Gazeti la
News of Rwanda ambalo linatajwa kuwa mshirika mkubwa wa Serikali ya nchi hiyo,
katika toleo lake la Jumapili iliyopita, liliandika kuwa Rais Kikwete amekutana
na waanzilishi wa chama cha upinzani nchini humo cha Rwanda National Congress
(RNC) na makamanda waandamizi wa waasi wa FDLR.
Habari
iliyoandikwa na gazeti hilo, imebainisha kuwa kikao hicho cha Rais Kikwete na
watu hao kilifanyika kwenye makazi binafsi ya Rais Kikwete.
Gazeti hilo
lilidai kuwa limepata taarifa hizo kutoka kwenye vyanzo vyake vya habari
vilivyopo nchini Tanzania, ambapo viliwaeleza kuwa ujumbe huo uliwasili, jijini
Dar es Salaam Alhamisi ya wiki iliyopita.
Wameandika
kuwa viongozi wa RNC waliokutana na Rais Kikwete ni Mratibu wa chama hicho, Dk.
Theogene Rudasingwa na mshauri wake, Condo Gervais.
Katika kikao
hicho, News of Rwanda lilidai kuwa kundi la waasi wa FDLR, liliwakilishwa na
Katibu Mtendaji wake, Luteni Kanali Wilson Irategeka na Kanali Hamadi ambaye ni
kamanda wa operesheni.
Luteni
Kanali Irategeka kwa sasa anatajwa kuwa ndiye nembo ya waasi wa Rwanda wa kundi
la FDLR na mara kwa mara amekuwa akionekana kwenye mahojiano na vyombo vya
habari.
News of
Rwanda liliendelea kuandika kuwa, majina hayo anayotumia Luteni Kanali
Irategeka si yake na kwamba jina lake kamili ni Ndagijimana.
Viongozi hao
wa FDLR wote wanaishi Washington, nchini Marekani na kwamba wanasafiri kwa
kutumia hati za kusafiria za Tanzania.
Hata hivyo,
News of Rwanda wameshindwa kuthibitisha madai yao ya pasi za kusafiria za waasi
hao kama zimetolewa na Serikali ya Tanzania, au zilipatikana kwa mlango wa
nyuma.
Aidha gazeti
hili lilikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa Januari 19, mwaka huu, Waziri Mkuu
wa zamani wa nchi hiyo, Faustin Twagiramungu alikuwa Tanzania kwa shughuli kama
iliyofanywa na waasi wa FDLR.
Walidai kuwa
hata hivyo aliondoka Tanzania Alhamisi ya wiki iliyopita, kuelekea Lyon, nchini
Ufaransa ambako alikuwa aongoze kikao cha kundi lake la kisiasa la RDI na
Rwanda RWIZA.
Limedai,
Twagiramungu aliondoka kabla ya timu ya RNC haijawasili Dar es Salaam, ingawa
Twagiramungu pia alipaswa kuwa pamoja na RNC na FDLR.
News of
Rwanda halikuweza kubainisha kilichopelekea Twagiramungu kuamua kukaa mbali na
wenzake hao, ingawa walidai kwamba Waziri Mkuu huyo wa zamani hataki kuingia
tena katika ndoa ya kisiasa na kundi linalohusisha waanzilishi wanne wa RNC.
Twagiramungu
ndiye Waziri Mkuu wa kwanza kushika wadhifa huo mara baada ya kumalizika kwa
mauaji ya kimbari, ambapo alishika wadhifa huo kwa kipindi cha mwaka mmoja na
baadaye kujiuzulu.
Limebainisha
kuwa, Twagiramungu amekuwa na uhusiano mbovu na Dk. Rudasingwa na Kayumba
Nyamwasa kutokana na kuwa sababu ya yeye kushindwa kutekeleza majukumu yake na
kuamua kuachia ngazi.
Wawili hao
wamedaiwa kuwa walikuwa maofisa waandamizi katika nyadhifa kubwa kisiasa na
kijeshi nchini Rwanda.
News of
Rwanda limebainisha kuwa, Twagiramungu na makundi mengine ya waasi ya Rwanda,
yameapa kutoingia katika ushirika wa kisiasa na watu waliokuwa karibu na
Serikali, baada ya kutofautiana na utawala wa Rais Kagame.
Kwa mujibu
wa vyanzo vya habari, si mara ya kwanza kwa wawakilishi wa RNC wanaomwakilisha
Kayumba Nyamwasa, kukutana na waasi wa FDLR.
Gazeti hili
limezidisha chokochoko kwa kudai kuwa Desemba 20, 2013, Luteni Kanali Wilson
Irategeka na Kanali Hamadi walisafiri wakitumia hati ya kusafiria za Tanzania
kwenda Msumbiji kwa mazungumzo na wajumbe wa RNC, na kwamba Tanzania imekuwa
ikitoa hifadhi kwa waasi wa FDLR.
Katikati ya
mwaka jana, Naibu Kamanda wa FDLR, Jenerali Stanislas Nzeyimana, maarufu kama Izabayo
Bigaruka, alitangazwa kuwa yupo Tanzania. Lakini wiki kadhaa baadaye, taarifa
ziliibuka kuwa ametoweka na kuzua maswali ya sababu za uwepo wake Tanzania.
Katika
kuhitimisha chokochoko zao, News of Rwanda liliandika kuwa nchini Tanzania,
upinzani haufurahishwi na mwelekeo wa Rais Jakaya Kikwete kuwabeba FDLR, na
kwamba Agosti mwaka jana, CHADEMA, ambacho ni chama kikuu cha upinzani
Tanzania, kilimtuhumu Rais Kikwete kwa kutokuwa tayari kukutana na wapinzani
nyumbani na kuingilia mambo ya ndani ya Rwanda.
“Hakuna
dhati yoyote ndani ya taarifa ya Rais Kikwete kuwa Rwanda inapaswa kuzungumza
na kundi la wanamgambo wa FDLR, ambalo limekuwapo katika misitu ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo tangu 1994,” walimnukuu Dk. Willbrod Slaa, ambaye ni
Katibu Mkuu wa CHADEMA
Katika
kuhalalisha kile walichokiandika, News of Rwanda liliendelea kumnukuu Dk. Slaa
kuwa: “Iweje Rais Kikwete hayuko tayari kujadiliana na upinzani nyumbani na
kwamba, Rais Kikwete hajachukua hatua zozote kuhusu wauaji wa mwandishi, Daudi
Mwangosi, na kwamba alimshauri (Kikwete) kuchukua hatua za kumwajibisha Kamanda
wa Polisi Mkoa Iringa, Michael Kamuhanda badala yake alimpandisha cheo,”
walihitimisha nukuu yao.
News of
Rwanda lilibainisha kuwa, Dk. Slaa alitoa kauli hiyo katika mkutano wa vijana
wa CHADEMA, kuhusu masuala ya ajira na ukosefu wa ajira mjini Dar es Salaam.
Source:Mtanzania.






No comments:
Post a Comment