Mfanyabiashara
maarufu nchini, Rostam Aziz (49), ametajwa kuwa ndiye tajiri namba moja
Tanzania kwa sasa.
Kwa mujibu
wa utafiti uliofanywa na Jarida la Marekani la Forbes na kutoa taarifa yake
juzi, Rostam amekamata nafasi hiyo na ya 27 katika Afrika akiwa na utajiri wa
Dola za Marekani bilioni moja (Sh1.6 trilioni).
Mbunge huyo
wa zamani wa Igunga, ameingia kwa mara ya kwanza katika orodha ya matajiri 50
wa Afrika ya jarida hilo, pamoja na wafanyabiashara wengine wa Tanzania, Reginald
Mengi na Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mohamed Dewji ‘Mo’.
Katika orodha hiyo
pia yumo Said Bakhresa ambaye aliwahi kutajwa siku za nyuma.
Rostam,
ambaye aliachana na siasa mwaka 2011, amempiku Bakhresa, ambaye mwaka jana
Jarida la Ventures Africa la Nigeria lilimtaja kuwa ndiye aliyekuwa tajiri
namba moja wa Tanzania. Bakhressa katika kipindi hicho alikadiriwa kuwa na
utajiri wa Dola 620 milioni (Sh971 bilioni).
Katika
orodha hiyo ya Ventures Africa, Bakhresa alifuatiwa na Rostam, Mengi na
mfanyabiashara mwingine maarufu, Ali Mufuruki.
Mengi
anashika nafasi ya pili kwa Tanzania na ya 34 Afrika akiwa na utajiri wa Dola
550 milioni (Sh861 bilioni).
Forbes
linaonyesha kuwa Bakhresa amefungana na Mo katika nafasi ya tatu ya orodha ya
matajiri wa Tanzania na ya 38 kwa Afrika, wote wakiwa na utajiri wa Dola 500
milioni (Sh783 bilioni).
Rostam,
Mengi na Bakhresa hawakupatikana jana kuzungumzia suala hilo huku Mo akisema
kwamba asingeweza kuzungumzia suala hilo kwa kuwa jana alikuwa katika mapumziko
ya Sikukuu ya Ashura.
Tajiri wa
Nigeria, Aliko Dangote, ambaye anajenga Kiwanda cha Saruji huko Mtwara ndiye
anayeshika nafasi ya kwanza katika orodha ya Afrika, akiwa na utajiri wa Dola20
bilioni (Sh31.7 trilioni), akifuatiwa na familia ya Johanny Rupert ya Afrika Kusini
yenye utajiri wa Dola7 bilioni (Sh10.7 trilioni) na Nick Oppenheimer, pia wa
Afrika Kusini mwenye utajiri wa Dola 6.6 bilioni (Sh10.3 trilioni).
1)Rostam
Aziz.
Jarida la
Forbes limeripoti kuwa utajiri wa Rostam unachangiwa zaidi na biashara ya
mawasiliano ya simu za mkononi, ujenzi na uchimbaji wa madini.
Anamiliki
asilimia 35 ya hisa katika Kampuni ya Simu za mkononi ya Vodacom. Ni kampuni
inayoongoza kwa biashara ya simu za mikononi nchini Tanzania ikiwa na wateja
zaidi ya milioni 9.5.
Pia
anamiliki Kampuni ya Caspian, ambayo inafanya kazi za kuchimba madini katika
migodi inayomilikiwa na Kampuni za BHP Billiton na Barrick Gold.
Pia ana hisa
katika Kampuni ya Hutchison Wampoa inayofanya kazi za kupakua mizigo bandarini
na anamiliki majumba nchini na katika nchi za Mashariki ya Kati.
![]() |
|
Reginald
Mengi.
|
2) Mengi.
Ni
Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP.
Utajiri wake
unatokana na kumiliki vyombo vya habari, kiwanda cha vinywaji baridi na madini.
Mengi
anamiliki magazeti kumi na moja, vituo vitatu vya televisheni na takriban vituo
10 vya redio.
Pia ana
mgodi wa madini ya dhahabu na viwanda vya CocaCola.
Kwa mujibu
jarida hilo, Mengi alizaliwa katika familia maskini na baadaye kusomea uhasibu
huko Uingereza na kufanya kazi huko.
Alijiunga na
Chama cha Wahasibu cha Uingereza kabla ya kurejea Tanzania mwaka 1971 na
kuajiriwa na Kampuni ya Ukaguzi ya Coopers & Lybrand Tanzania (sasa Price
Water House Coopers) hadi mwaka 1989, alipoacha kazi na kujikita zaidi katika
biashara.
3)
Bakhresa
Said Salim
Bakhresa ni mwasisi na Mwenyekiti wa Kampuni ya Bakhresa Group na ana utajiri
wa Dola500 milioni (Sh783 bilioni).
Ni kampuni
kubwa inayoajiri zaidi ya watu 2,000 ikijishughulisha zaidi katika kusaga
nafaka, kusindika matunda, usafiri wa meli na biashara ya mafuta. Pia kwa
kutengeneza pipi na ice cream.
Bakhresa
aliacha shule akiwa na umri wa miaka 14 na kuanza biashara ya kuuza viazi
mbatata. Baada ya hapo alifungua mgahawa na baadaye kuingia katika biashara ya
kusaga nafaka.
4) Mo
Mafanikio
yake yamechangiwa zaidi baada ya kuendeleza mali ya wazazi wake.
Anafanya
biashara ya nyumba, kuuza mazao na viwanda vya mafuta.
Mo alirejea
Tanzania baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Georgetown,
Marekani na kuendeleza biashara ya maduka ambayo yalianzishwa na baba yake.
Alinufaika
baada ya kununua viwanda vilivyobinafsishwa na Serikali.
Alivifanya
viwanda hivyo kutengeneza faida na kuinyanyua Kampuni ya Mohamed Enterprises
(MeTL) kuwa miongoni mwa kampuni zenye mafanikio makubwa Tanzania.
Mo pia
anajihusisha na biashara ya usambazaji bidhaa, viwanda vya nguo na kilimo.
Jarida hilo
lilipiga hesabu za utajiri wa wafanyabiashara hao kwa kuangalia thamani ya
bidhaa zinazouzwa na kampuni zao, mikataba yao na hasa wale walio kwenye sekta
ya mafuta na ukubwa wa kampuni zao.
Chanzo:- Mwananchi.







No comments:
Post a Comment