Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo,
Alhamisi, Septemba 20, 2012, ameweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Daraja la
Kigamboni, Dar es Salaam kwa kuwaonya watu ambao amewaeleza kuwa wanavyo
viwanda vya kutunga uongo kuacha tabia hiyo na kuelekeza nguvu kwenye
maendeleo.
Aidha,
Rais Kikwete amewahakikishia wakazi wote wa Kigamboni ambao wanaondolewa katika
maeneo yao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa daraja hilo na ujenzi wa Mji Mpya wa
Kigamboni kuwa watalipwa stahili na haki zao zote.
Daraja
hilo la Kigamboni ambalo wazo la kujengwa kwake lilibuniwa kwa mara ya kwanza
zaidi ya miaka 30, tokea mwaka 1978, wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, linajengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 214.6 na litakuwa
tayari katika muda wa miezi 36 ijayo, ingawa muda huo unaweza kupungua na
kubakia miezi 30.
Daraja
hilo ambalo litakuwa na urefu wa mita 680 linagharimiwa kwa pamoja na Serikali
na Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF ambalo litachangia kiasi cha asilimia 60
na Serikali asilimia 40.
Daraja
hilo ambalo litakuwa na jumla ya barabara za kupitisha magari sita kwa wakati
mmoja linajengwa na makampuni mawili ya China ambayo ni China Railway
Construction Engineering Group na China Railway Major Bridge Engineering
Company na mhandisi msimamizi wa ujenzi huo ni Kampuni ya Misri.
Daraja
hilo litapunguza adha ya usafiri kati ya Kigamboni na Dar es Salaam ambao kwa
sasa unategemea vivuko, ama boti ndogo, mitumbwi ama wenye magari kulazimika
kufanya mzungumo wa kilomita 52.
Kwa uamuzi wa sasa, wavuka kwa miguu ambao
watakuwa na njia maalum kwenye daraja hilo pamoja na waendesha baiskeli
watavuka bure bila malipo yoyote.
Akizungumza
kwenye sherehe hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali haiwezi kudhulumu
wananchi wake na hivyo watu wote ambao wanastahili fidia kutokana na ujenzi wa
daraja hilo na mji mpya wa Kigamboni watalipwa haki na stahiki zao.
Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake haitaruhusu mtu yoyote kuzuia ama
kuchelewesha miradi ya maendeleo ambayo inalenga kunufaisha watu wengi.
Rais
Kikwete pia amewaonya watu ambao wamelifanya suala la kutunga na kusema uongo
kama sehemu ya utamaduni wao. “Watu wana viwanda vya kuzalisha uongo.
Wanashinda wanasambaza uongo kwenye mitandao, kila mahali. Wamepata hata kusema
kuwa mimi nimemuuzia George Bush eneo la Kigamboni. Bush aje kufanya nini
Kigamboni?”
Rais
pia amesema kuwa wapo watu ambao hawapendi maendeleo ya nchi. “Wanatamani kila
siku tushindwe kuwaletea wananchi maendeleo. Lakini watakufa kwa kihoro kwa
sababu hatutashindwa. Kila tulilosema tutalifanya, litafanyika”.
Amesema
kuwa thamani kubwa ya vyama vya siasa ni maendeleo ya wananchi. “Lakini wapo
wenzetu ambao wanaudhika wakiona maendeleo. Wanapenda hata daraja hili
lisijengwe. Leo hawatalala usingizi. Kazi ya vyama vya siasa ni kuweka maslahi
yetu sote mbele.”
Imetolewa
na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,Ikulu.
Dar
es Salaam.
20
Septemba, 2012.








No comments:
Post a Comment