Askari
wakiwa kwenye msafara wa kumsindikiza Sheikh Ponda baada ya kuachiwa.
|
Sheikh Ponda
akiswali katika Msikitini wa Mtambani, Kinondoni Dar es Salaam.
|
Wafuasi wa
Sheik Ponda wakimshangilia alipokuwa akihutubia ndani ya Msikiti wa Mtambani.
|
Msafara
ukavamiwa na wafuasi baada ya dereva wa garilake kusimamisha awasalimie wafuasi
hao jambo ambalo polisi walikuwa hawalitaki na kuzua mabishano mazito lwenye
mataa ya Maktaba Squire.
|
Ulinzi wa
Ponda wakati wa kuondoka mahakamani hapo baada ya kuachiliwa.
|
"Takbir
... Takbir ..." zilitawala katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana
baada ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa
Ponda na wenzake 49 kuachiwa huru katika kesi iliyokuwa ikiwakabili.
Washtakiwa
hao waliachiwa huru na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
Victoria Nongwa.
Katika kesi
hiyo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini
Kweka na upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili Yahya Njama.
Akisoma
hukumu Hakimu Nongwa alisema: “Jamhuri imeshindwa kuthibitisha mashtaka kuanzia
shtaka la kwanza, tatu, nne na la tano kwa washtakiwa wote, katika mashtaka
hayo washtakiwa wote kuanzia wa kwanza hadi 50 hawana hatia.
“Katika
shtaka la pili la kuingia kwa nguvu katika uwanja wa Markaz Chang’ombe, upande
wa mashtaka umeweza kuthibitisha kwamba Ponda aliingia kwa nguvu hivyo anatiwa
hatiani kwa kosa hilo.
“Shtaka la
kuingia kwa nguvu halielezi adhabu inayostahili kutolewa lakini mahakama
inaweza kumpa adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela au faini au vyote kwa
pamoja.
Akapewa
ulinzi tena!
|
“Kwa
mshtakiwa wa kwanza (Ponda) hakuna kumbukumbu kwamba ni mkosaji wa makosa
mengine… mahakama inazingatia pia mshtakiwa alikaa rumande kwa muda mrefu
kuanzia Oktoba 18 mwaka jana hadi leo hivyo inamwachiwa kwa masharti.
Alisema
mahakama inamwachia Ponda kwa masharti ya kulinda amani, awe mwenye tabia njema
kwa miezi 12 na endapo atashindwa atarudi mahakamani apewe adhabu nyingine
inayostahili.
Ponda
alisaini fomu za kukubali masharti aliyopewa na kuachiwa huru huku wafuasi
waliorundikana nje ya mahakama wakimsubiri kwa ajili ya kumlaki.
Hata hivyo
ndoto zao zilizimwa na polisi ambao waliamuru asitoke nje kwa miguu.
“Hakuna
usitoke nje…. Gari litaingia humu humu ndani utapanda, “ hayo yalikuwa maneno
ya askari na maofisa usalama waliomzingira Ponda asitoke nje kwa miguu.
Naye Ponda
wakati akitoka nje ya mahakama alisikika akisema: “Sikuachiwa kwa huruma ya
mtu, ilikuwa ni haki yangu, kuna kesi nyingine nyingi nzito kubwa ambazo
Serikali inashindwa kuzithibitisha.
“Dola
inatengeneza kesi nzito hazina ushahidi, inaharibu mfumo wa usalama, kesi zote
hizo zinatokana na mashinikizo ya siasa, tuache kutengeneza kesi kwa ajili ya
masuala ya siasa.”
Akaingia
kwenye gari!
|
Gari aina ya
BIGHORN yenye rangi nyeusi ilipoingia ndani ya uzio wa mahakama, Ponda, mkewe
na ndugu mmoja waliingia ndani pamoja na maofisa usalama kwa ajili ya
kumsindikiza hadi nyumbani kwake.
Ponda
alitoka nje ya mahakama akiwa ndani ya gari ambalo lilikuwa likisindikizwa na
magari ya polisi wenye silaha.
Waumini wa
Kiislamu ambao walikuwa nje ya uzio wa mahakama waliishia kupunga mikono huku
wakisema Takbir…Takbir.
Awali
akisoma hukumu hiyo, Hakimu Nongwa alisema upande wa mashtaka ulikuwa na
mashahidi 16 na upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi 53.
Alisema
watuhumiwa walikuwa wanakabiliwa na mashitaka matano ambayo ni kula njama,
kuingia kwa nguvu uwanja wa Markaz Chang’ombe mali ya Agritanza Limited na
kuuzuia kwa nguvu uwanja huo.
Mengine ni
kuiba vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani zaidi ya Sh milioni 59 wakati
mashitaka ya kushawishi waislamu kukusanyika katika uwanja huo yakimkabili
Sheikh Ponda na Salehe Mukadamu.
“Matukio
hayo yalitokea kati ya Oktoba 12 na 16 mwaka jana. Shtaka la kula njama
halijaeleza washtakiwa walikula njama kutenda kosa gani… mahakama inajiuliza ni
kosa gani walikula njama kati ya mashtaka yanayowakabili.
“Katika kesi
hii mahakama haijaona hata shahidi mmoja aliyesema jinsi washtakiwa walivyokula
njama, mahakama inaona kosa la kula njama halijathibitika, inawaachia huru
washtakiwa wote,”alisema Nongwa.
Nongwa
alisema shtaka la kushawishi halikusema jinsi Ponda na Mukadamu
walivyowashawishi waislamu kukusanyika katika uwanja wa Markaz na hakuna
shahidi aliyetaja watuhumiwa walioshawishiwa hivyo shtaka hilo pia
halijathibitishwa.
Alisema
vilevile hakuna ushahidi kwamba washtakiwa wote ni wafuasi wa Sheikh Ponda.
“Shtaka la
pili la kuingia kwa nguvu limethibitika bila kuacha shaka kwamba Sheikh Ponda
aliingia katika uwanja huo hivyo anatiwa hatiani. Washtakiwa wengine wote
kuanzia wa pili hadi wa 50 katika shtaka hili wanaachiwa huru,”alisema.
Hakimu
Nongwa alisema shtaka la kuzuia kwa nguvu uwanja huo halijathibitika kwa sababu
hiyo washtakiwa wote wanaachiwa huru katika shtaka hilo na shtaka la wizi pia
halijathibitika.
Alisema
hakuna ushahidi kwamba msikiti wa muda uliojengwa na akina Sheikh Ponda ulikuwa
na thamani ya zaidi ya Sh milioni 59, sawa na thamani ya mali za Kampuni ya
Agritanza Limited.
“Naona shaka
kama malighafi yote iliyojenga msikiti wa muda ilikuwa mali ya Agritanza
Limited, mahakama inatia shaka hivyo kosa la wizi halijathibitika. Washtakiwa
wanaachiwa huru kwa shitaka hilo pia.
“Upelelezi
katika kesi hii haukufanyika vizuri, ungefanywa vizuri washtakiwa wote
wangeweza kutiwa hatiani kwani ukisikiliza ushahidi wao unaweza kuhisi kwamba
walishiriki lakini mahakama haiwezi kuwatia hatia kwa vile wenye jukumu la
kuthibitisha mashtaka ni Jamhuri,” alisema Nongwa.
Hakimu
Nongwa alisema ni jambo lisilobishaniwa kwamba kipande cha ardhi kinachodaiwa
kuwa cha Agritanza Limited kina mgogoro.
BAKWATA
walibadilishana na Kampuni ya Agritanza Limited bila waislamu wengine kuridhia.
Mahakama ya
Kisutu haina uwezo wa kumaliza mgogoro wa ardhi hivyo wasioridhika wanatakiwa
kufuata taratibu kwa kupeleka madai yao katika Mahakama ya Ardhi.
No comments:
Post a Comment