Mtuhumiwa wa
kesi ya dawa za kulevya, raia wa Sierra Leone (33), Abdul Koroma, (Pichani kushoto) amepigwa risasi
na kufa baada ya kujaribu kutoroka akiwa chini ya ulinzi wa askari wa Jeshi la
Magereza, jijini Dar es Salaam.
Mtuhumiwa huyo alipigwa
risasi jana Desemba 31,2014 asubuhi, wakati akitaka kukimbia kwa kuruka uzio wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na kuzua taharuki kubwa
mahakamani hapo.
Askari Magereza mmoja ambaye
aliomba jina lake lisitajwe kwa kuwa si msemaji wa jeshi hilo, aliiambia
NIPASHE kuwa Koroma alifikishwa katika mahakama hiyo akitokea katika Gereza la
Keko.
Koroma alikuwa akikabiliwa na
shtaka la kuingiza nchini dawa za kulevya aina ya cocaine gram 1,229 zenye
thamani ya Sh. milioni 61.4.
Alikamatwa Desemba 02, mwaka
2013 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa na dawa hizo.
Kesi hiyo namba PI 21/2013,
ilikuwa mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo,
Augustina Mmbando, na baadaye ilihamishiwa kwa Hakimu Warialwande Lema,
ambaye alikuwa akiendelea kuisikiliza.
Kesi hiyo ilikuja jana
Desemba 31,2014, katika mahakama hiyo kwa ajili ya kutajwa.
Hadi marehemu anataka kutoroka,
upelelezi wa kesi dhidi yake ulikuwa bado haujakamilika.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa
muda mfupi baada ya kufikishwa katika mahakama hiyo, mtuhumiwa huyo aliomba
kwenda chooni kujisaidia na kusindikizwa na askari.
Askari aliyekuwapo eneo la
tukio, alisema kuwa mtuhumiwa baada ya kumaliza kujisaidia, alivua suruali yake
aina ya jeans na kubaki na kaptura huku suruali hiyo akiishika mkononi.
Muda mfupi baadaye, Koroma
(mtuhumiwa), alijirusha kutoka katika choo hicho chenye vioo ambacho ni maalum
kwa ajili ya mahabusu na kujeruhiwa na vioo ambavyo vilimkatakata katika maeneo
kadhaa ya mwili wake.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa
mtuhumiwa huyo baada ya kuruka kutoka katika choo hicho licha ya kujeruhiwa,
alianza kutimua mbio na ndipo askari walipoanza kumfukuza wakiwa na silaha za
moto.
Askari hao wakati wakiwa
katika harakati za kumfukuza, walianza kupiga kelele kuwaomba walinzi wa
mahakama hiyo kufunga geti la kuingia na kutoka ili mtuhumiwa huyo asitoke nje
ya uzio wa mahakama.
Mtuhumiwa huyo baada ya kuona
geti limefungwa, alibadili uelekeo na kwenda kwenye ukuta wa mahakama ambao
ulikuwa na nondo na kujaribu kuruka.
Askari waliokuwa wakimfukuza
waliwaeleza wenzao kwamba wasimpige risasi kwanza kuepuka kuwajeruhi au
kuwadhuru watu wengine wasiokuwa na hatia na kwamba wasubiri hadi afike eneo
zuri.
Kutokana na mtuhumiwa huyo
kukaidi amri ya kutakiwa kusimama, askari mmoja alipiga risasi mbili hewani,
lakini marehemu hakujali na kuendelea kuparamia ukuta wenye nondo.
Hata hivyo, wakati anajaribu
kuruka, fulana yake ilinasa kwenye nondo na ndipo mlinzi mmoja aliyefahamika
kwa jina moja la Mwakasisi, alifanikiwa kumshika mguu mtuhumiwa huyo ndipo
Askari Magereza alipofyatua risasi zilizompata mtuhumiwa.
Risasi hiyo zilimpata mtuhumiwa
huyo kwapani na kutokea kichwani na hivyo kunasa juu ya nondo za uzio wa
mahakama hiyo.
Baadaye, yalifika magari
matatu ya Jeshi la Polisi na askari wawili walipanda kwenye uzio huo na
kumnasua mtuhumiwa huyo huku akivuja damu nyingi na kumpeleka katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Kwa upande wake, Kamanda wa
Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alithibitisha kupigwa
risasi kwa mtuhumiwa huyo ambaye alifariki dunia kabla ya kufikishwa katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kamanda Kova alisema Jeshi
hilo linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini sababu iliyosababisha mtuhumiwa
huyo kukimbia akiwa chini ya ulinzi.
Aliwatahadharisha watuhumiwa
kuondokana na majaribio kama hayo kwani yanaweza kuwaathiri raia wasio na hatia
wakati wa kuwakamata.
Naye Ofisa Uhusiano wa
Hospitali ya Taifa ya Muhumbili, Doris Ishenda, alithibitisha kupokea mwili wa
marehemu saa 2:47 na kwamba umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha
hospitali hiyo.
|
No comments:
Post a Comment