JAMII YETU:-Mzazi atiwa mbaroni kwa kumzuia binti wake asifanye mtihani wa Dasara la 7-Bukombe. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Saturday, September 13, 2014

JAMII YETU:-Mzazi atiwa mbaroni kwa kumzuia binti wake asifanye mtihani wa Dasara la 7-Bukombe.

Wakati wanafunzi wa darasa la saba Septemba 10 hadi 11,2014, walifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi, mzazi mmoja mkazi wa Bukombe, amejikuta akiingia matatani na vyombo vya dola kutokana na kumzuia binti wake asifanye mtihani, kwa kile kinachoelezwa alihofia akifaulu angekwamisha mpango wake wa kutaka kumuozesha.

Mwanafunzi aliyezuiwa (jina tunalo) alikuwa anasoma Shule ya Msingi Ihulike iliyoko Kata ya Ushirombo wilayani Bukombe mkoani Geita.

Hayo yalithibitishwa na Ofisa Elimu ya Msingi wilayani Bukombe, Shadrack Kabanga akisema walipokea taarifa ya ujumbe mfupi wa simu kutoka kwa wasamaria, ukisema mzazi mmoja amemzuia bintiwe (anamtaja jina) asifanye mtihani kwa hofu ya binti huyo kufaulu na kupata fursa ya kuendelea na masomo, jambo ambalo mzazi hakulipenda, kwani dhamira yake ni kumuozesha.

Anasema taarifa hiyo ilipokelewa Septemba 10, siku ya kwanza ya mtihani huo wa siku mbili na kwamba walipokwenda katika shule anayosoma binti huyo, walithibitishiwa kutokuwepo kwa mwanafunzi aliyetajwa.

Majira ya saa kumi za jioni nilikwenda shuleni Ihulike kujiridhisha na kukuta kweli mwanafunzi huyo hakuwepo shuleni kushiriki na wenzake kufanya mtihani ingawa alikuwa amejiandaa na hata dawati la kufanyia mtihani alishapewa,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, alilazimika kwenda Polisi alikopewa askari waliokwenda hadi nyumbani kwa mzazi na kumtia mbaroni, anasubiri kusomewa mashitaka wakati wowote.

Aidha, Kabanga alisema mwanafunzi huyo jana alitarajiwa kufanya mtihani uliosalia kwa kuwa bado ameonesha nia ya kutaka kufanya hivyo.

Ofisa Elimu huyo ametoa wito kwa wazazi wote wenye tabia kama hiyo waache mara moja kuzuia fursa za kusoma za watoto wao, kwani Serikali imejipanga kukabiliana na wazazi wanaokwamisha elimu kwa watoto wa kike.

Huyu atachukuliwa hatua ili awe mfano kwa wengine wenye tabia ya kutaka kusaka utajiri wa haraka kwa kuozesha mabinti zao wanaostahili kuwapo shuleni,” alisema Kabanga.

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Amani Mwenegoha amelaani vikali kitendo hicho, akisema: “Sisi kama Serikali ya Wilaya na Serikali Kuu kwa ujumla wake tunakemea vitendo vya wazazi kama hawa wanaozuia jitihada za Serikali kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu.”

Aliongeza kuwa, Serikali haitavumilia vitendo kama hivi hasa katika maeneo ya wafugaji, wachimbaji wa madini, watu wanaohamahama ovyo ili kuharibu utaratibu wa elimu.

Aidha, Mwenegoha alisema kwa kuwa mtoto huyo ameshindwa kufanya mtihani wa awali, Serikali itahakikisha anafanya mtihani wake wote baada ya kutengewa siku yake ya kufanya hivyo, huku mzazi wake akisubiri kupandishwa kizimbani kujibu tuhuma za kumzuia mwanafunzi kufanya mtihani wake wa kuhitimu elimu ya msingi.

Jumla ya wanafunzi 3,731 wilayani Bukombe walitarajiwa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi uliofanyika kote nchini kwa siku mbili kuanzia Jumatano ya Septemba 10, mwaka huu.

Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo hakupatikana kuzungumzia suala hilo ingawa baadhi ya wasaidizi wake, walikiri kuwapo kwa tukio hilo.

Habari Na:-Habari Leo.
 
UKIONA TUKIO LOLOTE LINATOKEA USISITE KUTUTUMIA PICHA KUPITIA WhatsApp:- 0789-925-630.
 
 Like ukurasa wetu wa facebook  ili habari ziwe zinakuijia punde tu zinapoweka kwenye mtandao huu BONYEZA HAPA

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad