Uwajibikaji mdogo na kukithiri kwa rushwa miongoni mwa
baadhi ya madiwani na watendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mpanda mkoani
Katavi ni sababu tosha inayochangia miradi mingi ya maendeleo kutekelezwa chini
ya kiwango.
Kiongozi wambio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, Honest Mwanossa alisema hayo jana mara baada ya kukagua na kukataa kuipokea baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo inapitiwa na mbio za mwenge wa uhuru mkoani humo.
Miradi ambayo aliikataa ni ile ya ujenzi wa ofisi ya Mbunge jimbo la Mpanda vijiji ambayo alidai imejengwa chini ya kiwango ambapo fedha iliyotumika haifanani na thamani ya jengo hilo.
Pia
amekosoa ujenzi wa miradi kadhaa na kutaka kasoro zilizojitokeza ikiwamo kuwa
na nyufa zinarekebishwa na wakandarasi waliotekeleza miradi hiyo haraka
iwezekanavyo.
Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge, licha ya kukataa kupokea majemgo hayo pia alimtaka mkurugenzi wa wilaya hiyo kutoa maelezo ya kina kwa nini hali hiyo inajitokeza, huku mhandisi wa wilaya akikacha msafara huo ili kukwepa hoja zilizokuwa zikimkabili kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo.
Alisema kuwa tabia ya baadhi ya watendaji kuchukua asilimia kumi "ten percent" kutoka kwa wakandarasi waliopewa zabuni imekuwa sugu kwa sasa hali ambayo inachangia miradi mingi ya maendeleo kutekelezwa ikiwa chini ya kiwango na kutofanana na fedha halisi inayotajwa kutumika.
Katika
hatua nyingine aliwataka madiwani kuacha udhaifu katika kusimamia vizuri
rasilimali fedha ndani ya halmashauri zao kwani kutofanya hivyo kunatoa mwanya
watendaji wasio waaminifu ambao sasa wamegeuka mchwa na kutafuna rasilimali
hizo kwa kutokuwa wazalendo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mwanossa aliongeza kuwa watendaji wasio waaminifu kamwe hawatafumbiwa macho kwa kuwa ndio wanaoichafua Serikali mbele ya wananchi kwa kutekeleza miradi mibovu, hivyo wanapaswa kubadilika mara moja kabla hatua za kuwashughulikia hazijaanza kuchukuliwa kwani wameanza kufahamika.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa katavi, Dk Rajab Rutengwe, akisoma taarifa ya mkoa baada ya kupokea mwenge kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ,Mhandisi Stella Manyanya katika kijiji cha Sitalike alisema mwenge wa uhuru ukiwa mkoani humo utapitia miradi 34 yenye thamani ya Sh 2,225,855,250- ambayo itakaguliwa kuwekewa mawae ya msingi , kuzinduliwa na kufunguliwa.
Alisema wananchi wamechangia Sh 398,547,241- huku Halmashauri zikiwa zimechangia Sh 1,298,842,859-, wahisani na wadau wengine wa maendeleo Sh 176,265,150- na Serikali Kuu Sh 352,200,000-.
Kwa mujibu wa Dk Rutengwe, baada ya kuhitimisha mbio zake katika mkoa wa Katavi , mwenge utakabidhiwa kwa uongozi wa mkoa wa Tabora Septemba 22, mwaka huu kijijini Ipole katika wilaya ya Sikonge.





No comments:
Post a Comment