Maaskofu 32 wa Kanisa Katoliki Tanzania, wametoa waraka maalumu wa Pasaka
(April 20,2014) wakiwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuheshimu maoni ya Watanzania
yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kuweka pembeni itikadi za kisiasa katika
mchakato wa kuandika Katiba Mpya.
Kupitia tamko lao la pamoja walilolitoa jana na kulipa jina la “Ujumbe wa
kichungaji wa Pasaka kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema,” maaskofu hao
walisema hivi sasa kuna makundi yenye nguvu ambayo yameanza kushinikiza
kuingizwa mambo yenye masilahi kwao kwenye Katiba .
“Tunalisihi na kulishauri Bunge Maalumu la
Katiba kuheshimu mawazo yaliyowasilishwa na kutumia busara zilizopendekezwa za
kujenga muundo wa Muungano utakaokidhi mahitaji ya utangamano, mshikamano,
amani, maadili, uhuru na uwajibikaji wa viongozi na raia wa Tanzania,” walisema
katika tamko hilo ambalo, Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi
alithibitisha kuwa umetolewa na kanisa hilo.
Kauli ya viongozi hao ambayo ilisomwa katika makanisa mbalimbali nchini
jana (April 20,2014), imekuja ikiwa zimepita siku sita tangu Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba kutokana na mvutano
unaoendelea juu ya hoja ya muundo wa Serikali.
Tangu kuanza kwa Bunge hilo kumekuwa na mvutano kuhusu muundo wa
Serikali, huku CCM kikiupinga muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na kutaka muundo wa serikali mbili, ambao unapingwa na
upinzani.
“Kazi ya kuandika Katiba ni ngumu na haishangazi kuona migongano ya hoja
kwa makundi kinzani. Mawazo ya wengi yamewasilishwa kisheria na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya kujadiliwa na Bunge Maalumu la Katiba,”
inasomeka sehemu ya tamko hilo ambalo limechapishwa kwa ukamilifu katika
ukurasa wa 6 wa gazeti hili na kuongeza:-
“Sasa, tunashuhudia makundi yenye nguvu yakijaribu kushinikiza kuingizwa
matakwa yake kwenye Katiba kwa njia zozote zile ili kujihakikishia kuendelea
kulinda masilahi yake ya kisiasa.”
Maaskofu hao ambao majina yao yameorodheshwa kwenye waraka huo,
wamewataka wajumbe wa Bunge hilo kuachana na itikadi za kisiasa ili kufikia
mwafaka katika masuala muhimu yatakayowahakikishia raia wa kawaida kushiriki
kwenye fursa za maendeleo kwa manufaa ya wote.
Huku wakitolea mfano umoja, amani na utulivu nchini ambao umekuwa
kimbilio kwa mataifa mengine, walisema hivi sasa kuna dosari kadhaa katika
umoja wa Watanzania.
“Kupungua kwa hisia za kujisikia watu wote ni taifa moja, ni dosari
iliyoanza kukua taratibu na sasa inaonekana kuwa ndiyo ukweli,” walisema.
Walisema kasoro zilizojitokeza katika mambo mbalimbali ndiyo chanzo cha
watu kutaka mabadiliko: “Watu wengi walitaka na wanataka mabadiliko au mageuzi
ya msingi. Kwa msukumo huo ndiyo sababu ya kuingia katika mchakato wa kuandika
Katiba Mpya.”
Walisema Watanzania hawatakiwi kukata tamaa, huku wakiwakata watu wenye
nia njema kushirikiana na kupambana na nguvu za maovu na ubinafsi na
kuachana na itikadi za kisiasa ili kupigania haki za wanyonge.
“Tuandae Katiba ambayo itatupatia misingi imara ya maadili
itakayotuongoza kupigana dhidi ya ubinafsi na ufisadi na kutetea haki za
binadamu kwa wote,” walisema.
Hata hivyo, walisema iwapo utakuwapo muafaka na kukubaliana katika mambo
muhimu kwa maisha ya mshikamano wa kitaifa ambayo katika Rasimu ya Katiba
yameandikwa kwenye sura ya kwanza hadi ya tano, muundo wowote wa serikali
unawezekana.
Walisema ili kufikia lengo la kuwa na Katiba bora ni lazima maoni ya Tume
ya Mabadiliko ya Katiba yaheshimiwe kama ambavyo imetamka Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba.
“Kuwe na nia njema ya kutafuta suluhisho la matatizo mengi ya utendaji
katika dola zilizopo katika Muungano, kutokuwa wabinafsi pamoja na kuchambua
matatizo ya sasa ya Muungano na kuridhia mfumo utakaomaliza matatizo hayo,”
walisema.
Akizungumzia waraka huo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema
ameusikia ukisomwa na Askofu Augustino Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar na
kuelezea kufurahishwa na yaliyomo.
Malasusa aonya.
Kwa upande wake Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),
Askofu Dk Alex Malasusa alisema wanasiasa wanatakiwa kutambua kuwa Katiba
Mpya si mali yao, bali ya Watanzania wote.
Akizungumza katika ibada ya Pasaka katika Kanisa la Azania Front jana
Malasusa ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, alisema:
“Katiba Mpya itapatikana kama watu wakiheshimiana, kuridhiana na kuaminiana.
Waliapa kufanya kazi bila upendeleo na hilo ni lazima walizingatie.”
Alisema kazi ya kuandika Katiba ni ngumu na kwamba licha ya misuguano ya
wajumbe wa Bunge hilo bado wanatakiwa kuweka tofauti zao za kisiasa pembeni na
kufikiria mustakabali wa taifa.
“Hatupendi kuona kundi lililoshindwa na lililoshinda. Tunachotaka kukiona
ni Katiba itakayowaweka Watanzania pamoja,” alisema.
Ibada hiyo iliyofanyika kitaifa katika kanisa hilo ilihudhuriwa na
aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania
(IGP), Ernest Mangu.
Habari Na:-Mwananchi.
No comments:
Post a Comment