14/11/2013 –
Dar es salaam.
Watanzania
wametakiwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara, kupima afya na
kuepuka tabia hatarishi zinazochangia uwezekano wa kupata ugonjwa wa kisukari.
Kauli hiyo
imetolewa jana(Novemba 14,2013) jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt.
Hussein Mwinyi wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu Siku ya Ugonjwa wa
Kisukari Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Novemba 14.
Amesema Tanzania
kama zilivyo nchi nyingine inaadhimisha siku hiyo kwa Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii kwa kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa kisukari Tanzania kutoa elimu
ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga na madhra mbalimbali yatokanayo na ugonjwa
huo.
Amesema
maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani 2013 yataongozwa na kauli mbiu isemayo
"Linda Maisha yajayo dhidi ya Ugonjwa kisukari" inayolenga
kuhamasisha jamii juu ya matatizo mbalimbali yanayotokana na ugonjwa wa
kisukari katika jamii.
Ameeleza
kuwa athari za ugonjwa wa kisukari katika mwili wa binadamu hutokea wakati
sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu
na kuongeza kuwa tafiti zinaonyesha kuwa mwaka 2007 kulikua na wagonjwa milioni
246 duniani huku mwaka 2012 kukiwa na wagonjwa milioni 371 ambapo nusu ya idadi
ya wagonjwa hao walikua hawajaanza kupata matibabu.
Kuhusu
dalili za ugonjwa huo Dkt. Mwinyi amesema kuwa ni rahisi kuzitambua na
huambatana na mgonjwa kuwa na kiu isiyoisha, kukojoa mara kwa mara, kupungua
uzito, kusikia njaa kila wakati na mwili kukosa nguvu na kuongeza kuwa athari
za ugonjwa huo ni kubwa kutokana na ugonjwa huo kuharibu mishipa ya damu na
fahamu, macho, figo, kusababisha upofu, moyo na figo kushindwa kufanya kazi na
miguu kufa nganzi na kuwa na vidonda.
Dkt. Mwinyi
ameeleza kuwa asilimia 80 ya wagonjwa wote duniani wanaishi katika nchi
zinazoendelea ikiwemo Tanzania na kuongeza kuwa utafiti uliofanyika mwaka 2012
nchini Tanzania kwa kuzihusisha wilaya 50 unaonyesha kuwa asilimia 9.1 ya
watanzania wenye umri wa miaka 25 na kuendelea wana ugonjwa wa kisukari.
"Ni jambo
lililo wazi kuwa lazima tubadili tabia hasa tabia hatarishi zinazochangia
ugonjwa wa kisukari zikiwemo unywaji wa pombe kupita kiasi, ulaji usiofaa,
ulaji usiofaa na tabia ya kupuuza kufanya mazoezi", sasa Tanzania katika
nchi 10 za Afrika zinazoongoza kwa kisukari barani Afrika inashika nafasi ya
8" Amesema Dkt. Mwinyi.
Kuhusu
sababu zinazochangia ugonjwa huo Dkt. Mwinyi amesema kuwa ni pamoja na tabia ya
ulaji usiofaa hasa matumizi ya chumvi kwa wingi , mafuta na sukari, uzito
uliozidi, unene uliokithiri, kutofanya mazoezi , uvutaji wa sigara na bidhaa
zitokanazo na tumbaku pamoja, kula vyakula vyenye mafuta mengi hasa yatokanayo
na wanyama, sukari nyingi,kula chakula kupita kiasi, kukoboa nafaka, kutokula
mbogamboga na matunda na unywaji wa pombe kupita kiasi.
Ameeleza
kuwa jamii inapaswa kuepuka mambo yanayochangia chakula kilicholiwa kutotumika
vizuri ikiwemo tabia ya kukaa muda mrefu bila kufanya mazoezi huku akisisitiza
kuwa unywaji wa pombe kupita kiasi huharibu maini na kusababisha utapiamlo kwa
wale wanaoishia kunywa pombe Zaidi bila kula chakula.
" Natoa
ushauri hasa kwa watumishi kuepuka kuketi ofisini, darasani au kuangalia
runinga kwa muda mrefu na hata kutumia lifti kwenda ghorofani badala ya ngazi
na matumizi ya magari katika umbali mfupi unaoweza kufikika kwa kutembea
tu"
Dkt. Mwinyi
ameleza kuwa serikali imejipanga kukabiliana na changamoto mbalimbali
zinazotokana na ugonjwa huo na kusisitiza kuwa utekelezaji wa Sera ya Afya ya
mwaka 2007 unaendelea kwa kuhakikisha kuwa utoaji wa hudunma za magonjwa yasiyo
ya kuambukiza ikiwemo kisukari unafanyika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
ndani na nje ya nchi.
Ameeleza
kuwa serikali kwa kutambua gharama za kutibu ugonjwa wa kisukari kuanzia mwaka
1983 ilitoa msamaha wa matibabu kwa wagonjwa wote wa kisukari kutochangia
gharama za matibabu pia kuhakikisha kuwa dawa muhimu zinapatikana katika
kliniki mbalimbali zilizopo nchini.
Kwa upande
wake Mganga mkuu wa Serikali Dkt. Donan Mmbando amewataka vijana kote nchini
ambao ni kundi kubwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara na
kuepuka maisha ya anasa ambayo huwaweka katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa
wa kisukari.
Amesema
mapambano ya ugonjwa wa kisukari yanahitaji ushiriki wa kila mwananchi hasa kuzingatia
kanuni za Afya na kujenga mazoea ya kufanya mazoezi mara mara.







No comments:
Post a Comment