Wanajeshi
wa Tanzania wanaokwenda kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC) wametakiwa kudumisha utamaduni wa askari wa kulinda amani wa Tanzania
katika maeneo mbali mbali duniani kwa kuifanya kazi hiyo kwa heshima, nidhamu
na utii ili kulinda heshima yao wenyewe na ile ya Tanzania.
Askari
hao wamekumbushwa utamaduni huo wa askari wa kulinda amani wa Tanzania katika
maeneo mbali mbali duniani na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri
Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Rais
na Amiri Jeshi Mkuu alikuwa akiwaaga wanajeshi wa Tanzania wanaokwenda kulinda
amani chini ya Umoja wa Mataifa katika DRC katika hafla iliyofanyika leo,
Jumatano, Mei 8, 2012, kwenye Makao Makuu ya Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu la
Tanzania yaliyoko Msangani, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Akizungumza
na askari hao, Rais Kikwete amewaambia kuwa hana wasiwasi kuhusu uwezo wao wa
kutelekeza majukumu yao yanayowapeleka DRC isipokuwa tu kwamba waifanye kazi
hiyo vizuri na kulingana na utamaduni wa majeshi ya kulinda amani ya Tanzania
katika sehemu mbali mbali duniani.
“Tunakwenda
kutelekeza majukumu ya Umoja wa Mataifa, sina shaka kuwa majukumu yenu
mnayaelewa vizuri. Kazi yetu ni kulinda amani na wala hatuendi kupigana na
yoyote. Kazi ya kijeshi mnaijua vizuri vile vile na kwa hili pia sina wasiwasi
hata kidogo,” amesema Amiri Jeshi Mkuu na kuongeza.
“Kubwa
ambalo lazima tulikumbuke ni kwamba nchi yetu kila ilikopeleka majeshi ya
kulinda amani imejenga utamaduni wa pekee. Imejenga utamaduni wa askari wetu
kuifanya kazi ya kulinda amani kwa heshima, kwa nidhamu na kwa utii wa kiwango
cha juu. Hii ni heshima kwetu binafsi na heshima kwa taifa letu. Nawashukuruni
na nawatakie kila la heri”
Kama
ishara ya kuagana na askari hao, Rais na Amiri Jeshi Mkuu amemkabidhi Bendera
ya Taifa Luteni Kanali Orestess Cassian Komba, Kamanda wa Kikosi cha Tanzania
katika DRC ambacho kitajulikana kwa jina la TANZBATT 1-DRC, akimwambia “Bendera
na Ikapepee”.
Katika
jukumu la kulinda amani Mashariki mwa DRC, Kikosi cha Tanzania chenye askari
1281, kitajiunga na vikosi vya Malawi na Afrika Kusini ambavyo vyote vitakuwa
chini ya Kamanda wa Brigedi hiyo, Brigedia Jenerali James Mwakibolwa wa
Tanzania pia. Kundi la kwanza la askari hao Tanzania linaondoka nchini kesho.
Majeshi
hayo ya Tanzania yatalinda amani katika DRC chini ya Azimio Nambari 2098 (2013)
la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Imetolewa
na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar
es Salaam.
8
Mei, 2013
No comments:
Post a Comment