Muuguzi wa
Hospitali ya Wilaya ya Misungwi Proscovia Leopod akimhudumia bi Tecra baada ya
kujifungua .
UKIONA TUKIO LOLOTE LINATOKEA USISITE KUTUTUMIA PICHA KUPITIA WhatsApp:- 0789-925-630.
|
MKAZI wa
Kijiji cha Lupili wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza, Tecla Kazimili (24),
amejifungua watoto wanne, watatu wa kike na mmoja wa kiume kwa njia ya kawaida
katika hospitali mbili tofauti na siku mbili tofauti.
Katika
hospitali ya kwanza, ambayo ni zahanati ya Kijiji cha Lupili Agosti mosi mwaka
huu, Tecla alionekana ana ujauzito wa mtoto zaidi ya mmoja ambapo wakati wa
kujifungua, alizaliwa wa kiume akiwa na kilo 1.6, lakini kwa bahati mbaya
alikufa.
Hata hivyo,
wakunga walishuhudia mzazi huyo akiendelea kuwa na dalili ya kujifungua mtoto
mwingine, lakini akawa amegoma kupita katika njia.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana(Agost 03,2014), Mganga Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Marko Mwita,
alisema baada ya kutokea kwa hali hiyo, alipigiwa simu kuombwa msaada.
“Baada ya kupokea
taarifa hiyo majira ya usiku, nilituma gari la wagonjwa kukimbilia kwenye
zahanati hiyo iliyopo umbali wa kilometa 60 na kumleta mama huyo katika
Hospitali ya Wilaya kwa huduma zaidi,” alisema.
Alisema
alipofikishwa hospitalini hapo, Tecla aliendelea kujifungua mpaka kesho yake
hatimaye idadi ya watoto ikafikia wanne.
“Hili ni
tukio la kwanza katika hospitali hii ya Wilaya, mtu kujifungua watoto wanne, ni
matukio yanayotokea mara chache, lakini tunamshukuru Mungu mzazi anaendelea
vizuri huku watoto wake watatu, wote wa kike kila mmoja akiwa na uzito wa kilo
mbili,” alisema.
Dk Mwita
alisema watoto hao wanahitaji uangalizi na msaada wa hali ya juu, kwani ni
rahisi kupata maambukizi. Alitoa mwito kwa jamii kumsaidia mama huyo, kwani
watoto hao wanahitaji msaada wa hali na mali kwa kuwa maziwa ya mama pekee
hayatawatosheleza.
Akizungumzia
historia yake ya uzazi, Tecla alisema watoto hao ni uzazi wake wa nne na katika
ule uliopita, watoto wote aliowazaa walifariki dunia katika umri tofauti,
lakini wa utoto.
“Kitendo cha
watoto kufa baada ya kufikisha umri fulani, kilimfanya mume wangu anifukuze,
nikalazimika kurejea nyumbani kwetu ambapo nilipewa ujauzito na kijana
mwingine,” alisema.
Alisema
wakati anahudhuria kliniki, alielezwa kwamba alikuwa na zaidi ya mtoto mmoja
baada ya kutoa taarifa kuwa anaona tabia ya ujauzito huo ni tofauti na uzazi
wake uliopita.
“Namshukuru
Mungu kwa kunipatia watoto hawa na naiomba Serikali inisaidie kuwatunza ili
wakue vizuri kwani peke yangu siwezi,” alisema.
Kwa mujibu wa Tecla, aliumwa
uchungu kwa siku tatu na alimaliza kujifungua Agosti 2.
Bi Tecra
hana msaada,na kama unaguswa basi piga simu namba 0768102438.
No comments:
Post a Comment