Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba
imewasilisha Rasimu ya Katiba inayopendekezwa ikionyesha jinsi ilivyoifumua
rasimu iliyowasilishwa bungeni hapa mwanzoni mwa mwaka huu na aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Rasimu hiyo iliwasilishwa bungeni Septemba
24,2014 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Andrew Chenge ambapo imeongeza mambo ya
muungano kutoka saba yaliyopendekezwa na rasimu ya Warioba hadi 14.
Kwa mujibu wa Chenge, rasimu hiyo ina sura
17, ibara 274 na katika ibara hizo, 233 zimetokana na rasimu ya Jaji Warioba.
Alisema pia kwamba ibara 47 za rasimu ya Jaji
Warioba hazikufanyiwa marekebisho, ibara 186 zimefanyiwa marekebisho ya
uandishi na kimaudhui, ibara 28 zimefutwa kabisa na pia zimeongezwa ibara mpya
41.
Pia alisema wakati wa kuandika rasimu hiyo,
wajumbe walichukua mambo machache ya msingi na mengine yaliachwa ili yaandaliwe
mazingira ya kuyatungia sheria kwa kuwa Katiba haiwezi kubeba kila kitu.
SURA YA KWANZA
Katika sura hii inayozungumzia muundo wa
Serikali, Bunge Maalumu la Katiba katika rasimu yake, limependekeza muundo wa
Serikali mbili tofauti na muundo wa Serikali tatu zilizokuwa zimependekezwa na
Tume ya Jaji Warioba.
Kwa maana hiyo, mapendekezo ya uwapo wa
Serikali ya Shirikisho lenye mamlaka kamili yaliyotokana na mapendekezo ya
muundo wa Serikali tatu yametupwa rasmi.
Akizungumzia kutupwa kwa Serikali tatu,
Chenge alisema kumetokana na kuhofia uwapo wa mgawanyiko katika jamii pindi
nchi itakapokuwa na muundo wa Serikali tatu.
Kwa upande wa tunu za taifa ambazo ziko
katika sura hii, rasimu mpya imezitaja kuwa ni lugha ya Kiswahili, muungano,
utu na udugu pamoja na amani na utulivu tofauti na ilivyo katika Rasimu ya
Warioba ambapo tunu hizo zimetajwa kuwa ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja,
uwazi, uwajibikaji na lugha ya taifa.
SURA YA PILI
Sura hii inayozungumzia malengo muhimu,
misingi ya mwelekeo wa shughuli za Serikali na sera za taifa, Bunge Maalumu la
Katiba limeongeza majukumu kwa Bunge kutakiwa kutunga sheria itakayofafanua juu
ya utekelezaji wa malengo muhimu kwa mujibu wa Katiba.
Katika sura hii, baadhi ya mambo
yaliyoongezwa yalitokana na mchango uliotolewa na kada wa CCM, Kingunge
Ngombale Mwiru aliyetaka Katiba ieleze wazi juu ya masuala ya kiuchumi kwa
kuhimiza mapinduzi ya kilimo, ufugaji, uvuvi, mapinduzi ya viwanda na kujenga sekta
muhimu za nishati, mawasiliano na miundombinu.
SURA YA TANO
Sura hii inayozungumzia haki za binadamu,
wajibu wa raia, jamii na mamlaka za nchi, katika rasimu mpya, vijana
wanaruhusiwa kuanzisha baraza lao la taifa wakati katika rasimu ya Jaji Warioba
baraza hilo halikuwapo.
SURA YA SABA
Katika rasimu mpya, sura hii inayozungumzia
muundo wa Jamhuri ya Muungano, Bunge Maalumu linapendekeza Tanzania kuundwa na
Serikali mbili ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar wakati Rasimu ya Jaji Warioba ilipendekeza muundo wa
Shirikisho lenye Serikali tatu.
Rasimu hiyo inazitaja serikali hizo kuwa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya
Tanganyika.
SURA YA TISA
Sura hii katika rasimu mpya inahusu uhusiano
na uratibu wa mambo ya muungano, lakini katika rasimu ya Warioba inahusu
uhusiano na uratibu wa Serikali.
Katika rasimu mpya sura hii katika ibara ya
122 inasema kutakuwa na Tume ya Usimamizi na Uratibu wa Mambo ya Muungano
itakayoitwa Tume ya Mambo ya Muungano, lakini Tume ya Jaji Warioba ilipendekeza
tume hiyo iitwe Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali.
Katika rasimu mpya imependekezwa tume hiyo
iwe na wajumbe ambao ni Makamu wa Kwanza wa Rais atakayekuwa Mwenyekiti, Waziri
Mkuu, kiongozi wa shughuli za Serikali katika Baraza la Wawakilishi na mawaziri
wenye dhamana ya Muungano.
Lakini katika rasimu ya Jaji Warioba wajumbe
waliopendekezwa ni makamu wa rais atakayekuwa mwenyekiti, rais wa Tanganyika,
rais wa Zanzibar, mawaziri wa kazi, mawaziri wenye dhamana ya mambo ya nje wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
SURA YA KUMI
Sura hii inahusu muundo wa Bunge la Muungano
na katika rasimu mpya inasema kutakuwa na wabunge watano watakaoteuliwa na rais
ambapo inafanana na ilivyopendekezwa na Tume ya Katiba.
Kitendo cha kuwapo kwa mapendekezo hayo
kunatofautiana na mapendekezo ya vyama vya walemavu ambao walitaka wawe
asilimia tano ya wabunge wote.
Katika rasimu mpya, Bunge Maalumu la Katiba
limependekeza idadi ya wabunge isizidi 360 wakati Rasimu ya Warioba
ilipendekeza wabunge 75 katika Bunge la Muungano.
Hata hivyo, rasimu hii mpya haikueleza wazi
jinsi wabunge wa viti maalum watakavyopatikana ingawa wakati wa mijadala ya
Bunge, wajumbe wanawake walikuwa wakitaka wagombee sambamba na wabunge wanaume.
BONYEZA HAPA KUSOMA==> RASIMU ILIYOPENDEKEZWA BUNGE MAALUMU LA KATIBA
|
Friday, September 26, 2014
Home
SIASA
KATIBA TANZANIA:-Soma sura hizi zilivyoandikwa na Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba ikiwa na sura 17, ibara 274 .
KATIBA TANZANIA:-Soma sura hizi zilivyoandikwa na Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba ikiwa na sura 17, ibara 274 .
Tags
# SIASA
Sambaza Hii
Chief Editor | Mhariri
SIASA
Labels:
SIASA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Kuhusu Mwandishi
Journalist / Chief Editor / Tanzanian Blogger
Simu: 0756830214 / 0620197747 / 0789925630.
No comments:
Post a Comment