Baadhi ya viongozi wa kiislamu kutoka nchi za Afrika
Mashariki na kati wameshauriana kuelimisha jamii katika nchi hizo kuepukana na dhana mbaya inayoenezwa na
baadhi ya watu kuwa dini ya kiislamu ni dini ya Kigaidi.
Akifungua Kongamano la kidini la Agosti 15 hadi 17,2014, katika
Jiji la Bujumbura nchini Burundi,Mufti wa nchi hiyo Shekhe Sadick Kajande alisema
dhana inayoenezwa ya waislamu kuwa magaidi inasababisha watu kutoaminiana
katika shughuli za maendeleo.
Shekhe Kajande alisema kuwa dini ya kiislamu
inahamasisha umoja amani na mshikamano na kukataza mabaya kulingana na sheria
za Mungu na hata za kiserikali ambazo hazikubaliwi ikiwa ni pamoja na
kutojihusisha na mauaji.
Alisema kuwa kinachotakiwa kwa waumini wa kiislamu ni
kujihadhari na hamaki kutoka kwa baadhi ya watu wanahamasishana kuuchafua
uislamu bali wazingatie misingi ya imani zao pamoja na kuzingatia sheria za
nchi wanakoishi.
Aidha shekhe Mrisho Kasimu kutoka kivu ya kaskazini
(DRC) amesema kinachotakiwa kufuatwa ni misingi ya imani za dini hiyo kwa
kuamini mungu mmoja malaika wake vitabu na mitume iliyowekwa na Mwenyezi Mungu.
Alisema kuwa imani nyingine ni kuamini kuwepo siku
ya kifo kwa matashi ya allha na kwamba kila jema na baya ni kutokana na kudra
zake muumba ambapo katika kuzingatia Q’urani lazima nguzo tano za kiislamu
zisimamiwe ipasavyo.
Akichangia hoja ya Maendeleo ,Shekhe Mohamad Gamaga
kutoka nchini Uganda alisema waislamu wasisitize vizazi vyao na jamii zinazowazunguka
kuondoa changamoto za elimu ,afya na
amani kwa kupinga uhalifu unaohatarisha usalama.
Gamaga aliwaomba waislamu wa mataifa mbalimbali
kufuata sunna za mtume na sheria za nchi zao ili mradi zile ambazo haziwazuii
kufanya ibada zao kwa Mujibu wa sheria na wao
wasitumie dhana inayoenezwa kujihusisha na uvunjifu wa Amani.
Katika kongamano hilo waumini na viongozi kutoka
nchi za Tanzania, Uganda , Rwanda
Burundi na DRC wamechanga kiasi cha
Faranga Milioni tatu kwa ajili ya kujenga Hospitali ya wanawake nchini Burundi ili kupata sehemu ya kujifungulia watoto wao.
Pamoja na mambo mengine,Waumini hao wamekubaliana kukutana mara kwa mara kujadili
changamoto za kiimani na kuweka mikakati ya kujenga Shule na
Hospitali za kidini kwa nchi wanachama
ambapo kongamano lingine litafanyika Desemba Mwaka huu nchini Uganda.
|
No comments:
Post a Comment