![]() |
|
Mkuu wa
Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe akifungua Kikao cha Kamati ya
Ushauri Mkoa (RCC) Januari 16,2014 katika
ukumbi wa ofisi za Mkuu wa Mkoa Kagera.
|
“Kagera Amani na Maendeleo, Amani na
Maendeleo Kagera”
Kwanza kabisa nachukua fursa hii
kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na asili ya mema yote kwa kutulinda
mwaka 2013 na kutuwezesha kuingia mwaka mpya wa 2014 tukiwa wazima.
Sambamba na hilo namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuhudhuria kikao cha
leo ili tuweze kujadili mambo kadhaa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa mkoa
wetu. Aidha, nachukua fursa hii kuwakaribisha kwenye kikao cha Kamati ya
Ushauri ya Mkoa kinachofanyika leo hii.
Ndugu Wajumbe, kikao cha leo ni cha kwanza katika mwaka wa fedha wa
2013/2014, cha muhimu sana na cha kihistoria katika mkoa wetu.
Aidha,
katika kikao hiki pamoja na agenda zingine tutapokea na kujadili taarifa
utekelezaji wa mfumo mpya wa ufuatiliaji na usimamizi miradi ya maendeleo wenye
kuleta Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now – BRN), taarifa ya Programu ya
usambazaji umeme vijijini na hali ya umeme mkoani Kagera, taarifa ya hali ya
ukuaji wa uchumi katika Kanda ya Ziwa Viktoria, taarifa kuhusu mchango wa
taasisi za kifedha katika maendeleo na ustawi wa mkoa na Mapendekezo ya
kuongeza vijiji na Vitongoji kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka
2014.
Aidha, tutapokea taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Matumizi ya
Kawaida na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka wa fedha tunaoendelea nao wa 2012/2013,
2013/2014 (Julai hadi Septemba) na Mapendekezo ya bajeti na mpango wa fedha kwa
mwaka wa fedha 2014/2015.
Ndugu Wajumbe, tofauti na ilivyozoeleka huko nyuma mwaka huu Serikali
imeamua kubadilisha mzunguko wa kuandaa, kujadili, kupitisha na kutekeleza
Bajeti ya Serikali.
Jambo hili linatugusa moja kwa moja na hivi leo kikao
chetu kitapokea, kujadili na kupitisha Bajeti na Mpango wa Maendeleo wa Mkoa
wetu wa mwaka wa fedha 2014/2015.
Aidha, nichukue nafasi hii kuwaomba
Waheshimiwa Wabunge wetu, kuitetea kwa nguvu zenu zote Bajeti ya Mkoa wetu
katika Bunge la Bajeti linalotarajia kuanza mapema mwezi Aprili, 2014.
MFUUMO MPYA WA UFUATILIAJI NA
USIMAMIZI WA MIRADI – MATOKEO MAKUBWA SASA
Ndugu Wajumbe, Mfumo wa tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results
Now) ni mfumo mpya wa ufuatiliaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo ambao
umeanzishwa na serikali ili iweze kuleta matokeo ya haraka ya kijamii na
kiuchumi kwa wananchi wetu.
Ndugu Wajumbe, napenda kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu mfumo huu wa Matokeo
Makubwa Sasa kutokana na mkanganyiko wa kiuelewa juu ya dhana na malengo yake
kwani baadhi ya watu wanautafsiri kuwa ni mpango huku wengine wakiutafsiri kuwa
ni programu.
Napenda ieleweke wazi kuwa serikali inao mpango wa miaka mitano
mmoja wa 2011/2012 hadi 2015/2016. Hivyo, katika kuhakikisha kwamba malengo ya
mpango huu yanafikiwa kwa wakati seriakali imeanzisha mfumo wa Matokeo Makubwa
Sasa.
Ndugu Wajumbe, kwa kuanzia serikali inatekeleza mfumo wa Matokeo Makubwa
Sasa katika sekta za Kiwizara sita (6) ambazo ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Wizara ya Maji, Wizara ya
Uchukuzi, Wizara ya Nishati na Wizara ya Fedha.
Katika Wizara ya Elimu na
Mafunzo serikali imelenga kuongeza ubora wa elimu kwa kushughulikia changamoto
zinazohusiana na masuala yanayohusu walimu, vifaa vya kufundishia na
kujifunzia, usimamizi wa mfumo wa elimu, tathmini ya ubora wa elimu na masuala
mtambuka.
Aidha, kwenye Wizara ya Kilimo
Chakula na Ushirika katika mkoa wa Kagera unalenga kuendeleza kilimo cha
kibiashara kwa zao la miwa katika shamba la Kitengule lenye ukubwa wa hekta
16,500 liliko wilaya ya Karagwe.
Katika mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa mkoa wetu
unalenga kuongeza wa uzalishaji wa sukari tani 50,564 kwa kipindi cha 2013/2014
– 2015/2016 kwa kushirikisha Kiwanda cha Sukari cha Kagera.
Ndugu Wajumbe, chini ya mfumo wa
Matokeo Makubwa Sasa serikali imelenga kuongeza upatikanaji wa maji kwa
wananchi wetu.
Kama inavyofahamika ni kwamba hali ya sasa ya upatikanaji wa
maji kwenye maeneo ya vijiji ni asilimia 55.3, upatikanaji wa maji katika
Manispaa ni asilimia 79 na kwenye makao makuu ya wilaya upatikanaji wa maji ni
asilimia 69.
Napenda kutoa wito kwa viongozi na watendaji mbalimbali wa wilaya
kusimamia kikamilifu miradi ya maji inayoendelea kujengwa ili ikamilike na
kutoa huduma kwa wananchi wetu. Vivyo, hivyo usimamizi ufanyike katika sekta za
uchukuzi, nishati na Wizara ya Fedha ili halmashauri ziweze kuongeza mapato
yake ya ndani.
USAFI WA MAZINGIRA.
Ndugu Wajumbe, kutokana na ufanisi katika kuyatunza mazingira yetu na
kuyaweka katika hali ya usafi, naendelea kuwapongeza viongozi na wananchi wote
tunaoshikamana pamoja katika kuuweka Mkoa wetu katika hali ya usafi.
Nichukue nafasi hii pia kuwapongeza viongozi na Watendaji wa Manispaa ya Bukoba
kwa kutunza mji wetu na kuufanya kuwa mshindi wa tatu (3) katika usafi wa miji
ya Manispaa Kitaifa, hii pia ni fahari kwetu wana Kagera.
Aidha,
niendelee kusisitiza kwa viongozi na Watendaji wa Halmashauri zetu zote kupanda
miti kwa wingi ili kukamilisha lengo la Mkoa wetu la kupanda miti 13,479,000
kwa mwaka 2013/2014 idadi ambayo ni ndogo kama tutaamua kwa dhati kufanya kazi
hiyo muhimu.
Ni matarajio yangu kuwa mnafahamu wazi suala la usafi wa
mazingira kuwa ni pamoja na kuhakikisha takataka zinakusanywa na kuwekwa mahali
panapostahili ili zichomwe au zifukiwe, utunzaji wa vyanzo vya maji,
kuhakikisha kila kaya ina choo na siyo bora choo bali choo bora na kuyaweka
majengo yetu katika hali ya kupendeza kwa kuyapaka rangi.
Ni imani yangu
kuwa maelekezo haya yatatiliwa mkazo na miti itaendelea kupandwa kando kando ya
barabara zote za Mkoa huu wa Kagera. Haya ni maagizo ya Mheshimiwa Makamu
wa Rais ambayo hatuwezi kuyakiuka. Mvua zinazoendelea kunyesha zitumike vizuri
ili kuhakikisha malengo ya upandaji miti yanafikiwa.
HALI YA CHAKULA MKOANI KAGERA.
Ndugu wajumbe, Mkoa wetu kwa mwaka wa 2013/2014 ulilenga kulima hekta
721,597 za mazao mbalimbali ya chakula zilizotarajia kuzalisha jumla ya tani
3,199,334 zikiwa nafaka tani 337,562; kunde tani 148,799; ndizi tani 1,506,020
na mazao ya mizizi tani 1,231,611.
Wakati huo huo eneo lililolengwa
kulimwa mazao ya biashara ni hekta 74,120 kwa lengo la kuvuna jumla ya tani
68,450 zikiwa kahawa za maganda tani 58,030; majani mabichi ya chai tani 7,845;
pamba mbegu tani 1,575 na tumbaku tani 1,000.
Pamoja na kwamba mwaka huu
mtawanyiko wa mvua kwa kipindi cha mvua za vuli haukuwa mzuri sana kwa maeneo
kadhaa hata hivyo hali halisi kwa mavuno mashambani inaridhisha na tathmini inaonesha
kuwa mkoa mzima hadi hivi sasa tuna ziada ya chakula.
Kwa pamoja tuzidi
kujishughulisha katika kilimo cha kisasa na chenye tija kwa kufuata kanuni za
kilimo.
Aidha, hali ya chakula kwa mkoa ni nzuri, hata hivyo nichukue
nafasi hii kuwataka wajumbe waalikwa na wadau wengine kwenye mkoa wetu
kuendelea kuhamasisha wananchi ili wazitumie mvua hizi za masika kwa kulima
mazao yetu ya kawaida bila kuacha yale yanayokomaa kwa muda mfupi ili kuepuka
kupatwa na njaa na ituwezeshe kuzalisha chakula cha ziada na tusaidie maeneo
ambayo yatakuwa na upungufu wa chakula.
Sehemu mbalimbali za nchi kuna taarifa
za njaa. Kwa bahati nzuri mkoa wetu hauko katika orodha ya mikoa ambayo
iko katika hali hatarishi ya njaa.
Ndugu wajumbe, pamoja na mkoa kutokuwa na tatizo la upungufu wa chakula
bado inatakiwa tuongeze mbinu za uzalishaji ili tupate ziada itakayowezesha
wakulima kuuza mazao na kujipatia kipato zaidi.
Hivyo matumizi ya
pembejeo za kilimo na hasa mbolea na mbegu bora ni muhimu kwa watu wetu.
Matumizi ya zana za kilimo yatumike mfano matrekta n.k. tuachane na jembe la
mkono. Aidha, kwa mwaka 2012/2013 wakulima 25,000 walinufaika na mbolea
za ruzuku katika Wilaya za Biharamulo, Missenyi, Karagwe na Ngara.
Idadi
hii imepungua ikilinganishwa na wakulima 53,192 kwa mwaka 2011/2012. Hii
ni kwa sababu Wilaya ya Chato iliyokuwa kwenye mpango huo imehamishiwa Mkoa wa
Geita na wakulima kadhaa wamemaliza miaka ya mkataba wao wa miaka mitatu (3) ya
kupata mbolea za ruzuku.
Ndugu Wajumbe, imani yangu ni kwamba kwenye mkoa wetu pia tuna mifugo
inayoweza kutupatia samadi ya kutosha kama wananchi wetu wataelimishwa,
kutahamasishwa na kushirikishwa. Ninasisitiza jamii zetu zihamasishwe
kutumia samadi itokanayo na mifugo yetu, pasipo kusubiri mbolea za ruzuku tu
ili zijiongezee uzalishaji.
HALI YA ELIMU.
Ndugu wajumbe, kwa mwaka 2013 Mkoa wa Kagera ulisajili wanafunzi 43,154
kufanya mtihani darasa la saba. (Wav.20,257 na Was. 22,897) hawa ni 75% ya
watoto 57,779 (Wav. 28,405 na Was. 29,374) walioandikishwa darasa la kwanza 2007,
asilimia 25 kutomaliza elimu ya msingi si swala la kujivunia bali tunatakiwa
tulilaani kwa pamoja na tupambane na sababu zote zinazofanya watoto wetu
kutomaliza darasa la saba ambazo ni pamoja na utoro 418, mimba 16, vifo 13 n.k.
Kati ya wanafunzi waliosajiliwa
kufanya mitihani ya darasa la saba, waliofaulu ni 24,546 (Wav. 11,919 na Was.
12,627) sawa na 58.1% ya wote waliofanya mitihani. Katika mwaka huu
wanafunzi wote waliofaulu mitihani ya darasa la saba wamepata nafasi za
kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza.
Kipekee ninachukua nafasi hii
kuipongeza Halmashauri ya Wilaya Biharamulo kwa kuwa ya kwanza kimkoa ikiwa
imefaulisha kwa asilimia 85.59 na Manispaa ya Bukoba asilimia 80.74 ambazo
zimechangia mkoa wetu kuwa nafasi ya 7 Kitaifa.
Vile vile nichukuwe nafasi hii
kuziagiza Halmashauri za wilaya za Karagwe/Kyerwa (50.99%), Muleba (52.87%),
Bukoba (53.41%) na Missenyi (58.59%) kuongeza bidii zaidi ili mwaka unaofuta
ziweze kufaulisha kwa kiwango cha juu.
Aidha, nichukuwe fursa hii kuwapongeza
ninyi viongozi na watendaji mbalimbali kwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa
miundombinu ya madarasa inayotosheleza mahitaji.
Kipekee niwashukuru wananchi
wote wa mkoa wa Kagera kwa kutoa michango yao ya nguvu na fedha ambayo
imechangia kukamilika kwa miradi mbalimbali ya maendeleo hususan vyumba vya
madarasa.
Aidha, napenda kuwaagiza viongozi na watendaji wote wa serikali
kuhakikisha mnasimamia na kushauri juu ya ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu
ya maabara kwa kila shule ya sekondari ili kuongeza wigo wa watoto watakaosoma
masomo ya sayansi.
UTEKELEZAJI WA OPERESHENI KIMBUNGA.
Ndugu wajumbe, Mkoa wetu ni miungoni mwa mikoa ya pembezoni ambako zoezi
la kuwaondoa wahamiaji haramu kutoka nchi za jirani linatekelezwa.
Operesheni
hii ilianza kufanyika kuanzia mwezi Oktoba, 2013 kwa kushirikisha wilaya na
idara za serikali, hivi sasa operesheni inatekelezeka kwenye awamu ya nne
ambapo katika awamu hii wananchi wanatoa taarifa kuhusu hali ya uhamiaji.
Aidha, napenda kuchukua fursa hii
kuipongeza serikali kwa kuona umuhimu wa kuwaondoa wahamiaji haramu katika
ardhi ya mkoa Kagera ambao pamoja na athari zingine walihatarisha usalama wa
wananchi wetu, uharibifu wa mazingira na kupokonya ardhi bila kufuata taratibu.
Kipekee napongeza viongozi na wananchi kwa kutoa ushirikiano wa dhati wakati
wote wa zoezi hili.
Napenda kuwaagiza viongozi na watendaji wote wa wilaya
kuendelea kushirikiana kwa kuwafichua wahamiaji na kuwachukulia hatua pale
wanapoingia, tusisubiri wajenge himaya katika maeneo yetu.
Aidha, tuendelee
kutoa elimu kwa wananchi wetu ili wafahamu athari za uhamiaji hivyo washiriki
kikamilifu katika kutoa taarifa zinazohusu wahamiaji haramu.
Ndugu wajumbe, kama mnavyofahamu katika mwaka wa fedha wa 2013/14
mkoa wetu uliidhinishiwa kiasi cha fedha cha shilingi 174,925,757,000 kwa
ajili ya matumizi ya kawaida ya mishahara na matumizi mengineyo na miradi
ya maendeleo.
Na hadi kufikia mwishoni mwa
Oktoba, 2013 tulikwishapokea kutoka Hazina shilingi 49,924,168,457 sawa
na asilimia 28.54. Katika kikao hiki tutapokea taarifa ya utekelezaji ya
matumizi ya fedha hizo.
Katika utekelezaji wa bajeti ya
2013/2014 Mkoa ulijiwekea malengo ya kukusanya mapato ya ndani kwa Halmashauri
zetu ambayo ni shilingi 13,737,670,000/=.
Hadi
Desemba, 2013 Halmashauri zilikuwa zimekusanya shilingi 4,541,794,736.5 sawa na
asilimia 34.73, kwa mchanganuo ufuatao:-
NA.
|
HALMASHAURI
|
MALENGO KWA MWAKA
|
MAKUSANYO HADI DESEMBA, 2013
|
ASILIMIA
|
1
|
Biharamulo
|
1,581,375,000
|
699,836,231.68
|
46.54
|
2
|
Bukoba
|
1,403,896,000
|
509,000,772.68
|
36.3
|
3
|
Manispaa
|
2,576,167,800
|
590,566,367.77
|
32.4
|
4
|
Karagwe
|
1,675,359,600
|
746,084,055.12
|
54
|
5
|
Kyerwa
|
1,798,538,040
|
550,219,015.00
|
31.18
|
6
|
Missenyi
|
1,090,000,000
|
365,093,020.60
|
34.12
|
7
|
Muleba
|
3,298,495,283
|
783,220,119.24
|
24.4
|
8
|
Ngara
|
1,577,130,001
|
297,775,154.41
|
18.9
|
JUMLA
|
13,737,670,000
|
4,541,794,736.5
|
34.73
|
Napenda kupongeze uongozi wa Wilaya
za Karagwe kwa kuvuka lengo la asilimia hamsini (50%).
Wilaya hii
inaonesha kuwa inaweza kufikia malengo waliyojiwekea, kwa Wilaya zilizobakia
hali ya makusanyo sio ya kuridhisha ni vema kikao hiki kikajiridhisha ni
kwanini Halmashauri hizo makusanyo ya ndani bado yako chini.
BAJETI NA MPANGO WA MAENDELEO WA
2014/2015.
Ndugu Wajumbe, Kikao chetu hiki kitapata nafasi ya kujadili na kupitisha
Bajeti na Mpango wa maendeleo wa Mkoa kwa mwaka ujao wa fedha wa 2014/2015.
Mkoa unakusudia kuomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi 252,349,563,967 kwa
ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo kwa Halmashauri zetu na
Sektretarieti ya Mkoa kipindi cha mwaka wa fedha 2014/15.
Ni matumaini yangu kwamba bajeti na
mipango ya maendeleo kwa kila Halmashauri imejadiliwa na kupitishwa na vikao
husika katika ngazi ya Wilaya.
Nachukua nafasi hii kuwataka wajumbe
kupitia kwa makini Bajeti ya matumizi ya kawaida na maendeleo ya mkoa kwa ajili
ya ustawi wa maisha ya wananchi wetu na maendeleo ya mkoa wetu.
Natumaini kuwa Waheshimiwa Wabunge
wetu wataendelea kutetea bajeti ya Mkoa wetu katika Kamati za Bunge na kwenye
kikao cha Bunge la Bajeti kilichopangwa kufanyika mwezi Machi, 2014.
Ndugu wajumbe, na waalikwa Mabibi na mabwana baada ya maelezo hayo
natamka rasmi kwamba kikao chetu kimefunguliwa na nawatakia majadiliano mema.
“KAGERA..... AMANI NA MAENDELEO,
AMANI NA MAENDELEO........KAGERA”






No comments:
Post a Comment