Wakati wadau
mbalimbali wa sekta ya habari wakifanya harakati za kuitaka serikali
kubadilisha Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976, serikali juzi imeyafungia
magazeti ya Mwananchi na Mtanzania.
Sheria ya
Magazeti ya Mwaka 1976 inampa ruhusa waziri mwenye dhamana ya habari kupiga
marufuku uchapaji na matumizi ya gazeti lolote ambalo anafikiri liko kinyume
cha masilahi ya umma.
Gazeti la
Mtanzania limefungiwa kwa siku 90, huku Mwananchi likifungiwa kwa siku 14, yote
adhabu zao zimeanza juzi Septemba 27, 2013.
Uamuzi huo wa
serikali umekuja mwaka mmoja baada ya kufanya hivyo kwa gazeti la Mwanahalisi
ililolifungia kwa muda usiojulikana, kwa kuandika habari na makala ilizodai ni
za uchochezi, uhasama na uzushi.
Taarifa
iliyosambazwa kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa
Idara ya Habari, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Assah
Mwambene, adhabu hiyo imeanza juzi.
Taarifa hiyo
imebainisha kuwa magazeti hayo yamepewa adhabu hizo kutokana na mwenendo wa
magazeti hayo kuandika habari na makala za uchochezi na uhasama, kwa nia ya
kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vya dola, hivyo kuhatarisha amani
na mshikamano uliopo nchini.
Mwananchi
Mwambene
alisema tangazo la kufungiwa kwa gazeti hilo limetangazwa kwa Tangazo la
Serikali namba 333 la Septemba, 27, 2013.
Alisema
Mwananchi limepewa adhabu hiyo kutokana na hivi karibuni kuchapisha habari
zenye mwelekeo wa uchochezi na uvunjifu wa amani.
Taarifa hiyo
iliongeza kuwa Julai, 17, 2013 katika toleo Namba 4774, lilichapisha habari
isemayo: ‘Mishahara mipya serikalini 2013’, kwa kuchapisha waraka uliozuiliwa
kwa matumizi ya vyombo vya habari, kwakuwa ulikuwa siri na haukupaswa
kuchapishwa magazetini.
Alisema
katika toleo la Jumamosi, la Agosti, 17, 2013 lilichapisha habari yenye kichwa
kisemacho: ‘Waislamu wasali chini ya ulinzi mkali.”
Mwambene
alisema habari hiyo ilikolezwa na picha ya mbwa mkali mwenye hasira, ambapo
picha hiyo ilitoa tafsiri ya kuwa Jeshi la Polisi lilipeleka mbwa katika maeneo
ya ibada ya waumini wa dini ya Kiislamu.
Alisema
jambo hilo halikuwa la ukweli kwa sababu Jeshi la Polisi katika doria siku hiyo
halikupeleka mbwa katika maeneo ya misikiti.
Alibainisha
kuwa serikali na Jeshi la Polisi linaheshimu na kuzingatia maadili ya dini ya
Kiislamu na haliwezi kupitisha au kuingiza mbwa katika maeneo ya ibada.
Aliongeza
kuwa kuchapisha habari hiyo iliyokolezwa na picha ya mbwa ni uchochezi wa
kulichonganisha Jeshi la Polisi na waumini wa dini ya Kiislamu. Mbwa ni najisi,
hapaswi kuingia katika maeneo ya ibada.
Mwananchi
wangoja barua
Akizungumza
na Tanzania Daima Jumapili, Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi, Bakari Machumu,
alisema mpaka jana jioni hawakuwa wamepata barua hiyo na wanaisubiri ili
waangalie hatua za kuchukua.
Machumu
alisema wataijibu serikali kulingana na hoja walizowaandikia na hawatafanya
hivyo kupitia tamko la Mkurugenzi wa Idara ya Habari alilolitoka katika mkutano
wake na waandishi wa habari jana.
“Siwezi
kukueleza hatua tutakazozichukua dhidi ya uamuzi wa serikali mpaka pale
watakapotuandikia barua, mimi nimeona tamko lakini hawajatuletea barua rasmi,”
alisema.
Kibano cha
Mtanzania
Mwambene
alisema Mtanzania limefungiwa kutochapishwa kwa kuchapisha habari zenye
uchochezi na serikali inadai imeshalionya mara nyingi lirekebishe mtindo wake
wa uandishi wa kichochezi na lizingatie maadili, sheria na kanuni za fani ya
habari.
Alisema
pamoja na kuonywa, gazeti hilo halikuonesha kuzingatia maelekezo ya Msajili wa
Magazeti.
Mwambene
alisema katika toleo Namba 7262 la Machi 20, 2013, liliandika habari yenye
kichwa kisemacho: ‘Urais wa damu’.
Juni 12,
2013,toleo Namba 7344, lilichapisha makala isemayo: ‘Mapinduzi hayaepukiki.’
Alisema
Septemba 18, 2013 katika toleo Namba 73414 ukurasa wa mbele lilichapisha kichwa
cha habari kisemacho: ‘Serikali yanuka damu.’
Alibainisha
kuwa taarifa hiyo ya serikali ilikolezwa na picha zilizounganishwa kwa ustadi
mkubwa, kwa kutumia kompyuta kutapakaza rangi nyekundu mithili ya damu nyingi
kumwagika.
Mwambene
alisema katika habari hiyo gazeti hilo limedai bila uthibitisho kuwa Jeshi la
Polisi linahusika na wahanga walioumizwa na watu wasiojulikana kwa kumwagiwa
tindikali na waliovamiwa na kujeruhiwa vibaya.
Aliongeza
kuwa gazeti hilo limeishutumu serikali kuwa goigoi katika kushughulikia matukio
yenye sura ya kigaidi.
Mwambene
alisema habari hiyo ni ya kichochezi na ina lengo la kuwafanya wananchi
wavichukie vyombo vya ulinzi na usalama, wavione kuwa haviwasaidii.
Alibainisha
kuwa kutokana na makosa yaliyotajwa hapo juu, serikali imelifungia gazeti la
Mtanzania kutochapishwa kwa muda wa siku tisini (90) kwa Tangazo la Serikali
Namba 332 la Septemba 27, 2013.
Mtanzania
wang’aka
Mtendaji
Mkuu wa New Habari 2006, Hussein Bashe, alisema uamuzi huo wa serikali si wa
haki na si sahihi.
“Wamelifungia
kimya kimya, tarehe 27, hatujaona barua wala hatujaitwa, hii inashangaza sana.
Tumeiona katika mitandao, hii imetusikitisha. Hii ni taswira ya aina ya
viongozi tulionao katika nchi hii, wizara hiyo hiyo naibu waziri wake alitutaka
tuandike barua ya kuomba radhi kutokana na stori yetu, tulifanya hivyo. ..
lakini leo mkurugenzi ametuandikia barua ya kutufungia,” alisema Bashe.
Bashe
alisema adhabu hiyo inawapa funzo la kufanya kazi na aina ya viongozi na
watendaji wa serikali wanaoamua mambo bila kuwahoji watuhumiwa.
“Nawaomba
wenzangu tuungane kupambana na sheria hii kandamizi, la sivyo wataendelea
kuitumia vibaya,” alisema.
Sheria ya
Magazeti
Sheria ya
Magazeti ya Mwaka 1976 inampa ruhusa waziri mwenye dhamana ya habari mamlaka
makubwa ya kuweza kupiga marufuku uchapaji na matumizi ya gazeti lolote ambalo
anafikiri liko kinyume cha masilahi ya umma.
Kwa vile
sheria haitoi orodha halisi ya vigezo vya kutumika ili kupiga marufuku, inampa
waziri hiari ambayo anaweza kuitumia bila sababu za msingi, ama hata kuitumia
kwa sababu binafsi kunyamazisha magazeti yaliyo makini na uandishi wa habari za
kitafiti.
Katika sehemu ya pili ya sheria hii, kipengele cha 5(2), waziri
anapewa mamlaka kama ya kutoa tangazo kupitia Gazeti la Serikali, kulizuia
gazeti lolote kufanya kazi zihusianazo na baadhi ya vipengele ama vipengele
vyote vya sehemu hii, aidha moja kwa moja ama kwa kuzingatia masharti ambayo
waziri ataona yanafaa.
Katika
mwelekeo huohuo, kipengele cha 25(1) cha sheria hiyohiyo kinampa waziri uwezo
wa kupiga marufuku uchapaji wa gazeti lolote, wakati wowote atakaoona inafaa.
Kipengele kinasema:
‘Pale waziri
anapoona kwamba ni kwa masilahi ya umma, ama ni kwa masilahi ya amani na
utulivu kufanya hivyo, anaweza, kwa kutoa agizo kupitia Gazeti la Serikali
kuagiza kwamba gazeti lililotajwa katika agizo hilo liache kuchapwa tangu
tarehe ile iliyoelezwa katika agizo.
Mamlaka hayo
makubwa aliyonayo waziri yanaweza kutumiwa kinyume cha masilahi ya umma,
tofauti na ilivyokusudiwa.
Wakitoa
maoni yao kuhusu kufungiwa kwa magazeti hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Zitto Kabwe na Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, wamelaani kitendo cha kufungiwa kwa
magazeti ya Mwananchi na Mtanzania, wakisema ni dalili za utawala unaoanguka.
Walisema
hayo walipokuwa wakihutubia mkutano wa hadhara eneo la Ugindoni, Kata ya Mji
Mwema, Jimbo la Kigamboni. Wamewaomba wananchi kutokubali jambo hilo, kwani
halikubaliki.
Zitto alisema kwamba watawala wanaendelea kupata nguvu ya
kuendelea kufungia vyombo vya habari kwa sababu ya ukimya wa wananchi.
“Wananchi
mkichukua mamlaka yenu kama inavyosema Katiba ya nchi, chukueni mamlaka yenu
hata mambo ya hovyo wanayofanya CCM bungeni yatakwisha.
Leo nikiwa jukwaani
hapa nimesikia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania yamefungiwa, yaani watawala
walipofungia MwanaHalisi na wananchi mkakubali kuwa kimya, wanaweza kufungia
magazeti yote ili yaache kuripoti habari.
Source:Tanzania Daima.






No comments:
Post a Comment