MTANZANIA.
Kesi 18 za dawa za kulevya zilizokuwa zikisikilizwa Mahakama Kuu
Kanda ya Dar es Salaam zinafutwa kwa sababu zilisajiliwa kimakosa katika katika
mahakama hiyo na washtakiwa wanapandishwa upya kizimbani.
Hayo yalibainika jana baada ya kesi nne kufutwa na kufanya idadi
ya kesi hizo kufikia nane baada ya nne nyingine kufutwa juzi, ambapo washtakiwa
walisomewa upya mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu.
Kesi zote zinazofutwa matukio yalitokea kati ya mwaka 2010 na
2011, ambapo upelelezi ulishakamilika na zilipelekwa Mahakama Kuu kwa ajili ya
kuendelea kusikiliza ushahidi.
Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Kamishna Msaidizi
Mwandamizi, Godfrey
Nzowa, alipoulizwa
kuhusu kufutwa mfululizo kwa kesi hizo, alisema kesi hizo zinazofutwa zipo
katika orodha ya kesi zilizopo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wiki hii kwa
ajili ya kusikilizwa.
“Kwa wiki
hii tutafuta kesi 18 ambazo zilianza kufutwa nne juzi, na jana nne, ambapo tatu
zimefikishwa Kisutu na moja imepelekwa mkoani Pwani.
“Kesi
zinazofutwa zimebainika kusajiliwa Mahakama Kuu katika kitabu cha kesi za
uhujumu uchumi, ni makosa, zinarudi upya mahakamani ili washtakiwa waweze
kusomewa mashtaka, na kwa kuwa upelelezi ulikamilika, watasomewa maelezo ya
awali na kurudishwa tena mahakamani,” alisema.
Kamishna Nzowa alisema leo wanatarajia kufuta kesi nyingine nne,
kesho zitafutwa tatu na keshokutwa pia zitafutwa kesi tatu.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga,
alisema kesi za dawa za kulevya zilizosajiliwa kimakosa na Mahakama Kuu katika
kitabu cha kesi za uhujumu uchumi zitaendelea kufutwa.
“Zipo kesi
nyingi na zitaendelea kufutwa kutokana na Mahakama Kuu kufanya makosa
kuzisajili katika kitabu cha kesi za uhujumu uchumi,” Maganga.
NIPASHE.
Watendaji wa kata ya Mkolani Mwanza wameagizwa kufanya haraka
kuwahesabu watu wenye ulemavu wa ngozi ndani ya kata hiyo ili kubaini idadi
yao.
Diwani wa kata hiyo Stansalaus
Mabula alisema
zoezi hiyo linatakiwa kuanza haraka ili kutengeneza ulinzi shirikishi kwa jamii
kuwalinda albino waliopo ndani ya kata yake.
“Ili
kuwalinda watu hawa wenye ulemavu wa ngozi, lazima jamii ichukue hatua ya
kukomesha mauaji yanayowalenga na kila mmoja awe mlinzi wa mwingine ili
kukomesha tabia hii“- Mabula.
Mabula alisema ulinzi huo unatakiwa kuanzia majumbani ili
kurahisisha kuwabaini wenye nia ya kuwadhuru watu hao ambao hawana hatia.
NIPASHE.
Rais Jakaya
Kikwete amesema
serikali itaendelea kuboresha mazingira ya walimu nchini, lakini inatofautiana
nao katika suala la kuongeza mishahara kutokana na wao kutaka kuongezwa
kwa kiwango cha asilimia 100.
Amesema hayo jana katika hafla ya kukabidhiwa vitabu milioni 2.5
vya sayansi, fizikia na hisabati na Balozi wa Marekani nchini,
Mark Childress, vilivyotolewa na serikali ya nchi hiyo kupitia Shirika la
Misaada (USAID).
Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Mtakuja,
Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali, akiwamo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Tamisemi-Elimu), Kassimu Majaliwa.
“Tutaendelea
kuongeza uwekezaji kwenye sekta ya elimu. Tutaendelea kuboresha mazingira ya
walimu. Na msanii ameimba hapa suala la maslahi. Tunatofautiana na walimu
sababu wanataka waongezwe kwa asilimia 100, lakini yote hayo tunaendelea
kuyaangalia na kuongeza taratibu,” alisema.
Kuhusu usambazaji wa vitabu hivyo, alisema kazi hiyo iliyoanza
Januari 2, imeshafanyika na imekamilika Januari 25, mwaka huu na ilifanywa
na Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuzitaka taasisi za serikali
kuangalia uwezekano wa kulitumia jeshi katika kazi za halali.
Naye Balozi wa Marekani nchini, Childress alisisitiza umuhimu wa
kuimarisha stadi za msingi kwa wanafunzi, ambazo ni kusoma, kuandika na
kuhesabu ili kuwawezesha kuelewa vyema maudhui ya vitabu hivyo na kuyatumia
kikamilifu.
NIPASHE.
Vurugu kubwa zimeibuka katika Kijiji cha Ilula, Wilaya ya Kilolo
mkoani Iringa baada ya wananchi kufunga barabara kuu ya Iringa-Morogoro,
kuchoma matairi, kujeruhi watu na kuharibu magari kadhaa yakiwamo ya polisi
kufuatia kifo cha mwanamke mmoja anayedaiwa kuponzwa na operesheni ya polisi ya
kuwasaka watu wanaojihusisha na unywaji wa pombe wakati wa saa za kazi.
Mwanamke anayedaiwa kufa katika msako huo wa wanywaji wa pombe
mchana na kuwa chanzo cha kuibuka kwa hasira za wananchi ametajwa kwa jina la Shida Mtandi.
Inadaiwa
alifariki dunia wakati askari walipokwenda kijijini hapo kusaka watu
wanaokunywa pombe mchana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mvungi alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema
yupo nje ya mkoa huo na kutoa maelekezo kwamba atafutwe kaimu wake, Pudensiana
Protace.
Naye
alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi hakupatikana.
Taarifa zaidi kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa katika vurugu
hizo watu wanne wamejeruhiwa akiwamo Mkuu wa Kituo cha Polisi Ilula.
Inaelezwa kuwa wananchi walivamia kituo hicho cha polisi na
kuchoma moto magari manne na pikipiki moja.
Mashuhuda walisema kuwa vurugu hizo zilianza jana saa 6:45 mchana
na kusababisha magari yaliyokuwa yakisafiri kutoka mikoa ya Nyanda za Juu
Kusini na nchi jirani kwenda Dar es Salaam kushindwa kuendelea na safari kwa
zaidi ya masaa mawili kutokana na barabara hiyo kufungwa.
NIPASHE.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba,
amesema uandikishaji wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa
kutumia mfumo wa Biometric Voter Registration (BVR), haupaswi
kuharakishwa, kwani baada ya kazi hiyo, ni lazima Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ifanye uhakiki wa majina ya
wapigakura.
Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na
Independent Television (ITV), alisema kwa uzoefu wake alipokuwa kiongozi wa
timu ya waangalizi wa uchaguzi wa Jumuiya ya Madola nchini Malawi miaka 11
iliyopita, alibaini kuwa mfumo huo unaweza kuandikisha mtu mmoja mara mbili
hadi nne.
“Tulikuta
wanatumia BVR, utaratibu huu ni mzuri kwa kuzuia udanganyifu. Nchi ya Malawi
ina takriban watu milioni tisa. Lakini tulikuta watu milioni sita
wamejiandikisha. Tunaona haiwezekani zaidi ya theluthi mbili wajiandikishe
kwenye uchaguzi,” alibainisha.
Aliongeza: “Tulibaini
wengi walijiandikisha mara mbili tatu, nne, utaratibu huu ukijiandikisha majina
mawili unafuta unabakiza moja, na hiyo ni muhimu tume ikishaandikisha lazima
ihakiki, isipohakiki lazima yatafutwa, mtu atakuja kwenye kituo jina lake
halipo na la mwingine lipo mara mbili na kulalamika.”
Alisema baada ya uandikishaji kumalizika ni lazima Nec ihakiki
majina hayo kabla ya kuanza kutumika kwa daftari hilo.
Jaji Warioba alirejea kauli yake kuwa kura ya maoni haiwezekani
kufanyika Aprili 30, mwaka huu, kama ambavyo serikali imeeleza kutokana na
sababu mbalimbali.
Alizitaja sababu hizo kuwa ni Nec kuandikisha wapigakura, ambao
pia watapiga kura katika Uchaguzi Mkuu, huku sheria ikiruhusu kuandikisha
vijana, ambao hawajafikisha miaka 18, ambao Oktoba, mwaka huu, watakuwa
wamefikisha umri huo.
HABARI LEO.
Watendaji wa Halmashauri waliokaa kwenye vituo vya kazi kwa zaidi
ya miaka 10 , wataanza kuhamishwa wakati wowote kuanzia sasa kuleta ufanisi
katika utendaji na kukomesha kufanya kazi kwa mazoea.
Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda ameagiza
ofisi za mikoa ziainishe majina ya watendaji husika, utaratibu wa kuwahamisha
ufanyike kunusuru utendaji wa kazi kwenye maeneo walikokaa muda mrefu. Alitoa
agizo hilo juzi wilayani Mufindi katika mkoa wa Iringa.
Alisema serikali imebaini watendaji wanaokaa kwenye vituo vya kazi
kwa miaka 10 na zaidi kwenye halmashauri, wanakuwa kikwazo cha utendaji kazi
wenye ufanisi kutokana na kufanya kazi kwa mazoea badala ya kitaalamu.
Alisema, “Niliwahi kwenda kutembelea halmashauri fulani nikamkuta
mzee mmoja amekaa hovyo kwa kujiachia achia tu na kusahau kuwa ni mtendaji wa
serikali. Ilibidi nimuulize, mzee nawe umo, akasema , ndio mheshimiwa.
Nikashangaa,
hata huyu! Kwa jinsi hivi alivyo atafanya kazi vizuri kweli?” “…Nilipomwuliza
nilipata majibu yaliyodhihirisha kuwa alikuwa alivyo na kutenda kazi kwa mtindo
aliokuwa akiufuata kwa sababu ya mazoea yaliyotokana na kuwepo kwenye
halmashauri husika kwa zaidi ya miaka 10, hii haikubaliki kwa watendaji wa
halmashauri”.
Pinda alisisitiza, kuwepo kituoni kwa muda mrefu kwa watendaji
katika halmashauri ni miongoni mwa udhaifu unaotoa mwanya wa wizi wa fedha za
halmashauri kwa sababu wanakuwa wakifahamu mbinu za kuiba na jinsi ya kukwepa
kujulikana uhusika.
“Huu ni
ukweli na ushahidi tumeuona katika maeneo ambako watumishi walikuwa wakiiba
fedha. Kuwapangua kulisaidia sana kunusuru fedha zisiibwe katika baadhi ya
halmashauri zilizokuwa na matatizo ya kifedha kutokana na wizi wakati wa
kukusanya kodi na ushuru mbalimbali,” – Pinda
HABARI
LEO.
Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) kitatumia
Dola za Marekani bilioni 1 katika kujenga miundombinu ya elimu Afrika Mashariki
kati ya hizo Dola za Marekani milioni 700 zitawekezwa Tanzania.
Akizungumza wakati wa mkusanyiko wa wahitimu uliokwenda sambamba
na kutimiza miaka 15 kwa chuo hicho tangu kuanza kufanya shughuli zake Afrika
Mashariki, Rais wa AKU, Firoz
Rasul alisema
kiasi hicho kitatumia katika kujenga kampasi Tanzania, Kenya na Uganda ndani ya
miaka 15 ijayo.
“Lengo letu ni kuzalisha wahitimu ambao si tu wako tayari kwa
ajili ya kupata ajira, lakini ambao wana ujuzi na wanaoweza kujiajiri na
kutengeneza ajira mpya.
Hivyo,
kila kampasi yetu itakuwa ikiwahudumia wanafunzi kutoka nchi zote za Afrika
Mashariki,” alisema.
Alisema kuwa uwekezaji huo utakaoanza mwaka 2015 hadi 2029 kwa
Tanzania utachangia wastani wa Dola bilioni 6.3 kwenye uchumi na kuongeza
udahili wa wanafunzi 10,000 kutoa ajira za moja kwa moja kwa watu 10,000 na
ajira zisizo za moja kwa moja zipatazo 30,000.
Akifafanua zaidi, kampasi ya Dar es Salaam itakuwa kitovu cha
kuwafundisha walimu bora wa viongozi wa shule kitatoa shahada katika kitivo cha
sayansi.
Alisema kampasi ya Nairobi itakuwa kitovu cha sayansi ya afya na
kozi ya uandishi wa habari na mawasiliano ambacho kitatoa mafunzo kwa waandishi
wa habari na viongozi katika vyombo vya habari wakati Kampala italenga mafunzo
ya uongozi na utawala katika sekta binafsi, za umma na kijamii.
MWANANCHI.
Mwanamke mmoja ameieleza mahakama ya nchini Kenya kwamba
alilazimika kumuuza mtoto wake wa siku tano kutokana na umaskini wa kupinfuka
ambao ulisababisha kukosa fedha za kumtunza mtoto huyo.
Mama wa mtoto huyo Virginia
Mwangi aliiambia
Mahakama ya Nyeri kwamba alilazimika kumuuza mtoto huyo Shilingi 7,00 kwa Eunice Wangeci Kibira ambaye pia alishtakiwa kwa kosa hilo.
Wanawake hao wawili wanakabiliwa na mashtaka manne ya kushirikiana
katika biashara ya kumuuza mtoto huyo kinyume na sheria ya watoto.
Mwangi alikiri makosa hayo mbele ya mahakama hiyo lakini Wendi
alikanusha mashtaka na kuachiwa kwa dhamana ya shilingi 50,000.
JAMBO LEO.
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imeingilia kati tukio la mwalimu
wa Sekondari ya Kibasila, Gaudensia
Albert kukaa na
kinyesi ,mende na funza ndani kwa muda wa miaka miwili na kutaka kumchukulia
hatua.
Ofisa Afya Manispaa ya Temeke Willium Mihemu alisema kwa sasa yupo
kwenye mikakati ya kujiandaa kushirikiana na na askari polisi kumchukulia
hatua mwalimu huyo anayefundisha masomo ya sayansi hapo shuleni.
“Leo sisi
na Polisi tutaungana ili kwenda kumkamata,kwani kwa hali ya kawaida inaonekana
mwalimu huyo hana akili timamu“-Mihemu.
Kwa upande wa mwenye nyumba Ruben
Shayo ambaye
wanaishi eneo la Yombo Visiwani alisema kuwa licha ya kufanya tukio hilo kwa miaka
miwili mfululizo lakini bado alimruhusu kuendelea kuishi ndani ya nyumba yake
na kumtaka kuondoa kinyesi hicho.
Shayo alisema hajawahi kumuona mwalimu huyo akimwingiza mgenindani
ya nyumba hiyo badala yake alikua akimalizana nao nje ya chumba chake.
UNGANA NASI KATIKA FACEBOOK , TWITTER , INSTAGRAM , Pia tutumie tukio la Picha kwa WhatsApp +255789925630.
Source:-Millard
Ayo.
|
Wednesday, February 25, 2015
Home
HABARI
HABARIKA / MAGAZETINI:-Leo February 25, 2015 hapa Ni STORI 9 zilizogonga Vichwa vya Habari.
HABARIKA / MAGAZETINI:-Leo February 25, 2015 hapa Ni STORI 9 zilizogonga Vichwa vya Habari.
Tags
# HABARI
Sambaza Hii
Chief Editor | Mhariri
HABARI
Labels:
HABARI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Kuhusu Mwandishi
Journalist / Chief Editor / Tanzanian Blogger
Simu: 0756830214 / 0620197747 / 0789925630.
No comments:
Post a Comment