![]() |
|
Basi la
kampuni ya Mtei lenye T 742 ACU Scania likiwa limeteketezwa kwa moto na
wananchi baada ya kugonga na kusababisha vifo vya watu watatu wa familia moja
mjini Singida jana(Januari 09,2014).
|
![]() |
| Abiria wanasema walipokusanyana wananchi, walitafuta mafuta ya petroli na kumwaga ndani ya basi hilo kisha wakalipua kibiriti. |
Wananchi
wenye hasira, jana walifanya kitendo cha kikatili kwa kulichoma moto basi la
kampuni ya Mtei lililokuwa likisafiri kutoka Singida kwenda Arusha, baada ya
kugonga bobaboda na kuua watatu wa familia moja.
Tukio hilo
lilitokea jana (Januari 09,2014) saa 1:10 asubuhi katika eneo la Ijanuka, nje
kidogo ya mji wa Singida…na Lilitokea kufuatia dereva wa basi la Mtei lenye namba
za usajili T 742 ACU aina ya Scania, Dismas Ludovick, akijaribu kuipita
pikipiki yenye namba za usajili T 368 BXZ ikiwa na abiria watatu na dereva wao.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, alisema baada ya pikipiki hiyo
kugongwa na basi hilo lililokuwa na abiria tisa, watu wawili waliokuwa
wamepakiwa walifariki dunia papo hapo na mwingine mmoja kufia Hospitali ya Mkoa
wa Singida.
Aliwataja
waliofariki dunia kwa jina moja moja kuwa ni Tamili, Kassim na Hamza, wote
watoto wa mmiliki wa pikipiki hiyo, Shabani Bunku, mkazi wa Ijanuka, ambaye
naye yupo mahututi na amelazwa katika hospitali hiyo.
Kwa mujibu
wa baadhi ya wananchi waliofika eneo la tukio, marehemu hao walikuwa wanakwenda
shambani na baba yao.
Kamanda
Kamwela alisema wakati dereva wa basi anajaribu kuipita, pikipiki hiyo, nayo
ilikata kona kuelekea kulia, hali iliyosababisha kukanyagwa na kuburuzwa mita
20 kutoka eneo la tukio.
Mashuhuda wa
tukio hilo, akiwamo Husna Ramadhani, Yassin Ibrahim na Samuel Massawe,
waliokuwa kwenye basi la Mtei, walisema kuwa baada ya pikipiki kugongwa,
wananchi wa eneo hilo waliwasiliana kwa simu na kukusanyika kwa haraka.
Walisema
walipokusanyana, walitafuta mafuta ya petroli na kumwaga ndani ya basi hilo
kisha wakalipua kibiriti.
Mashuhuda
hao walisema kuwa kabla wananchi hao kuchukua hatua hiyo, walivunja kwanza vioo
vyote vya madirisha ya basi hilo.
“Walianza
kukusanyika kidogo kidogo huku wakipigiana simu, walipojaa walianza kuvunja
vioo vyote vya madirisha huku wakidai kwamba mabasi ya Mtei yamezidi sana
kuwakanyaga pamoja na ng’ombe wao, leo acha na yeye wamkomeshe,” alidai mmoja
wa abiria wa basi hilo.
Husna,
abiria aliyekuwa anasafiri kwenda Arusha, alisema alipata hasara katika sakata
hilo kwa kuwa alipoteza begi la nguo lililoteketea kwa moto pamoja na mfuko wa
nyanya alizokuwa anapeleka kama zawadi kwa ndugu zake.
Kamanda
Kamwela aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na ameahidi
kuwasaka wote wakiwamo vinara wa tukio hilo la uchomaji moto basi hilo ili
wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Habari Na:-Nipashe.









No comments:
Post a Comment