WAZIRI MULUGO:Matokeo mabovu ya Kidato cha Nne 2012,Kuchelewesha Matokeo ya Kidato cha Sita 2012/2013. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Sunday, May 12, 2013

WAZIRI MULUGO:Matokeo mabovu ya Kidato cha Nne 2012,Kuchelewesha Matokeo ya Kidato cha Sita 2012/2013.



Matokeo ya mtihani wa kidato cha sita yaliyotarajiwa kutangazwa mwezi  huu yatachelewa  ili kutoa nafasi kwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta),  kurekebisha matokeo mabaya ya mitihani  kidato cha nne ya mwaka jana yaliyofutwa na serikali  mwezi huu.




Matokeo ya kidato cha sita ambayo huwa yanatangazwa mwanzoni  mwa mwezi Mei mpaka sasa hayajatolewa  na kwamba hayatatangazwa mpaka matokeo mapya ya kidato cha nne yatakaporekebishwa rasmi.




Alipoulizwa  juu ya suala hilo, Naibu Waziri   wa Elimu na  Mfunzo ya Ufundi  Philipo Mulugo alisema ingawa wakati huu ndio unaopaswa yatangazwe matokeo ya kidato cha sita haitafanyika hivyo hadi yatangazwe matokeo mapya ya kidato cha nne baada ya kufutwa.




Hata hivyo, akasema huenda yakatolewa  pamoja au yakafuata wakati mwingine lakini mara baada ya  kukamilisha kazi ya kurejea na kusahihisha matokeo ya kidato cha nne.




Philipo Mulugo.
"Siyo kwamba yamechelewa kwani muda wa kujiunga na chuo ni Septemba hivyo haitawaathiri kwa hilo," alisema Mulugo.




Kuhusu hatma ya wanafunzi wa kidato cha nne ambao wapo mashuleni wanaendelea na masomo ya kidato cha sita, alisema  kama kutakuwa na wanafunzi ambao wapo madarasani  shule zilizowasajili  zitakuwa hazijafuata mfumo wa elimu unavyoelekeza.




Alifafanua kuwa mfumo wa elimu kwa kidato cha nne ulibadilishwa na kwamba endapo mwanafunzi akifaulu anatakiwa kujiunga rasmi kidato cha sita  Julai na si vinginevyo.




Alisema licha ya  ucheleweshaji  wa matokeo  hali hiyo haikuwaathiri wanafunzi hao kwa kuwa ratiba ya kwenda masomoni  haijaanza kwa mujibu wa kalenda  ya shule ya serikali.




Bungeni mjini Dodoma.
Wiki iliyopita serikali ilichukua uamuzi mgumu na kufuta matokeo kidato cha nne ya mwaka 2012.




Uamuzi huo mgumu ulifanywa na Baraza la Mawaziri kabla ya tume ya Waziri Mkuu kuwasilisha ripoti yake kama njia ya kuwafariji wanafunzi waliofeli mtihani na kulitaka Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kuyapanga upya kwa kutumia utaratibu wa kupanga madaraja uliotumika mwaka 2011.




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, akiwasilisha kauli ya serikali bungeni mjini Dodoma Ijumaa iliyopita, alisema utaratibu mpya uliotumika kupanga madaraja ulichangia katika matokeo mabaya yaliyosababisha zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi kupata sifuri.




Februari mwaka huu, Dk. Kawambwa alitangaza matokeo ya kidato cha nne na kubainisha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 walipata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 walipata daraja la nne.




Watahiniwa walikuwa 456,137 kati yao wa shule wakiwa 397,136 huku wa kujitegemea 68,806.



Kwa mujibu wa matokeo hayo, watahiniwa waliopata daraja la kwanza ni 1,641, wavulana wakiwa 1,073 na wasichana 568, daraja la pili ni 6,453, wavulana wakiwa 4,456 na wasichana 1,997.




Matokeo hayo yaliibua mjadala mkali huku makundi mbalimbali ya jamii yakihoji sababu zilizosababisha wanafunzi wengi kufeli na kutaka Kawambwa na wasaidizi wake wawajibike kabla Waziri Mkuu kuunda tume iliyoongozwa na Profesa Sifuni Mchome kuchunguza ili kupata ufumbuzi wa kudumu.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad