Tume ya
Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa taratibu za kuusafirisha
mwili wa Mjumbe wake, Dkt. Sengondo Mvungi aliyefariki nchini Afrika Kusini
zimekamilika na mwili wake unatarajia kuwasili nchini siku ya Ijumaa, Novemba
15, 2013.
Baada ya
kuwasili, mwili huo utahifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo iliyopo
jijini Dar es Salaam.
Aidha, siku
ya Jumamosi, Novemba 16, 2013 kutafanyika Ibada ya mazishi katika Kanisa
Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi.
Baada ya misa, marehemu ataagwa katika Viwanja vya Karimjee kuanzia saa 6:30
mchana siku hiyo hiyo ya Jumamosi, Novemba 16, 2013.
Aidha,
Marehemu Dkt. Mvungi anatarajiwa kusafirishwa siku ya Jumapili, Novemba 17,
2013 kwenda Kisangara Juu, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya
mazishi yanayotarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu, Novemba 18, 2013.
Dkt. Mvungi
alifariki jana (Jumanne, Novemba 12, 2013) katika Hospitali ya Millpark jijini
Johannesburg nchini Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya uchunguzi na
matibabu zaidi akitokea Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) aliokuwa amelazwa
baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es
Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili,
Novemba 3, 2013.
Wakati
huohuo, Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakiongozwa na Mwenyekiti wake
Jaji Joseph Warioba leo (Jumatano, Novemba 13, 2013) wameungana na Mheshimiwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kufika
nyumbani kwa marehemu Dkt. Mvungi eneo la Kibamba jijini Dar es Salaam kwa
ajili ya kutoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu Dkt. Mvungi.
Akiwa
nyumbani kwa marehemu, rais Kikwete alipata fursa ya kutoa pole kwa familia ya
marehemu dokta Mvungi na kisha kusaini kitabu cha kumbukumbu na kutoa pole kwa
wafanyakazi wa tume ya katiba akiwemo mwenyekiti wa tume ya katiba jaji mstaafu Joseph Warioba,
waziri mkuu mstaafu Daktari Salim Ahamed Salim,jaji mstaafu Agustino Ramadhani
na viongozi wengine wa serikali na vyama vya siasa.







No comments:
Post a Comment