![]() |
Jeneza lenye
mwili wa Dk Sengondo Mvungi likishushwa kaburini katika maziko yaliyofanyika jana (Novemba 18,2013) kwenye kijiji cha Chanjale Kisangara Juu, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
|
Aliyekuwa
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi alizikwa jana
kijijini kwake, Chanjale, Kisangara Juu katika mazishi ambayo yalihudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
wajumbe wa tume hiyo, vyama vya siasa na wananchi.
Akizungumza
katika mazishi hayo, Askofu Rogath Kimario wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Same
alisema tukio la kushambuliwa lililosababisha kifo chake halikuwa la ujambazi.
Akizungumza
wakati wa ibada ya mazishi iliyofanyika Kanisa la Moyo Mtakatifu Yesu la
Parokia ya Kisangara Juu iliyopo Chanjale, ambayo pia ilihudhuriwa na Askofu
Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu; Askofu wa Jimbo la Mbulu, Beatus
Kinyaiya na Askofu Damiani Ngalu wa Geita wote wa Kanisa Katoliki, Askofu
Kimario alisema waliofanya mauaji hayo ni wauaji wa kimtandao na kuitaka
Serikali kutoa majibu sahihi kuhusiana na tukio hilo badala ya majibu mepesi
yasiyofanyiwa utafiti.
Kauli hiyo
ilionekana kujibu ile ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova kuwa mauaji ya Dk Mvungi ni tukio la ujambazi.
“Eti
waliotenda hilo ni majambazi, nani kasema ni majambazi?... Ni research
(utafiti) ipi ama upelelezi gani umefanyika?… Hawa ni wauaji wa kimtandao, kuna
maswali mengi yasiyo na majibu,” alisema Askofu Kimario na kuongeza:
“Ni kifo cha
fedheha hata kuku hauawi hivyo. Watu wana uchungu, kila mtu ana maswali ambayo hayana
majibu… kwa nini auawe? Kwani alikuwa tajiri hata majambazi watake pesa?”
Askofu
Kimario alisema Watanzania wanamlilia Dk Mvungi na familia yake inamlilia kama
ambavyo wasomi na wanazuoni wanavyomlilia hivyo Serikali inawajibika kutoa
majibu sahihi juu ya kifo chake.
“Damu yake
inadai Watanzania tujiulize Dk Mvungi yuko wapi… wanausalama ndugu yetu yupo
wapi? Wasomi mlikuja hapa kwenye harusi yake mkafurahi naye leo mnatuletea
marehemu,” alisema.
Askofu huyo
alisema kinachofanya taifa kubwa kama Marekani liheshimike ni wepesi wake wa
kuwaeleza wananchi wake ukweli na kutaka Watanzania wasiridhike na majibu
mepesi ya kifo hicho.
“Tusiridhike
na majibu rahisi. Marekani wanafanya uchunguzi mpaka ukweli unajulikana kama
ilivyokuwa kwa Osama Bin Laden… ilichukua muda mrefu lakini ukweli
ulijulikana,” alisema.
Akitoa
salamu za Serikali katika mazishi hayo, Waziri Mkuu Pinda alisema Serikali
inafanya jitihada kuwakamata waliohusika na mauaji hayo.
“Ni kweli
Serikali inafanya jitihada za kuwakamata waliofanya tukio hili la ovyo lakini
hata tukiwapeleka mahakamani wakahukumiwa kunyongwa hiyo si mbadala wa Dk
Mvungi,” alisema.
Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema watamuenzi Dk
Mvungi kwa kukamilisha kazi ya kutunga Katiba Mpya yenye masilahi ya nchi.
“Tunawaomba
wananchi wote tumuenzi Dk Mvungi kwa kuangalia mapendekezo ya Katiba kwa
masilahi ya Taifa ili tupate Katiba ya maridhiano,” alisema.
Mwenyekiti
wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alisema
kifo cha Dk Mvungi kimewaumiza lakini akasisitiza kuwa tukio hilo halitarudisha
nyuma harakati za kupigania haki ya Watanzania.
Baadhi ya
viongozi waliohudhuria mazishi hayo ni Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa
Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Steven Wassira, Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe na Naibu
Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki.
Wengine
waliohudhuria ibada hiyo ni Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia na Naibu
Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba.
Habari na :Mwananchi.








No comments:
Post a Comment