Simba na Yanga, zakabidhiwa vifaa mbalimbali vya michezo vyenye thamani ya sh milioni 68 kutoka kwa mdhamini wao mkuu, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager kwa ajili ya msimu mpya wa ligi kuu. - Mwana Wa Makonda

Muhtasari

X-BET


Post Top Ad

Thursday, September 06, 2012

Simba na Yanga, zakabidhiwa vifaa mbalimbali vya michezo vyenye thamani ya sh milioni 68 kutoka kwa mdhamini wao mkuu, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager kwa ajili ya msimu mpya wa ligi kuu.


Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu (kushoto) na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ (kulia), wakionesha baadhi ya vifaa vya michezo  walivyokabidhiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ambao ndio wadhamini wakuu wa klabu hizo. Wa pili kushoto ni Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe na Mkurugenzi wa Mashindano, Saad Kawemba. Hafla hiyo ilifanyika katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jijini Dar es Salaam.



Klabu  kongwe nchini za Simba na Yanga, zimekabidhiwa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh milioni 34 kila moja kutoka kwa mdhamini wao mkuu, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager.


George Kavishe
Akikabidhi vifaa hivyo katika Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jijini Dar es Salaam, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, alisema, kukabidhi vifaa hivyo ni moja ya sehemu katika mkataba baina yao na klabu hizo.


Kavishe alisema lengo kubwa la kudhamini timu hizo ni kutokana na historia kubwa ya klabu hizo, pamoja na kuleta ushindani wenye burudani kwa Watanzania, ambao ni wadau wakubwa wa kunywa kinywaji hicho.


“Sisi tunafanya kazi vema na klabu hizi, tunajisikia faraja kubwa kutokana na timu hizi kuwa na historia kubwa hapa nchini na ushindani mkubwa katika soka na huu ni udhamini wa nusu msimu peke yake,” alisema Kavishe.


Aidha vifaa hivyo vilivyotolewa ni pamoja na jezi, bukta, soksi, viatu, bips, nguo za kusafiria, vikinga ugoko na mifuko.


Katika hatua nyingine, Kavishe alisema, kuhusu mabasi ya timu hizo, wako katika hatua za mwisho kuyakabidhi kwa wahusika, kwani tayari yamewasili hapa nchini, ambapo kuna mambo kadhaa wanayakamilisha.


Kaburu
Akizungumza kwa niaba ya klabu ya Simba, Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, aliwashukuru wadhamini hao kwa moyo walionao, huku akiwaahidi kuhakikisha wanafanya vema na kushinda ili kuonesha umuhimu wa vifaa ambavyo wamewapa.



“Nawashukuru TBL kwa kutudhamini na kuona umuhimu kwa sisi Simba bila ya kupepesa macho na ndiyo maana hata sisi tutapigana kufa na kupona ili kuhakikisha tunavitendea haki vifaa hivi,” alisema Kaburu.


Louis Sendeu
Kwa upande wa Yanga, Ofisa Habari wake, Louis Sendeu, naye aliishukuru TBL, huku akiwaomba kutoishia kwa Simba na Yanga, bali waziangalie na timu nyingine.



“Tunawashukuru sana ila msiishie kwa Yanga na Simba tu, mziangalie na klabu nyingine ambazo zinasuasua,” alisema Sendeu.


Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe (kushoto) akimkabidhi baadhi ya vifaa vya michezo Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na katikati ni Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba.


Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu (kushoto) akipokea vifaa vya michezo kutoka kwa Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe.


Kwa mujibu wa shirikisho la mpira wa miguu nchini Tanzania TFF,Michuano ya Ligi Kuu kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kwa msimu wa 2012/2013 itaanza Septemba 15 mwaka huu kwa timu zote 14 kujitupa kwenye viwanja tofauti.



Mechi za ufunguzi zitakuwa kati ya Simba vs African Lyon (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Polisi Morogoro vs Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro), Tanzania Prisons vs Yanga (Sokoine, Mbeya), Mgambo JKT vs Coastal Union (Mkwakwani, Tanga), JKT Ruvu vs Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), Kagera Sugar vs Azam (Kaitaba, Bukoba) na Toto Africans vs Oljoro JKT (Kirumba, Mwanza).


Mzunguko wa kwanza (first round) utamalizika Novemba 11 mwaka huu ambapo kwenye mzunguko huo mechi ya watani wa jadi Yanga na Simba itachezwa Oktoba 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Ligi hiyo itamalizika Mei 18 mwakani kwa mechi kati ya Toto Africans vs Ruvu Shooting (Kirumba), Mgambo JKT vs African Lyon (Mkwakwani), JKT Ruvu vs Mtibwa Sugar (Azam Complex), Tanzania Prisons vs Kagera Sugar (Sokoine), Simba vs Yanga (Uwanja wa Taifa), Oljoro JKT vs Azam (Sheikh Amri Abeid Kaluta) na Polisi Morogoro vs Coastal Union (Jamhuri).


Endapo Simba na Azam hazitafanikiwa kuvuka hatua mojawapo ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, ratiba hiyo itafanyiwa marekebisho.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad