![]() |
| simu. |
Watumiaji wa
simu wapatao milioni nane wapo hatarini kufungiwa simu zao ifikapo mwishoni mwa
mwezi huu, Tanzania Daima limebaini.
Tayari
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeziandikia kampuni za simu waraka wa
kuzitaka zianze kukata kodi mpya ya laini (simu card) mara moja kuanzia Julai
30, 2013.
Hatua hiyo
inatokana na serikali kushindwa kufuta kodi hiyo ya sh 1,000 iliyopitishwa na
Bunge kama alivyoagiza Rais Jakaya Kikwete baada ya kukutana na wadau wa sekta
ya mawasiliano.
Kwa maana
hiyo kila anayemiliki laini moja ya simu atakatwa sh 3,000; anayemiliki laini
mbili sh 6,000 na anayemiliki laini tatu sh 12,000, lengo ni kuhakikisha
serikali inakusanya sh bilioni 178 zitakazopelekwa kwenye bajeti kuu ya
serikali.
Watumiaji wa
simu sasa watalazimika kulipia kodi hiyo ya miezi mitatu ya Julai, Agosti na
Septemba kwa wakati mmoja.
Bunge
kupitia Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew
Chenge (CCM) lilitaka kuwapo kwa kodi hiyo ili kusaidia shughuli za bajeti ya
Serikali Kuu.
Kupitishwa
kwa kodi hiyo kuliibua malalamiko ya wanasiasa dhidi ya Chenge anayelazimisha
kuwapo kwa kodi hiyo, huku akishindwa kuamini kwamba kuna Mtanzania anayekosa
sh 1,000 kwa mwezi kwa ajili ya laini ya simu.
Malalamiko
hayo yaliendelea hadi kwa wananchi na baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) waliotaka posho za wabunge zipunguzwe ili kuziba pengo
hilo badala ya kuwabebesha wananchi mzigo.
Inadaiwa
kwamba msimamo wa Chenge unaungwa mkono na Spika wa Bunge, Anne Makinda, jambo
lililosababisha kutojadiliwa kwa hoja binafsi ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee
(CHADEMA) iliyohusu kodi hiyo katika mkutano wa Bunge lililopita kwa kisingizio
cha kukosekana kwa muda wa kufanya hivyo.
Hata hivyo,
takwimu zilizotolewa na kampuni za simu zinaonyesha kuwa miongoni mwa wamiliki
wa laini za simu milioni 22; milioni nane wanatumia chini ya sh 1,000 kwa
mwezi.
Baada ya
malalamiko hayo, Rais Kikwete alikutana na wadau wa mawasiliano ambao ni
wamiliki wa kampuni za simu Tanzania (MOAT), Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Waziri wa Fedha, William Mgimwa,
kisha kuwaagiza waiondoe kodi hiyo.
“Rais
alisema lengo kuu la mkutano huo liwe kupendekeza jinsi ya kuziba pengo la sh
bilioni 178 zitakazopotea katika bajeti iwapo kodi hiyo itafutwa.
“Alisema
hawezi kuifuta moja kwa moja kodi hiyo, bila kutafuta njia nyingine za kupata
fedha kujazia pengo litakalotokeza huku tayari Bunge limezipangia matumizi,”
alinukuliwa Makamba baada ya kikao hicho na rais.
Kwa upande
wake, rais alikaririwa akiwaambia wadau hao wa mawasiliano kwamba: “Nakuombeni
kaeni pamoja, wekeni bongo zenu pamoja, wekeni akili yenu pamoja tutafute namna
gani tutajaza pengo hili la sh bilioni 178 endapo tutakubaliana kuwa kodi hii
inawabebesha wananchi mzigo mzito, na kuwa pengine menejimenti ya kodi yenyewe
ni ngumu.”
Licha ya
agizo hilo la rais kutekelezwa kwa MOAT kutakiwa kuongeza kodi nyingine iitwayo
‘Excise duty’ kutoka asilimia 14 hadi 17 bila kujali kwamba katika Bunge la
bajeti kodi hiyo iliongezwa kutoka asilimia 12 hadi asilimia 14, tozo hiyo ya
laini za simu haijaondolewa.
Wachambuzi
wa masuala ya siasa na mawasiliano walisema kutojadiliwa kwa mabadiliko ya kodi
hiyo ya simu ni dalili kwamba Waziri wa Fedha amezidiwa nguvu na kiti cha spika
kinachounga mkono hoja hiyo ya Chenge na kushindwa kutekeleza agizo la rais.
Wataalamu wa
mawasiliano walilieleza gazeti hili kwamba kuongezeka kwa kodi hiyo kutaifanya
Tanzania kuwa na kiwango cha juu cha kodi kuliko nchi nyingine za Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Ushauri wa
wataalamu hao ulibainisha kwamba kuongezeka kwa kodi hiyo kunaleta nafuu kidogo
kuliko ile ya laini za simu inayomuumiza zaidi mwananchi wa kawaida.
Source:Tanzania Daima.






No comments:
Post a Comment