![]() |
|
Timu ya Azam
FC imeisogelea Simba kileleni mwa Ligi Kuu ya soka ya Vodacom Tanzania Bara
baada ya kuifunga African Lyon bao 1-0 katika mchezo wa ligi hiyo kwenye Uwanja
wa Chamazi, Dar es Salaam.
Azam FC ambayo
ilimaliza mechi hiyo ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja baada ya beki wake Samir hajji Nuhu kutolewa
nje kwa kadi nyekundu dakika ya 83 kwa kuonyeshwa kadi ya pili ya njano,
imefikisha pointi 13 sawa mabingwa watetezi Simba, ambao wapo kileleni sasa kwa
wastani wa mabao tu.
Hadi
mapumziko, Azam walikuwa tayari mbele kwa bao hilo, lililotiwa kimiani na
mfungaji bora wa Ligi Kuu John Raphael
Bocco ‘Adebayor’ katika dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza baada ya kutimu
dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Katika
mchezo mwingine, wa leo wenyeji Ruvu Shooting wameifunga Coastal Union ya Tanga
mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani, mabao
yaliyotiwa kimiani na Hussein Sued dakika ya sita na Hassan Dilunga dakika ya
12.
Ligi hiyo
itaendelea kesho kwa mabingwa watetezi na vinara wa ligi hiyo, Simba kuumana na
Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam, wakati vibonde wa ligi hiyo, Mgambo Shooting watakuwa wenyeji wa
vibonde wengine wa ligi hiyo, Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini
Tanga, wakati Toto Africans wataikaribisha JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Kirumba
mjini Mwanza na Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja
wa Sokoine mjini Mbeya.
Kagera Sugar
wataikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba Jumatatu.
Hadi sasa,
mwenendo wa ligi unaonyesha ushindani ni kati ya mabingwa watetezi, Simba SC na
washindi wa pili wa msimu uliopita, Azam FC ambazo zinakabana kileleni.
Hali bado si
nzuri kwa mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo, Yanga SC ambayo inazidiwa pointi
tano na mabingwa watetezi, Simba SC ambao pia ni wapinzani wao wa jadi.
Timu mbili
kati ya tatu zilizopanda Ligi Kuu msimu huu JKT Mgambo na Polisi Morogoro ndizo
zipo mkiani, wakati Prisons ndio inaonekana kuwa imara zaidi, kwani ipo nafasi
ya tano katika msimamo huo.
No comments:
Post a Comment