FUNUNU :-Tazama tukio la Mwandishi aliyeshambuliwa na Polisi wilayani Muleba wakati Wananchi walipoandamana hadi kituo cha Afya Kaigara kushinikiza mwili wa mtoto aliyefariki uchunguzwe. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Tuesday, June 17, 2014

FUNUNU :-Tazama tukio la Mwandishi aliyeshambuliwa na Polisi wilayani Muleba wakati Wananchi walipoandamana hadi kituo cha Afya Kaigara kushinikiza mwili wa mtoto aliyefariki uchunguzwe.

Wananchi wakiwa wameziba barabara katikati ya mji wa Muleba ,mkoani Kagera na magari kushindwa kuendelea na safari kwa zaidi ya saa 3,Baada ya wananchi hao walioandamana hadi kituo cha afya Kaigara kushinikiza mwili wa mtoto Asila Tresphory uchunguzwe ili kubaini chanzo cha kifo cha mtoto huyo wakidai  kuwa baadhi ya viungo havikuwepo.


Mochwari ya kituo cha Afya Kaigara ikiwa na ulinzi mkali baada ya kuvamiwa na Wananchi waliotaka kushuhudia mwili wa mtoto(16) anaedaiwa kufariki,kisha kutolewa baadhi ya Viungo vyake.

Mwandishi wa habari ,Shaban Ndyamukama alieshambuliwa na Polisi  wakati akifanya shughuli zake katika kituo cha afya cha Kaigara ambapo  wananchi walikuwa wakivunja chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo hicho.
Jeshi la Polisi wilayani Muleba mkoani Kagera  limemshambulia mwandishi wa habari wa gaezti la Mwananchi na Radio Kwizera FM mkoani humo,  wakati akifanya shughuli zake katika kituo cha afya cha Kaigara ambapo  wananchi walikuwa wakivunja chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo hicho.

Askari Polisi waliambatana na mkuu wa wilaya ya Muleba ,Lambris Kipuyo ambapo walikuwa wakipiga mabomu ya machozi kutawanya wananchi na ndipo walimkuta mwandishi huyo , Shaaban Ndyamukama  akipiga picha za matukio  na kumtembezea kipigo kikali wakidai aliingia kufanya kazi bila ruhusa yao.

Mwandishi huyo amejeruhiwa kwa virungu katika mguu wake wa kulia sehemu ya chini ya goti na bega la kushoto ambapo alinyanganywa kamera yake, recorder na simu yake ya mkononi huku wananchi wakipigwa mabomu ya machozi kuwatawanyika  kuoondoka eneo la tukio.

Mwandishi huyo alilazimika kumweleza Mkuu wa wilaya kuwa awaruhusu Polisi kumwachia kwani  hana hatia yoyote katika tukio hilo lakini askari polisi walimburuza hadi kwenye gari la Polisi na kushikiliwa kwa muda  hadi wananchi waliokuwa katika eneo hilo kumtaka DC Kipuyo amwachie mwanahabari huyo.

Papo hapo wananchi waliziba barabara  kushinikiza mwandishi kuondolewa katika gari la polisi ambapo mkuu wa wilaya licha ya kumpa maneno ya pole ..’’ alisema hiyo ni sehemu ya kazi.

Pole kwa hayo ni mewaagiza askari wakupatie vifaa vyako na uendxelee na shughuli zako za kawaida na usalama katika eneo hili utakuwepo na mwili wa marehemu utapelekwa kuzikwa panapohusika”Alisema Kipuyo.

Katika kuhakikisha  anafanya kazi zake kwa usalama alilazimika kwenda katika kituo hicho cha afya Kaigara na kupata matibabu ambapo alikaa mpaka saa 8 mchana na kuruhusiwa  kwenda kupumzika mjini Muleba.

......................Hapa akiwa chini ya Ulinzi wa Jeshi hilo la Polisi........................
Picha juu na chini ni muonekano wa Jeraha na kuvuja damu baada ya kipigo alichokipata Mwandishi wa Habari Shaban Ndyamukama kutoka kwa Polisi waliokuwa wakituliza ghasia hizo.


Shaban Ndyamukama akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kaigara,Muleba.

Jeneza la Mwili wa Marehemu anaedaiwa kukatwa baadhi ya Viuongo vya mwili wake .

Mkuu wa wilaya ya Muleba,mkoani Kagera ,Lembris Kipuyo akiwasihi wananchi kuwa na Uvumilivu na Subira wakati vyombo vya dola vikifanya Uchunguzi ili kubaini ukweli.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Muleba wakishuhudia tukio hilo lililotokea June 15,2014 katika kituo cha Afya Kaigara.

Awali katika tukio hilo wananchi wenye hasira kali  wa  Kata ya Muleba ,Kijiji cha Bukono  wamevunja mlango wa  chumba cha kuhifadhi maiti cha kituo cha afya Kaigara wilayani humo,  mkoani Kagera wakitaka kuchukua maiti ya msichana wa miaka (16 ) aliyepoteza maisha akiwa mkoani Arusha alikokuwa akifanya kazi za ndani.

Msichana huyo aliyetajwa kwa jina la Asera Tresphory, alikuwa akifanya kazi za ndani kwa mama mmoja aliyetambulika kwa jina la Valentina Maxmilian   ambapo alimchukua kutoka kwa wazazi wake Mzee Tresphory  Basheka  na mkewe   Georgina Tresphory.

Wananchi walifikia uamuzi huo  wa kubomoa chumba hicho baada ya kudaiwa kuwa  mwili uliokuwa katika jeneza ulikuwa umenyofolewa baadhi ya viungo vya mwili kama sehemu za siri , mkono na sehemu ya mguu , kuwa imekatwa kwa kile kilichosemwa ni imani za ushirikina.

Inasemekana mara baada ya  kufikishwa mkoani  Arusha binti huyo alianza kufanya kazi  za ndani   na katika kufanya kazi hizo za ndani alipoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha na mwili wake kurudishwa juzi (June 15,2014) kwa wazazi wake.

Afisa Tabibu wa kituo cha afya cha Kaigara, Bi Florence Kayungi amesema baada ya uchunguzi wamekuta viungo vyote vikiwa sawa licha ya michubuko midogo na kuwataka wananchi kutoeleza vitu bila kupata uthibitisho wa Daktari .

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Muleba ,Lembris Kipuyo amewataka wakazi hao kuwa watulivu baada ya ndugu na mashuhuda kubaini ukweli kwa kushuhudia mwili huo na kukabidhiwa kwa ajili ya shughuli za maziko



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad