![]() |
| Bangladesh, Dhaka. |
Vikosi vya
uokoaji vinasema, watu wapatao 30 wamefariki dunia na mamia wengine wanahofiwa
kukwama baada ya jingo la ghorofa nane kuporomoka katika mji mkuu wa
Bangladesh, Dhaka.
Juhudi za ziada zinaendelea kuwaokoa watu walionaswa kwenye vifusi. Watu wapatao 200 wamejeruhiwa kufuatia ajali hiyo. Jeshi linasaidia shughuli za uokoaji katika eneo la tukio nje kidogo ya jiji la Dhaka.
Matukio ya majengo kuporomoka nchini Bangladesh ni ya kawaida kutokana na majengo mengi marefu kujengwa kinyume na sheria za ujenzi.
Jengo lililoporomoka lilikuwa na kiwanda cha nguo, benki na maduka kadhaa. Liliporomoka asubuhi wakati watu wakielekea makazini.
Watu wengi wamekusanyika karibu na eneo la tukio wakiwatafuta ndugu na marafiki. Haijafahamika kilichosababisha jengo hilo kuporomoka, lakini vyombo vya habari nchini humo vimesema kwamba, nyufa zilionekana kwenye jengo hilo siku ya Jumanne.
Polisi wameviambia vyombo vya habari kwamba, waliona ghafla sehemu ya nyuma ya jengo hilo ikianguka Jumatano asubuhi na baada ya muda mfupi jengo lote likafuatia isipokua nguzo kuu na sehemu ya ukuta wa mbele hali iliyosababisha taharuki.
Maafisa wanasema, ni sehemu ya chini pekee ya jengo hilo la Rana Plaza ndio ilibakia imara baada ya kuporomoka, wakati wanajeshi na waokoaji wa idara ya zimamoto wakiwa na vifaa vya kukatia vyuma na matingatinga wakifukua vifusi ili kuwaokoa watu walionaswa .
Mkuu wa polisi wa eneo hilo, Mohammed Asaduzzaman, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, hali ilikua mbaya sana.
Novemba mwaka jana, moto uliounguza kiwanda cha nguo nje ya jiji la Dhaka uliua watu 110 na kusababisha wananchi kupigia kelele kuhusu viwango vya usalama kwenye viwanda husika.
Mara mwisho
jengo la ghorofa nne liliporomoka jijini Dhaka mnamo mwaka 2010 na kusababisha
vifo vya watu 25 na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Nchini Tanzania mwezi wa Aprili
29 ghorofa lilopo katika eneo la Posta jijini Dar es salaam nchini Tanzania
lilianguka na kuuwa watu zaidi ya 30 na kujeruhi mamia ya watu waliokuwepo eneo
hilo na kusababisha uharibifu wa mali.






No comments:
Post a Comment