JESHI la
Polisi limekamata watu 15 wakiwemo wengine wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa kundi
la Al-Shabab, wanaohusishwa na tukio la kumwagia tindikali Father wa Parokia ya
Cheju wilaya ya kati Unguja, Anselmo Mwang'amba, pamoja na lita 29 za tindikali.
Watu hao,
wamekamatwa baada ya jeshi hilo kuendesha msako katika maeneo mbali mbali ya
mji wa Zanzibar, ambapo baadhi yao wamedaiwa ni wafuasi wa makundi ya Al-Shabab
lenye msimamo mkali wa kidini lenye maskani yake nchini Somalia.
Kamishna wa
Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema hayo jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari, ofisini kwake Kilimani mjini Zanzibar.
Alisema watu
waliokamatwa wote ni raia wa Tanzania, wanaotuhumiwa kuhusika na matukio ya
umwagiaji tindikali likiwemo kiongozi huyo wa dini lililotekelezwa wakati
akitoka katika kituo cha huduma za mtandao wa internet cha Sun Shine kilichopo
Mlandege mjinii Zanzibar.
Alisema watu
hao walikamatwa katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar, wakiweno watatu
waliokutwa wakijitayarisha kuelekea kwenye kituo cha kundi hilo, ambapo hata
hivyo kamanda huyo hakutaja kilipo kituo hicho wala majina yao.
“Tumekamata
mengi, lakini hatuwezi kusema yote hivi sasa kwani tunaweza kuharibu uchunguzi
wetu,” alisema.
Alisema
uchunguzi wa tukio hilo umeenda sambamba na ukamataji wa tindikali ambayo
imeenea Zanzibar.
Alisema
tindikali hiyo, ipo iliyokamatwa madukani, nyumba za kuishi na baadhi ya ofisi,
ambazo zinazifanyiwa uchunguzi.
Alisema
baadhi ya wahusika wamekamatwa na tindikali iliyozimuliwa na isiyozimuliwa, na
hivi sasa wanahojiwa waeleze walikoipata na kama wana vibali vya kufanya
biashara hiyo ama kuingiza nchini.
Alisema
polisi wameanzisha msako rasmi wa kusaka tindikali katika maeno yote ya
Zanzibar, ikiwa ni hatua inayolenga kupunguza matumizi yasiyofaa nchini.
Alisema
operesheni hiyo inaendeshwa na polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu
wa Serikali.
“Jeshi la
Polisi linawaomba wananchi kuunga mkono katika mapambano haya na waendelee
kutupa taarifa na kutustahamilia, kwani upo uwezekano mkubwa kuwa mapambano
haya yakahusu jamaa zetu,” alisema.
Akizungumzia
juu ya matukio mengine ya umwagiaji wa tindikali, alisema tayari uchunguzi
unaohusu raia wawili wa Uingereza, waliofanyiwa kitendo hicho katika maeneo ya
Mji Mkongwe, unaendelea na watu watatu wamekamatwa kuhusishwa na tukio hilo.
Kuhusu kesi
inayomuhusisha Shekh Fadhil Soraga, alisema wanasubiri matokeo ya Mkurugenzi wa
Mashtaka ili hatua za kuendelea na kesi hiyo ziendelee, huku akisema kesi
iliyokuwa ikimuhusu aliyekuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Rashid Ali
Juma, jalada lake limefungwa baada ya kukosekana ushahidi.
Aidha kesi
inayomuhusu sheha wa shehia ya Tomondo, Mohammed Said Omar, alisema uchunguzi
unaendelea.
Katika hatua nyingine,Huenda Padri
wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mpendae Zanzibar, Anselmo Mwang’amba aliyemwagiwa
tindikali siku tano zilizopita, akasafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu
kutokana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako amelazwa, kudaiwa kushindwa
kumtibu.
Chanzo -
ZanziNews






No comments:
Post a Comment