TASWIRA.Waziri Mkuu Mizengo Pinda Alipotembelea na Kuwapa Pole Wakulima Eneo la Maafa Mauaji Ya Wakulima Kiteto. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Saturday, January 18, 2014

TASWIRA.Waziri Mkuu Mizengo Pinda Alipotembelea na Kuwapa Pole Wakulima Eneo la Maafa Mauaji Ya Wakulima Kiteto.

Eneo la Mtanzania  wilayani Kiteto  ambalo ni moja kati ya maeneo ya  makazi  yaliyovamiwa na watu wanaodaiwa kuwa wafugaji  ambapo watu watatu waliuawa na nyumba kuchomwa moto.  Waziri Mkuu, Mizengo  Pinda alitembelea eneo hilo Januari  16, 2014.


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na wanakijiji wa  Mtanzania Januari 16, 2013 wakati alipokwenda kuwapa pole  kufuatia uvamizi waliofanyiwa  na watu wanaosadikiwa kuwa wafugaji ambao waliua watu watatu  na kuchoma nyumba . Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Erasto Mbwilo.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na viongozi wa wilaya ya Kiteto baada ya kuwasili wilayani humo  Januari 16, 2014  na Alikwenda Kiteto kuwapa pole wakulima  ambao walishambuliwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafugaji ambao waliua na  kuchoma moto nyumba.


Baadhi ya wananchi wa Kiteto  wakimsikiliza  Waziri Mkuu , Mizengo Pinda wakati alipowahutubia  Januari 16, 2014 katika mji wa Kibaya alipokwenda kuwapa pole wakulima wa wilaya hiyo  ambao walishambuliwa, kuuwawa na nyumba zao kuchomwa moto na  watu wanaosadikiwa kuwa  ni wafugaji.

Baadhi ya wananchi wa Kiteto  wakimsikiliza  Waziri Mkuu , Mizengo Pinda wakati alipowahutubia  Januari 16, 2014 katika mji wa Kibaya alipokwenda kuwapa pole wakulima wa wilaya hiyo  ambao walishambuliwa, kuuwawa na nyumba zao kuchomwa moto na  watu wanaosadikiwa kuwa  ni wafugaji.Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameagiza wote waliovamia eneo la Hifadhi ya Jamii ya Emborey ya Murtangos, kuondoka ili kuheshimu uamuzi wa mahakama ya rufani na akaagiza waliohusika na mauaji ya watu 15 kusakwa.

Waziri Mkuu pia, ameagiza vijiji saba vinavyounda hifadhi hiyo, kuunda kamati za kutafuta maridhiano, ambazo zitashirikisha wakulima, wafugaji na wazee wa jadi ili kuhakikisha hakutokei mapigano tena.

Tamko hilo la Pinda, limekuja siku chache, baada ya kauli ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye amekuwa akiwatetea wakulima waliovamia hifadhi hiyo, kushauri kuchukuliwa hatua, Mkuu wa Wilaya hiyo, Martha Umbulla na watendaji wengine kwa kushindwa kudhibiti mapigano.

Akizungumza katika kikao cha ndani na viongozi wa Serikali wa Mkoa wa Manyara na Dodoma, Pinda alisema, haiwezekani watu kuvamia ardhi kama haina mwenyewe.

“Nimepita kwenye soko la mahindi Kibaigwa karibu wote wanaeleza kulima Kiteto, sasa hakuna ambaye anazuia watu kutoka eneo moja kwenda lingine kulima lakini lazima sheria zifuatwe,”alisema Pinda.

Pinda alisema hakuna ardhi ambayo haina mwenyewe na kimsingi mwenyewe mkubwa ni rais na kutoka kwake ndipo kuna ardhi ya vijiji, hifadhi, misitu ama ardhi ya jumla.

Hata hivyo, wakazi wa Kiteto walionekana kupandwa na munkari na kumweleza Pinda, kwamba viongozi wa wilaya na mkoa hawawezi kuwasaka na kuwakamata wauaji.

Pinda, alijibu kelele hizo na kusema kuwa, wataangalia jinsi ya kuboresha utaratibu huo na kwamba iwapo wataona kuna haja ya kufanya hivyo, kuna majeshi mengine nchini ambayo yanaweza kuifanya kazi hiyo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Erasto Mbwilo, alisema mauaji yaliyotokea hivi karibuni yalitokana na wakulima kutoridhika na kauli yake aliyoitoa katika mkutano wa Januari 9, mwaka huu ya kuwataka kuondoka katika hifadhi hiyo kama utekelezaji wa hukumu ya Mahakama ya Rufani.

Alisema baadhi ya wakulima waliopata nafasi ya kuuliza maswali kwenye mkutano huo walisema hawataondoka kwa namna yoyote katika hifadhi hiyo.

Wakati huohuo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwasimamisha kazi, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri, wilayani humo.

Kama hiyo haitoshi, Chadema kimemtaka Pinda kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuwafukuza kazi viongozi hao kwa madai ya kushindwa kutatua mgogoro wa wakulima na wafugaji ambao umedumu kwa miaka mingi.

Habari Na:-Mwananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad