UKIONA TUKIO LOLOTE LINATOKEA USISITE KUTUTUMIA PICHA KUPITIA WhatsApp:- 0789-925-630.
Kuna kila dalili kwamba
mchakato wa Katiba mpya unafikia ukomo kabla ya muda wake baada ya jana Rais
Jakaya Kikwete, kutoa msimamo wake na kujiweka mbali na lawama kwamba ndiye
aliyeingilia mchakato huo, huku Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ukisisitiza
achukue hatua kuukamua.
Hali hiyo inajitokeza wakati
Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, amekwisha kuitisha Bunge Maalum la
Katiba mjini Dodoma kuendelea na ngwe ya pili ya kupitisha rasimu ya Katiba
iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba Aprili, mwaka huu.
Jana (Julai 31,2014) kwa
nyakati tofauti misimamo inayokinzana kuhusu mchakato huu ilitolewa, kwanza na
UKAWA wakisisitiza kuwa ni miujiza kwao kurejea bungeni kama masharti waliyotoa
ikiwamo kujadiliwa kwa rasimu kama ilivyowasilishwa na Tume ya Marekebisho ya
Katiba hayatatekelezwa.
UKAWA pia wanasisitiza Rais
Kikwete aingilie kati kukwamua mchakato huo wakimtuhumu kwamba kwenye hotuba
yake ya ufunguzi ndipo mambo yalipoharibikia.
Hata hivyo, akihutubia Taifa
jana (Julai 31,2014) katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi, Rais Kikwete
alisema hivi karibuni amekuwa akilaumiwa kuwa mambo yalikuwa yanaenda vizuri
mpaka pale alipotoa hotuba ya ufunguzi wa Bunge Maalumu ndipo yalipoharibika.
Pia alisema amekuwa
akilaumiwa kwamba anawezaje kuikana Rasimu ya Katiba ambayo na yeye alikuwa ni
mmoja wa watu waliotia sahihi katika Rasimu hiyo.
Akijibu madai hayo, Rais
Kikwete alisema wanaotoa madai hayo yameitafsiri isivyo sahihi yake katika
Gazeti la Serikali lililotangaza rasmi Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Alisema kwa mujibu wa Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba baada ya Tume kumaliza kazi yake ya kuandika Rasimu ya
Katiba, Rais wa Jamhuri ya Muungano amepewa kazi tatu kufanya.
Alizitaja kazi hizo kuwa ni
kupokea Rasimu hiyo na Taarifa ya Tume kutoka kwa Mwenyekiti, kuitangaza rasmi
Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume kwa watu wote kuiona na kuisoma ndani ya
siku 30 na kuitisha Bunge Maalumu.
Rais Kikwete alisema katika
kutangaza katika Gazeti la Serikali sharti linamtaka anayetangaza ajitambulishe
kuwa yeye ni nani na atie sahihi yake.
Alisisitiza kuwa kwa kufanya
hivyo, hakumfanyi yeye kuwa naye ni mhusika na maudhui ya kila kinachopendekezwa
na Tume.
Aidha, alisema suala lingine
ni madai kwamba alikuwa anapata taarifa ya maendeleo ya mchakato ndani ya Tume
mara kwa mara na sasa inakuwaje atoe maoni tofauti kama aliyoyatoa katika
hotuba yake kwenye Bunge Maalumu.
Alisema ni kweli kabisa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, Makamu wake,
Jaji Agustino Ramadhani na Dk. Salim Ahmed Salim, walikutana na yeye kwa
nyakati mbalimbali kuzungumzia mwenendo wa mchakato.
Hata hivyo, alisema hayakuwa
mazungumzo ya kina kuhusu nini kiwe vipi katika maudhui na mapendekezo ya Tume.
Rais Kikwete aliongeza kuwa
na kwa bahati nzuri alitoa maoni yake mahali penyewe hasa, na kwa uwazi, kwenye
Bunge Maalumu la Katiba.
Hata hivyo, alisema ni muhimu
kusisitiza kuwa hakutoa maoni yake kama maagizo wala kushurutisha na ndiyo
maana kila wakati aliwakumbusha Wajumbe kuwa mamlaka ya uamuzi ni yao.
Wakati Rais Kikwete akiyasema
hayo, UKAWA kwa upande wao wamesisitiza kuwa hawatarajii kama kutatokea muujiza
wa kuwafanya wao kurejea katika Bunge hilo kwa kuwa mpaka sasa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) bado hawajaonyesha dalili za kubadilisha msimamo wao wa muundo
wa serikali mbili badala ya maoni yaliyotolewa na wananchi ya serikali tatu
yaliyomo kwenye rasimu ya katiba.
Akisoma tamko la UKAWA mbele
ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaama jana kuhusu wito wa viongozi wa
dini wa kuwataka kurudi katika Bunge hilo, Mwenyekiti Mwenza wa Umoja huo,
Profesa Ibrahim Lipumba, alisema mpaka sasa hakuna dalili yoyote ya wao kurudi
kwa sababu hawajahakikishiwa madai yao.
Profesa Lipumba alisema
hawatarajii kama kutatokea muujiza wa kuwafanya wao kurejea katika Bunge hilo
kwa kuwa mpaka sasa CCM bado hawajaonyesha dalili za kubadilisha msimamo wao wa
muundo wa serikali mbili badala ya maoni yaliyotolewa na wananchi ya serikali
tatu yaliyomo kwenye rasimu ya katiba.
Alisema UKAWA wanawashangaa
viongozi wa dini kwa kuwataka warejee katika Bunge hilo wakati hawajawahi
kuwaita wakazungumza nao ili kufahamu sababu za msingi zinazowafanya wakatae
kurudi bungeni.
Profesa Lipumba alisema
viongozi wa dini wamekuwa wakikaa na viongozi wa serikali, lakini hakuna hata
siku moja wamewahi kuwaita Ukawa na kuzungumza nao.
Alisema badala yake viongozi
wa dini wamekuwa wakisimama katika majukwaa tofauti kuwataka UKAWA warejee
bungeni bila kufahamu sababu za msingi za wao kukataa kurudi bungeni.
Profesa Lipumba alisema UKAWA
wanaheshimu wito wa viongozi wa dini, lakini ni vema wangekuwa wamezungumza na
pande zote mbili wafahamu sababu zinazowafanya wakatae kurudi bungeni, badala
ya kuishia kuzungumza na upande mmoja na kutoa matamko.
“Sababu ya msingi iliyotutoa
bungeni ni mkakati uliokuwa ukitekelezwa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba
wa CCM kupuuza maoni ya wananchi waliyokusanya na kuratibiwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, ambayo inapendekeza muundo wa shirikisho lenye serikali
tatu,” alisema Profesa Lipumba.
Aliongeza: “CCM wameukana na
badala yake wanataka muundo wa serikali mbili, ambao haujapendekezwa na
wananchi walio wengi."
“Kwa sababu muundo wa
muungano ndiyo moyo wa rasimu ya katiba, hivyo ukiunyonga hautakuwa na Rasimu
ya Katiba inayotokana na maoni ya wananchi.
Ukawa tunatetea maoni ya wananchi
yaheshimiwe na ndiyo njia bora ya kutufanya turidhiane. Bunge Maalumu la Katiba
halina uwezo na kibali cha kuvunja misingi mikuu ya maoni ya wananchi na kazi
ya tume.”
Pia alikumbusha kuwa UKAWA
walikwazwa na lugha za ubaguzi, uchochezi, matusi na kejeli zilizokuwa
zikitolewa na baadhi ya wajumbe wa CCM ndani na nje ya Bunge hilo.
Alisema lugha hizo pia
zilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge),
William Lukuvi, pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Profesa Lipumba alisema
viongozi wa dini ni watu wenye nafasi ya kipekee katika jamii kwa kuwa wamepewa
wajibu wa kuongoza watu hapa duniani, hivyo wanaheshimu miito yao.
Hata hivyo, aliwataka
kutambua kuwa sababu ya wao kutoka bungeni ni kutokana na kuwapo kwa njama za
kuhujumu mchakato wa katiba ikiwa ni pamoja na viongozi wa serikali kuingilia
mchakato huo kwa kutoa kauli za kejeli na uchochezi.
Alisema licha ya viongozi wa
dini kutoa kauli hizo, hawajawahi kuwaomba radhi, badala yake wanaendelea kutoa
kauli hizo na hakuna kiongozi wa dini wa kukemea.
“Tunaamini viongozi wetu wa
kiroho wanao uwezo wa kuangalia pande zote mbili na kutoa miito yenye ukweli,
usawa na haki.
Tunawasihi kabla ya
kututaka kurejea bungeni wangetumia
busara hiyo hiyo kutusikiliza na sisi kama, ambavyo wanasikiliza viongozi wa
CCM. Hatujawasikia wakitoa wito kwa wabunge wa chama hicho wala kumkemea waziri mkuu na Lukuvi,” alisema Profesa
Lipumba.
Alisema leo watakuwa na kikao
na Msajili wa Vyama vya Siasa na kwamba, muafaka wa wao kujerea bungeni au
kutorejea utajulikana, lakini hawategemei kutokea kwa muujiza katika kikao
hicho.
Akijibu maswali ya waandishi
wa habari, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, alisema dalili
inavyoonyesha mpaka sasa hakuna uwezekano wa wao kurudi bungeni kwa kuwa
misimamo ya uchakachuaji wa rasimu haijabadilika.
Naye Mwenyekiti wa Ukawa,
Freeman Mbowe, pia aliunga mkono msimamo huo kwa kusema hawatakuwa tayari
kurudi bungeni kama katika kikao cha leo CCM hawatakubali kujadili rasimu ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mbowe alisema dalili ya
kutokuwa na nia njema ya kufikia maridhiano pia imeonyeshwa na Mwenyekiti wa
Bunge hilo, Samwel Sitta, kwa kutoa matamko akisema hata Ukawa wasiporejea,
Bunge litaendelea.
Alisema kauli hiyo inaonyesha
yeye kama kiongozi wa Bunge hilo ameonyesha udhaifu wa kutokuwa na nia ya
kufikia maridhiano tena kipindi, ambacho mazungumzo kati ya CCM na Ukawa bado yanaendelea.
Ukawa wameendelea kutoa
msimamo huo wakati tayari Bunge hilo likiwa limekwishaitishwa kuendelea na
vikao vyake Agosti 5, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa ya
kuwaita wajumbe iliyotolewa juzi na Ofisi ya Katibu wa Bunge hilo, wajumbe wote
wanatakiwa kuwasili mjini Dodoma, kuanzia keshokutwa kwa ajili ya kuanza
mkutano huo kama ilivyopangwa.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa
Agosti 4, mwaka huu, itakuwa siku maalumu kwa ajili ya mambo ya kiutawala na
kwamba, wajumbe wote wanapaswa kufika ofisi za Bunge, majira ya saa 4:00
asubuhi.
Bunge hilo lililoanza
Februari 18, mwaka huu, lilitumia takriban siku 21 za mwanzo kujadili na
kupitisha kanuni za kuliongoza, ikiwamo kuunda kamati 16, kati ya hizo, 12 za
kujadili sura za Rasimu ya Katiba.
Kamati hizo zilijichimbia
katika kumbi mbalimbali mjini Dodoma na kujadili sura ya kwanza na ya sita,
huku mjadala mzito uliosababisha Bunge kuingia kwenye mvutano mkubwa ni sura ya
sita inayozungumzia muundo wa Muungano.
Kundi la wajumbe wengi,
wakiongozwa na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanatetea muundo wa sasa wa
serikali mbili uendelee kwa maelezo kuwa ndiyo utakaodumisha Muungano.
Kundi la Ukawa linaloundwa na
vyama vya upinzani, vikiwamo Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na baadhi ya vyama
vidogo lilisimamia serikali tatu kwa hoja kwamba, rasimu ilipendekeza serikali
tatu kutokana na maoni ya wananchi.
Aidha, baada ya kamati hizo
kumaliza kazi na kurudi kama Bunge Maalumu, wenyeviti wa kamati hizo
waliwasilisha taarifa ya wengi, huku wengine wakiwasilisha ya wachache.
Hata hivyo, mjadala huo
ulijikita katika kurushiana vijembe, maneno yasiyo na staha, matusi, kudhihaki
waasisi, kumshambulia Jaji Warioba kwamba alichakachua takwimu na kupendekeza
serikali tatu kwa maslahi yake binafsi.
Hata hivyo, wakati mjadala wa
sura hizo ukiwa katikati, kundi la wajumbe wanaounda Ukawa walitoka nje ya
ukumbi Aprili 16, mwaka huu, kususia mchakato huo kwa madai kwamba, CCM
imeliteka Bunge na mjadala huo kutokana na kufuta mapendekezo ya tume ya sura
hizo mbili na kupenyeza rasimu yake.
Hadi Bunge hilo
linaahirishwa, ngwe yake ya kwanza Aprili 25, mwaka huu, wajumbe wa Ukawa
walikuwa nje ya Bunge kwa takriban siku tisa, huku wakianza kuzunguka maeneo
kadhaa ya nchi kuwaeleza wananchi juu ya mwenendo wa Bunge kupitia mikutano ya
hadhara.
Bunge hilo liliahirishwa
kupisha Bunge la Bajeti, Mei, mwaka huu na litaendelea tena Agosti 5, mwaka huu
kwa siku 60 zilizoongezwa na Rais Kikwete.
Habari Na:-Nipashe.
No comments:
Post a Comment