Katika tukio
linaloweza kuitwa kama ndoa ya karne, mzee mmoja mwenye umri wa miaka 91,
Nkwabi Ngobola Kapimbi, wiki iliyopita alifunga pingu za maisha na mkewe Maria
Mkiwa (78) mbele ya mchungaji Thobias Shilole wa Kanisa la Maombezi huko Kibaha
mkoani Pwani.
Tukio hilo
lililovuta hisia za watu wengi, lilitokea baada ya wanandoa hao kutimiza miaka
55 tokea walipoanza kuishi pamoja, katika uhusiano ambao walibahatika kupata
watoto saba, wajukuu 78 na vitukuu 24.
|
Mzee Nkwabi
Ngobola Kapimbi (91) baada
ya kufunga
pingu za maisha
na mkewe
Maria Mkiwa (78).
|
Akiwa
amevalia suti huku mkewe akiwa ndani ya vitenge, mzee Nkwambi alisema
amejisikia furaha sana kufanya kitendo hicho kwani ni jambo ambalo kwake na la
tatu kwa umuhimu, mengine yakiwa ni kuzaliwa na kifo.
“Nimefurahi
kufunga ndoa, tukio hili ni muhimu kwangu, umri wangu ni miaka 91, nimezaliwa
mwaka mmoja na Nyerere, mke wangu ana miaka 78, tulionana kwa mara ya kwanza
mwaka 1958, tukio hili limefungua ukurasa mpya wa maisha yangu, najua Mungu
yuko pamoja nasi, nina wajukuu 78 na Vitukuu 24.
“Watu wengi
wanauliza tulikuwa wapi siku zote hizi, ni kwamba nilikuwa simuamini sana mke
wangu, tulikuwa tukikorofishana lakini bado tuliweza kudumu. Mungu ni mwema
sana,” alisema.
Alisema
hajali kama kuna watu watakuwa wakizungumza wanalojua kuhusu ndoa yao, lakini
anachofurahi yeye ni kufunga ndoa na mke wake anayempenda.
“Mara ya
kwanza mke wangu alikuwa anasita, lakini nilisema lazima tukafunge ndoa kwenye
kanisa la Mzee wa Upako ( Antony Lusekelo), nampongeza mchungaji Thobias
Shilole kwa kuwa pamoja nasi na kukubali kubariki ndoa yetu, lilikuwa jambo la
furaha kwangu na mke wangu,” alisema Babu Nkwabi.
|
Sherehe
baada ya ndoa ikiendelea.
|
Kwa upande
wake, mkewe Maria alisema awali alikuwa akisita kwa kuona kama itakuwa ni
kituko mbele ya jamii, lakini baada ya majadiliano na mumewe, akaridhia jambo
hilo kwa moyo mmoja.
“Najua
maneno lazima yasemwe lakini mimi nampenda sana mpenzi wangu, tuliwahi kupitia
mambo magumu, milima na mabonde lakini leo tumeamua kuzishinda hila za muovu ya
shetani, si kitu cha kawaida kufunga ndoa kwa umri wetu lakini Mungu ndiyo njia
ya kweli na uzima,” alisema mama huyo.





No comments:
Post a Comment