Na
Victor Bariety, Geita.
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, amesema Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kiko jirani na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Pinda alitoa kauli hiyo juzi wilayani hapa kabla ya kuanza ziara yake katika
Vijiji vya Bugulula na Senga wilayani Geita kwa ajili ya kuzindua miradi ya maendeleo.
Katika
kijiji cha Bugulula, Waziri Mkuu alizindua mradi wa ufugaji wa kisasa wa nyuki
na Senga alifungua jengo la kliniki ya baba, mama na watoto.
Wakati
Waziri Mkuu akitoa kauli hiyo, alikuwa akimtambulisha Mbunge wa Bukombe,
Profesa Kulikoyela Kahigi (CHADEMA).
Baada
ya kauli hiyo, baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali
walionekana kucheka.
Awali,
akizungumza mjini hapa, Pinda alisema, migogoro ya wachimbaji wadogo wadogo wa
dhahabu dhidi ya wawekezaji wakubwa, haitakwisha kama hawatatengewa maeneo ya
kuruhusu kufanya shughuli za uchimbaji.
Kutokana
na hali hiyo, alisema kuna haja kwa wawekezaji wakubwa kukubali kutenga maeneo
kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo ambao wamekuwa wakidaiwa kuvamia baadhi
ya maeneo ya migodi kwa ajili ya kujitafutia maisha.
Alisema,
migogoro inayotokea sasa inajenga uhusiano mbaya kwa wachimbaji wadogo na
wakubwa na jamii inayozunguka maeneo hayo.
"Suala
hili la migogoro ya wawekezaji wakubwa dhidi ya wachimbaji wazalendo wadogo
haliwezi kwisha kama wamiliki wa migodi mikubwa hawatakuwa tayari kukubali
kuwatengea walau maeneo kidogo wachimbaji wadogo ili waweze kuchimba na
kujipatia mahitaji yao,"alisema Pinda.
Pamoja
na mambo mengine, Waziri Mkuu Pinda aliyasema hayo baada ya kupokea taarifa
kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, Omary Mangochie iliyoonyesha, moja ya
changamoto kubwa katika wilaya hiyo ni ongezeko la migogoro ya wachimbaji
wadogo dhidi ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).
Aliwasihi
viongozi wa GGM kukubali kutenga maeneo machache ili wachimbaji wadogo waweze
kupata maeneo kwa ajili yao badala ya kuendelea kuwa na mvutano ambao umekuwa
chanzo cha baadhi ya wananchi kupoteza maisha kutokana na kuvamia kwenye maeneo
ya mgodi huo.
"Bahati
nzuri leo tumejaliwa kuwa na viongozi wa Mgodi wa GGM, niwaombe ndugu zangu
mkubali kutenga walau maeneo kidogo ambayo hamjaanza kuyachimba kutoka kwenye
maeneo yenu mnayoyamiliki kwa lengo la kupunguza migogoro isiyo ya lazima na
wachimbaji hawa wadogo,"alisema Waziri Mkuu Pinda.
Kuhusu
mabaki ya miamba, alisema Serikali inatarajia kuzungumza na wawekezaji hao ili
kuweka utaratibu mzuri wa kuyakusanya kwenye maeneo maalumu ili iwe rahisi kwa
wananchi kufika na kuyachukua kwa ajili ya kwenda kusaga na kutafuta mabaki ya
dhahabu.
Chanzo:
Mtanzania.






No comments:
Post a Comment