Hii ni moja
ya nyumba za Walimu wa shule ya Msingi Mihuga iliyopo Wilayani Bagamoyo.
mazingira ya namna hii yanasababisha walimu wengi kuikimbia fani yao ya ualimu.
Picha na Ibrahim Yamola.
Shirika la
Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, (UNESCO) hivi karibuni limetoa
ripoti inayoonyesha Tanzania itahitaji angalau walimu 406,600, ifikapo mwaka
2030.
Wakati
mahitaji ya walimu katika nchi mbalimbali yakizidi kuwa makubwa, shirika hilo
linasema uhaba wa walimu wenye mafunzo unazidi kutamalaki katika nchi
mbalimbali, ikiwamo Tanzania.
Kwa sasa na
inawezekana na baadaye, Afrika ndiyo inayoongoza kwa kuwa na uhaba mkubwa wa
walimu, jambo linalohatarisha mustakabali wa sekta ya elimu barani humu.
Ukiondoa
Tanzania, ripoti hiyo inaonyesha mahitaji makubwa ya walimu pia yanazikabili
nchi kadhaa za Afrika, zikiwamo Uganda, Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC).
Kwa ngazi ya
dunia ripoti hiyo inasema hadi mwaka huo, walimu zaidi ya milioni 27
watahitajika kuziba mapengo ya walimu wanaostaafu na nafasi mpya za ajira.
Hata hivyo,
taarifa nzuri ya ripoti hiyo inaonyesha kama Tanzania itajipanga vizuri,
inaweza kuziba pengo la walimu , hasa katika shule za msingi ifikapo mwaka
2026.
Hilo linawezekana ikiwa nchi hiyo itakuwa inaajiri angalau asilimia 10 ya
walimu kila mwaka.
Hata hivyo,
Unesco inasema mikakati ya kuziba mianya hiyo ya walimu katika nchi nyingi
imegubikwa na dosari kubwa kwa vyombo husika kuajiri walimu wasio na mafunzo
bora ya ualimu.
“Takwimu
zinaonyesha kuwapo kwa tatizo sugu la walimu wasio na mafunzo katika nchi
nyingi. Kama hatua hazitochukuliwa, itakuwa vigumu kwa watoto wote kwenda shule
na kujifunza,” inasema taarifa ya Unesco iliyotolewa kwa umma.
|
No comments:
Post a Comment