Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana Agosti 31,2014,waligoma
mbele ya Rais Jakaya Kikwete kuruhusu wajumbe wao kurejea katika Bunge Maalumu
la Katiba, walipokutana katika kikao cha kusaka suluhu ya mkwamo wa mchakato wa
Katiba.
Mkutano wa jana ulikuwa na sehemu mbili kuu, wa kwanza ulifanyika katika
Ikulu ya Kilimani, Dodoma ambako viongozi hao walikutana na Rais Kikwete na
mwingine katika Hoteli ya St. Gasper ambao uliwashirikisha viongozi na maofisa
wa vyama vilivyoshiriki bila Rais Kikwete.
Mkutano huo ni matunda ya jitihada zinazofanywa na Kituo cha Demokrasia
Tanzania (TCD) ambacho kiliratibu mazungumzo hayo yaliyochukua zaidi ya saa mbili
na nusu, katika Ikulu ya Kilimani, wakati yale ya St. Gaspar yalichukua
takriban saa moja na nusu.
Viongozi walioshiriki kikao hicho cha Ikulu ni Makamu Mwenyekiti wa CCM
(Tanzania Bara), Philip Mangula, Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana,
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu
Lissu, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu wa CUF
(Tanzania Bara), Magdalena Sakaya.
Wengine ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, Katibu Mkuu wake,
Mosena Nyambabe, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, Mwenyekiti wa UDP ambaye
pia ndiye mwenye zamu ya uenyekiti wa TCD, John Cheyo na Mwenyekiti wa UPDP
pamoja na mwakilishi wa vyama visivyokuwa na wabunge ndani ya TCD, Fahmi
Dovutwa.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema Rais Kikwete baada ya kuanza
kwa kikao hicho alitoa fursa kwa kila aliyekuwapo kuzungumza na hapo
zilijitokeza hoja mbalimbali, nyingi mwelekeo wake ukiwa ni kutaka kusitishwa
kwa Bunge Maalumu ili kutoa fursa kwa nchi kuendelea na masuala mengine
makubwa.
Chanzo chetu kilisema: “Rais amekuwa msikivu kweli, amewasikiliza wote
lakini ugumu ulianza kuonekana pale ilipotolewa kauli ya kuwauliza wale watu wa
Ukawa kama wanaonaje wakirejea halafu hoja zao zikazungumzwa ndani ya Bunge
Maalumu, yaani hawataki kabisa kusikia hilo.”
Kuhusu hoja ya kusitishwa kwa Bunge, habari zinasema ilijadiliwa kwa
kirefu na wataalamu wa sheria wakijaribu kutoa uzoefu wao, lakini kikwazo
kilichoonekana ni Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo haimpi Rais mamlaka ya
kusitisha Bunge.
“Rais alisema hoja zao ni nzuri na zina mashiko, lakini suala kubwa
likawa ni kwamba tunafikaje huko wanakopendekeza? Maana sheria iko kimya kuhusu
mamlaka ya Rais kusitisha Bunge Maalumu, ndiyo maana sasa tulitoka Ikulu tukaenda
St. Gaspar ili kujadili, ngoja tusubiri hiyo tarehe 8 maana siyo mbali,”
alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.
|
No comments:
Post a Comment