Watu 10
wamefariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa katika ajali mbili zilizotokea katika
Mikoa ya Dodoma na Morogoro jana (Novemba 18,2013).
Katika ajali
ya Dodoma, watu saba wakiwamo wanaume sita na mwanamke mmoja, wamekufa papo
hapo na watano kujeruhiwa, baada ya gari ndogo aina ya Noah waliyokuwa
wakisafiria kutoka Gairo kwenda Morogoro, kugongana uso kwa uso na lori kisha
kupinduka, katika eneo la Dakawa Ranchi , wilayani Mvomero.
Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alisema gari hilo dogo
liligongana na lori aina ya Scania lililokuwa likitokea Morogoro kwenda Dodoma.
Alisema
ajali hiyo ilitokea saa 11:45 alfajiri ya jana na kwamba chanzo ni dereva wa
gari ndogo aina ya Noah, Masoud Hamis, mkazi wa Kihonda, kujaribu kulipita gari
lililokuwa mbele yake na hivyo kukutana na lori hilo.
Dereva huyo
ni miongoni mwa waliokufa katika ajali hiyo.
Mwananchi
ilishuhudia Noah ikiwa imeharibika kwa kiasi kikubwa huku jitihada za kuisogeza
kando ya barabara zikifanywa baada ya kuwatoa maiti na majeruhi.
Kamanda
Shilogile alisema majeruhi wa ajali hiyo wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu, na miili ya waliokufa, imehifadhiwa katika
chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali hiyo.
Waliofariki
kwenye ajali hiyo ni Isack Mehele (25) mfanyakazi wa Kiwanda cha Tumbaku cha Alliance
One cha mjini Morogoro.
Wengine ni, Sam
Elisha (40), ambaye ni daktari wa Mimea, Maugo Salum (30), Sophia Hassan (20)
na Adini Mwisholwa (70) wote wakazi wa Gairo.
Maiti
mwingine ambaye ni mwanaume hajatambuliwa.
Majeruhi
wametambuliwa kuwa ni, Juma Mohamed (21) mkazi wa Gairo, Hashim Ally Dafa (42)
mkazi wa Lushoto, Junior Msenga, Selemani Hamis (20) mkazi wa Babati Manyara, Martin
Msobi, mkazi wa Dumila, Festo Paulo mkazi wa Kimara Mwisho jijini Dar es Salaam
na mwingine ambaye jina lake halikufahamika mara moja.
Daktari
bingwa wa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Francis
Semwene, alisema hali za majeruhi wawili ni mbaya.
Kwa upande
wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Wami Sokoine, Marco Ndesse, aliiomba Serikali
kuweka matuta katika eneo hilo la makazi, ili kuepusha ajali.
Wakati
huohuo, watu watatu wamefariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa katika ajali ya gari
iliyotokea katika Kijiji cha Gulwe, Wilaya ya Mpwapwa.
Ajali hiyo
ilikuja baada ya lori kuacha njia na kuparamia kingo za daraja kabla ya
kutumbukia katika korongo na kupinduka.
Mashuhuda
walisema ilitokea saa 12.00 asubuhi na kuhusisha lori hilo lililokuwa
limesheheni mizigo na watu waliokuwa wanakwenda mnadani.
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Suzan Kaganda, alithibitisha kutokea kwa
ajali hiyo iliyopoteza maisha ya Idd Mbelwa, Burhani Mzuza na mtu aliyefahamika
kwa jina moja la Bakari. Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, Mohamed
Pathan, alisema hospitali yake ilipokea miili ya watu watatu na majeruhi 13.






No comments:
Post a Comment