Mabingwa wa Tanzania Bara 2013/2014, Azam FC wamechukua
nafasi ya Yanga SC Kombe la Kagame 2014. |
Baraza la Vyama vya Soka
Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limeiengua Yanga SC katika michuano ya Kombe
la Kagame na nafasi hiyo kupewa Azam FC, zote za Tanzania.
Yanga SC imeenguliwa kwa
sababu moja tu kubwa, kushindwa kuthibitisha kupeleka kikosi cha kwanza pamoja
na kocha Mkuu, Marcio Maximo kwa mujibu wa kanuni za mashindano.
Yanga SC ilitakiwa hadi jana
jioni kuwa imethibitisha na kutuma kikosi, lakini haikufanya hivyo na CECAFA
ikawasiliana na TFF kuwaambia wapeleke timu nyingine iliyo tayari, ndipo zali
likawaangukia Azam FC.
Yanga SC ilitaka kupeleka
kikosi cha vijana kwenye nashindano hayo, jambo ambalo CECAFA waliwakatalia
wakiwaambia hiyo si michuano ya watoto.
Katibu Mkuu wa Baraza la
Vyama Vya Soka Afrika Mashariki na Kati, Nicholas Musonye.
|
Azam FC, mabingwa wa Tanzania
Bara, sasa wanaingia Kundi A katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati,
CECAFA Kagame ya 40 pamoja na wenyeji, Rayon Sport, Coffee ya Ethiopia,
Atlabara ya Sudan Kusini na KMKM ya Zanzibar.
Kundi B lina timu za APR ya
Rwanda, KCC ya Uganda, Flambeau de L’Est ya Burundi, Gor Mahia ya Kenya na
Telecom ya Djibouti wakati Kundi C linaongozwa na mabingwa watetezi, Vital’O ya
Burundi, El Merreikh ya Sudan, Polisi ya Rwanda na Benadir ya Somalia.
Timu 14 zinatarajiwa
kushiriki michuano hiyo kuanzia Agosti 8 hadi 24 mwaka huu- jumla ya mechi 34
zikichezwa katika viwanja vya Amahoro na Nyamirambo, Kigali.
Rais Paul Kagame wa Rwanda
ndiye mlezi wa mashindano haya ambaye hutoa dola za Kimarekani 60,000 kila
mwaka kwa ajili ya zawadi.
Wizara ya Michezo ya Rwanda
na mashirika mengine yatadhamini michuano hiyo, itakayokwenda sambamba na
maazimisho ya miaka 20 ya mauwaji ya kimbau.
Televisheni ya kulipia ya
Supersport ya Afrika Kusini ambao ni maswahiba wa muda mrefu wa CECAFA, ni
miongoni mwa wadhamini pia na wataonyesha mechi zote za michuano hiyo moja kwa
moja.
Kwa kuwa Azam imechukua
nafasi ya Yanga, sasa itacheza mechi ya ufunguzi dhidi ya wenyeji Rayon Sport
Uwanja wa Amahoro Agosti 8, mwaka huu, mchezo ambao utatanguliwan na mechi kati
ya KMKM ya Zanzibar na Atlabara
ya Sudan Kusini.
Azam FC itarudi tena dimbani,
Agosti 10 kumenyana na jirani zao KMKM, kabla ya kucheza na Atlabara Agosti 12
na kukamilisha mechi za kundi lake, kwa kumenyana na Coffee ya Ethiopia Agosti
16.
UKIONA TUKIO LOLOTE LINATOKEA USISITE KUTUTUMIA PICHA KUPITIA WhatsApp:- 0789-925-630.
Habari Na:-Bin Zuber.
No comments:
Post a Comment