![]() |
| Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es salaam |
Viongozi wa dini wamewataka waumini kote nchini
kulinda amani na umoja uliopo ili nchi isije ikaingia kwenye
mgawanyiko wa kidini na kuleta machafuko hapa Tanzania.
Wito huo umetolewa na viongozi wa dini leo Ikulu ya
Dar-Es-Salaam mara baada ya kikao cha pamoja baina ya viongozi wa dini na Rais
Jakaya Kikwete.
Viongozi hao wa dini wamefika leo wakiongozwa na
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania (TEC).
Viongozi wengine wametokea Baraza la Kikristo
Tanzania (CCT) Seventh Day Advertist (SDA) na Baraza la Pentekoste Tanzania
(PCT).
Mkutano huo umeanza kwa Askofu Ngalalekumtwa kusoma
tamko lao la pamoja kwa Rais Kikwete ambalo ndilo limetoa muongozo wa
mazungumzo hayo ya leo ambayo yamehusu Amani na Usalama wa Taifa na migogoro ya
kidini ndani ya jamii.
Mkutano wa viongozi wa dini ya Kikristo Tanzania ni
mojawapo ya jitihada za Rais Kikwete kutafuta muafaka na kutafuta utatuzi wa
hali ya sintofahamu ambayo inanyemelea nchi yetu katika kipindi hiki.
“Nataka tuzungumze ni namna gani tunaweza kutoka
kwenye hali hii na tunakwendaje mbele zaidi na kuhakikisha nchi yetu bado
inakua ya amani na umoja kama ilivyozoeleka” Rais amesema na kutoa nafasi
kwa viongozi wa dini kutoa maoni yao.
Viongozi hao wa dini wamemueleza Rais Kikwete kuwa
wanaunga mkono jitihada zake za kutafuta amani na kwa pamoja wamekubaliana
uandaliwe mkutano wa pamoja baina ya viongozi wa dini zote ambapo masuala ya
amani na umoja wa nchi utajadiliwa kwa kirefu.
Katika kikao cha leo pande zote zimekubaliana kuwa
kuna changamoto zilizoko sasa zinahitaji kutatuliwa haraka iwezekanavyo ili
kuepusha nchi kutumbukia katika mgogoro mkubwa zaidi, na pia kukubaliana kuwa
pande zote, kwa maana ya serikali na taasisi za dini, zinawajibu mkubwa wa
kuhakikisha amani inadumu.
Kabla ya kikao cha leo , Rais amewahi kukutana na
viongozi wa dini ya kiislamu na kikristo mmoja mmoja ambapo alikua akitafuta
maoni na ushauri wa pande zote kabla ya pande zote hazijakaa pamoja na kuwa na
msimamo wa pamoja.
Kikao cha leo kimehitimisha jitihada hizo na
kinachofuata ni mkutano mmoja ambapo Rais Kikwete atakutana na viongozi wa dini
zote kwa pamoja hivi karibuni.
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu-DSM
23 Aprili, 2013









No comments:
Post a Comment