Halmashauri ya Wilaya ya Ngara inadaiwa kukumbwa na kashfa
ya ubadhirifu wa fedha za umma katika miradi mitatu kwenye maeneo tofauti hali
ambayo Kamati ya Utekelezaji ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera imeamuru
irudiwe na kukamilishwa.
Ubadhirifu
huo uligundulika baada ya kamati hiyo kufanya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya
maendeleo juzi kwa lengo la kutathmini na kujiridhisha utekelezaji wa Ilani ya
chama ya mwaka 2010.
Pia ililenga
kujiridhisha kama fedha inayotolewa na serikali ya chama hicho inafanya
shughuli zilizokusudiwa na kwa viwango.
Ikiongozwa
na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera,Bi. Costansia Buhiye, ilibaini nyumba ya walimu
katika Shule ya Msingi Ngoma iliyoko Kata ya Kasulo iliyojengwa kwa gharama ya
Sh milioni 45 kuwa chini ya kiwango.
Kamati hiyo
iliagiza ndani ya siku saba Halmashauri imtafute mkandarasi aliyejenga nyumba
hiyo, aondoe milango, vigae na nyavu za madirisha na kuweka vingine kutokana na
vilivyowekwa kuwa chini ya kiwango ikilinganishwa na fedha zilizotumika.
Ubadhirifu mwingine umebainika katika Mradi wa Maji katika Kijiji cha Nterungwe,
Kata ya Nyamiaga.
Ilibainika
mradi huo uliojengwa tangu mwaka 2004, maji hayajawahi kutoka licha ya
Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kutenga zaidi ya Sh milioni moja kila mwaka kwa
ajili ya kufanya ukarabati wa mradi huo ‘hewa’.
Kamati
ilimwagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw.Cornel Ng'udungi kuhakikisha mradi huo unakamilika
haraka iwezekanavyo ili kuondoa kero kwa wananchi wa eneo hilo ambao hutembea
umbali wa kilometa 10 kufuata maji.
Mradi
mwingine ni wa upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya maji Ngara mjini ambao Sh
milioni 150 zilitolewa na Rais Jakaya Kikwete.
Pia ilibainika katika fedha
hizo, zaidi ya Sh milioni 32 zimetumika tofauti na utaratibu.
Hata hivyo,
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanal Fabian Massawe aliiambia kamati hiyo kuwa baada ya
kugundua ubadhirifu huo, Meneja wa Mamlaka ya Maji Ngara,Bw. Edward Magai (60)
amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
|
No comments:
Post a Comment