajua fika kwamba huwa nakuja Rulenge nyumbani kwangu na huwa nahudhuria mikutano ya kijiji cha Rulenge na kufanya mikutano ya hadhara lakini ukumbuke kwamba ninapokuwa Dar es Salaam nakutana na watendaji wa wizara pamoja na mashirika kama REA na kujadili masuala ya umeme. 

Mara nyingi natembea wizara ya maji kuwaomba watoe fedha kwa ajili ya maji ndiyo maana tumeweza kupata umeme wa Rulenge na maji kwa ajili ya vijiji vya Rulenge na Munjebwe. 

Huwa nagawa muda wangu kati ya Ngara na Dar es Salaam ‘Akanyoni katugurutse ntikamenya iyo bweze’ nikikaa Rulenge muda wote haisaidii kimarendeleo.

10. Seth  Feruzi mkazi wa Ngara Mjini.

Uliahidi vijana wa mijini na vijijini kuwaunganisha na kuwapatia vifaa vya michezo ili washiriki kwenye timu mbalimbali na kucheza ligi hadi ngazi ya Taifa cha kushangaza hakuna timu uliyoipatia vifaa vya michezo wala kuanzisha ligi ya mbunge. Je, ahadi hiyo unategemea kuitekeleza lini kwa wananchi wa jimbo lako?

Jibu: Sikutoa ahadi ya kutoa vifaa vya michezo kwa vijana wa mijini na vijijini. Hata hivyo nimetoa jezi na mipira kwa baadhi ya vijiji nitaendelea kufanya hivyo kwa kipindi kidogo kilichobaki.

Source:-Mwananchi.

UNGANA  NASI KATIKA  FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad